NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
SHEMSA
Hakim Khamis wa Chanjamjawiri wilaya ya Chake chake, ameiambia mahakama maalum
ya makosa ya udhalilishaji ya mkoa wa kusini Pemba kuwa, mume wake hajambaka
mtoto wao wa kumlea, bali ni uongo alioutengeneza mtoto huyo.
Alidai kuwa, mtoto huyo
amekuwa muongo mzoefu na mzushi, maana siku ambayo, alidai amebakwa na mumewake,
alikuwa safarini kikazi kisiwani Unguja.
Shemsa ambae ni shahidi
nambari nne kwenye shauri linalomkabili mumewake (mtuhumiwa Said Abdalla Issa), alidai kuwa mumewa alikuwa kisiwani
Unguja kikazi siku hiyo aliyodaiwa kubaka.
Alidai kuwa, mtoto huyo
ambae ni wa kulea, amekuwa muongo na alishawahi kumsingizia jirani wao mwanamme,
kuwa alishawahi kumvulia nguo na kumuonesha sehemu zake za siri, ingawa
walipofuatilia, haikuwa sahihi.
Mke huyo wa mtuhumiwa,
alidai kuwa mtoto huyo pia alishawahi kukamatwa na barua ya mahaba, ndani ya
mkoba wake wa mabuku ya skuli, akiashiria kuwa mtoto huyo alishaanza kubadilika
kitabia zamani.
‘’Mume wangu hahusiki na
kesi hii, maana hata siku ambayo alipelekwa hospitali kwa uchunguzi mtoto huyo,
alishaoonekana kuingiliwa, ingwa sio mume wangu,’’alidai shahidi huyo.
Aidha shahidi huyo
akiongozwa na wa utetezi Abied Mussa Omar, alidai kuwa alishakanywa na mama
yake mzazi anaeishi nae kuwa, ni vyema mtoto huyo amrejeshe kwao eneo la Kiwani,
kabla hajazusha balaa jengine.
Shemsa, aliendelea
kuiaminisha mahakama kuwa, chanzo cha mtoto huyo kumtaja baba yake huyo wa
kambu (mtuhumiwa), kuwa alimbaka, ni baada ya kumuadabisha kwa bakora.
‘’Ni kweli siku moja, baada
ya kuwaita wenzake na kukila chakula chaote cha ndani, baba yake wa kambu
(mtuhumiwa), alimchapa bakora, na kisha mtoto huyo kuahidi kumlipizia babayake
huyo kwa kipigo hicho,’’alidai shahidi huyo.
Aidha shahidi huyo alidai
kuwa, kuanzia hapo, ndio baada ya siku chache, alifikiwa na Polisi kutoka
wilaya ya Chake chake, wakimuelezea kuwa, mume wake anakabiliwa na kesi ya ubakaji.
Baada ya kumaliza kutoa
suahidi wake, Hakimu wa mahakama hiyo Muumini Ali Juma, alimpa nafasi wakili wa
serikali, Ali Amor Makame, kumuuliza maswali shahidi huyo wa upande wa utetezi.
‘’Unakumbuka kuwa, awali
ulikwenda kituo cha Polisi kumlalamikia mume wako (mtuhumiwa), kwa kosa la
kumbaka mtoto wenu wa kulea,’’alihoji Wakili huyo.
‘’Utakubaliana na mimi kuwa,
baadae wewe tulikuletea wito wa mahakama, kuja kutoa ushahidi, juu ya
malalamiko yako na ulishindwa kuja, na leo uko umegeuka unamtetea mume wako,’’aliuliza
Wakili wa serikali.
Hata hivyo, wakili huyo
alimuuliza shahidi huyo, ikiwa anakumbuka vyema kuwa, mtoto wake huyo,
alimpeleka hospitali kwa ajili ya uchunguuzi, mara baada ya mumewake kumbaka.
Hata hivyo shahidi huyo wa
upande wa utetezi, ambae ni shahidi nambari nne, aliyakana maswali yote,
aliyoulizwa na wakili wa serikali.
Baada ya maelezo hayo, wakili
wa upande wa utetezi Abied Mussa Omar, alimueleza Hakimu Muumini Ali Juma kuwa,
ameshafunga ushahidi wake, na kuiachia mahakama iendelee na taratibu nyingine.
Hivyo, hakimu huyo
aliliahirisha shauri hilo hadi Novemba
28, mwaka huu, kwa ajili ya kusomewa hukumu ya mtuhumiwa huyo, ambae yuko
nje kwa dhamana.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa
huyo Said Abdalla Issa mkaazi wa Kengeja na Chanjamjawiri wilaya ya Chake chake,
alidaiwa kumbaka mtoto wake wa kulea, tokea mwaka 2019.
Kufanya hivyo ni kinyume, na
kifungu 108 (1), (2) (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6
ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment