HAJI NASSOR, PEMBA:::
VIONGOZI wa dini kisiwani Pemba, wamewakumbusha
wazazi na walezi, kuwafichua na kuwasajili watoto wao wenye ulemavu, ili
wajiunge na wenzao, kama njia ya rahisi ya kupata haki zao za msingi ikiwemo
elimu.
Walisema, wazazi na walezi
wanaowajibu wa kuhakikisha watoto wao wote wanapata haki za msingi kama elimu,
matibabu bora, haki ya kucheza ili kutanua upeo wa ufahamu wao.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi, juu ya mchango wa viongozi wa dini, katika kuihamasisha jamii ili
kundi la watu wenye ulemavu, kupata haki zao, walisema kwanza ni kuwatoa nje.
Mmoja kati ya viongozi hao
sheikh Issa Hassan Maalim wa Chake chake alisema, kumfungia ndani mtoto kwa
sababu ya ulemavu wake, ni kosa.
‘’Suala la ulemavu ni kudura
ya Muumba, sasa kama mzazi anaichukulia kama ni kosa na kuamua kumfungia ndani,
anamdhalilisha mtoto wake,’’alieleza.
Nae kiongozi wa kidini
nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Aisha Hasnuu Omar, alisema wazazi
wote wanalojukumu la kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanawapatia haki zao.
‘’Sisi wanawake kama kweli
ni watu wa huruma na tuliojaa hofu ya Muumba, tuanze kwa kuwafichua watoto wetu
na wale wa jirani wenye ulemavu, ili wapate haki zao,’’alieleza.
Alieleza kuwa, mwaka 2020
wakati wanawapitai wazazi kuwahamasisha jambo hilo, katika wilaya ya Micheweni
mkoa wa kaskazini Pemba, waliwagundua watoto watatu wenye umri tofauti, wakiwa
wamefungiwa ndani,’’alieleza.
Kwa upande wake sheikh
Othman Hassan Juma na mwenzake Issa Nassor Kassim wa Machomane Chake chake,
walisema elimu kwa wazazi bado iko chini.
Mtoto mmoja ambae sasa
anasoma darasa la sita skuli ya msingi Madungu alisema, baada ya kufungiwa
ndani kwa miaka mitano, kisha alipata msaada wa Idara ya ustawi.
‘’Watendaji wa Idara
walivamia nyumbani na kuwauliza wazazi sababu ya kunifungia ndani, wakasema
nitachekwa nje na sina kiti mwendo cha kwendea skuli,’’alisema.
Mzazi wa mtoto huyo, Iddi
Khamis Iddi, alisema baada ya kupata elimu juu ya haki za watoto wenye ulemavu,
tayari ameshamuandikisha elimu ya awali.
‘’Hata vifaa saidizi mwaka
huu mwanzoni, ameshapatiwa na sasa anaendelea na masomo, ingawa changamoto ni
miundombinu,’’alieleza.
Mratibu wa baraza la taifa
la watu wenye ulemavu Zanzibar kisiwani Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, alisema ni
kosa kisheria, mzazi kumfungia ndani mtoto wake kwa sababu ya ulemavu.
‘’Hata kama mtoto hana vifaa
saidizi vya kujifunzia, anatakiwa aende skuli na changamoto imkute akiwa kwenye
mfumo wa elimu, na sio kufungiwa ndani,’’alieleza.
Afisa Mdhamini wizara ya
elimu na Mafunzo ya amali Pemba, Mohamed Nassor Salim, alisema wizara imekuwa
na mfumo wa kuwanunulia na kuwapa bure vifaa saidizi wanafunzi wenye ulemavu.
Hata hivyo, alisema hakuna uhusiano kati ya
kutokuwepo vifaa saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu na kuwazuilia
kukosa elimu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment