IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA
“KESI ya mtoto wangu mwenye ulemavu wa matamshi, ilifutwa mwaka jana mahakamani, kwa sababu ya siuntafahamu ya eneo alilobakwa ni tofauti na walilolitaja mashahidi,’’anasema mama wa mtoto huyo.
Mama huyo mkaazi wa Pujini dodo wilaya ya Mkoani, anasema tokea asili mtoto wake anaulemavu wa akili na matamshi, sasa kasoro ya kumbu kumbu yake ndio chanzo cha kukosa haki zake.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii, anasema bado watu wenye ulemavu, mara baada ya kubakwa imekuwa ni shida mpya kuvifikia vyombo vya sheria.
Anasimulia kuwa, baada ya mtoto wake kubakwa na Abdalla Khatib Abdalla miaka 25, mwanzoni mwa mwaka 2018, kesi hiyo ilichukua tena miezi minane, hadi kufika mahakamani.
“Nilipofika kituo cha Polisi Chake chake, kwanza sikupata ushirikiano, na walionipokea wakaniambia kesi yangu inaweza kuwa ngumu mahakani, kwa sababu hakuna mkalimani,’’anasimulia.
Anasema ingawa askari hao wenyewe kwa wenyewe, walipingana na kuelezana kuwa, hiyo wao sio kazi yao, na walitakiwa wanichukue maelezo.
Alipelekwa kwenye dawati la jinsia la Polisi la wanawake na watoto, na kuchukuliwa maelezo, ingawa shida ya kwanza ilikuwa wakati siku mbili alipotakiwa kumfikisha mtoto wake kwa mahojiano.
Kwa siku hiyo, anasema mtoto wake alieleza kila kitu na kama alivyofanywa na mtuhumiwa, ikiwa ni pamoja na kumfanyia udhalilishaji kichakani chini ya Mwembe.
Anasema baada ya kuchukuliwa maelezo hayo, kesi yake alikaa miezi mitatu bila ya kufikishwa mahakamani na alipoulizwa, aliambiwa asubiri upelelezi ukamalike.
Ilipofika Disemba 2019, anasema alipata simu kuwa, anatakiwa kufika mahakama ya Mkoa Chake chake na kwa mara ya kwanza kesi yake ilisomwa.
Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huo huo, aliatakiwa kumpeleka mtoto wake mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi, na akawaeleza kuwa anatabia ya kupoteza kumbu kumbu.
“Ni kweli siku aliyotoa ushahidi wake, alisema alifanyiwa tendo hilo ndani ya nyumba, ingawa Polisi alitaja kwenye kichaka,’’anasimmulia mama huyo.
Kisha kesi hiyo mwishoni mwa mwaka 2020, Mahakama ya Mkoa Chake chake, ilimuachia huru mthumiwa huyo kwa sababu ya mkanganyiko wa eneo alilodaiwa kubakwa.
Lakini hata dada wa mtoto wa miaka 16 mwenye ulemavu wa matamshi, wa Wawi Chake chake, anasema baada ya mdogo wake kutoa taarifa za kubakwa na kijana Shaaban Mohamed Issa miaka 35, kwanza alichelewa kutafutwa.
“Familia ilikuwa inaniambia mtoto wenu mwenye ulemavu hawezi kushinda kesi dhidi ya mtoto wangu, kama mnamtafutia muume kwa nguvu sio mtoto wetu,’’anadai kuelezwa.
Alipofika kituo cha Polisi Juni 12, mwaka 2020 alielezwa kuwa, wahusika wa kesi hizo hawapo, hivyo alirudi na kwenda siku ya pili.
“Siku ya pili nilifika saa 1:00 asubuhi, lakini huduma niliipata majira ya saa 8:00 mchana maana wanasema walikuwa kwenye kikao, na siku hiyo nilichukuliwa maelezo nusu tu,’’anasimulia.
Siku tatu baadae, alipata tena wito wa kutakiwa kufika kituo cha Polisi akiwa na mdogo wake, na kuchukuliwa maelezo hadi na walipomaliza walirejea nyumbani.
Alipotaka kujua ikiwa mtuhumiwa wameshamkamatwa walimueleza kuwa bado, ingawa alipewa namba za simu za Polisi, ikiwa atamuonea apige simu.
“Haya kama nitamuona kama simu yangu ikiwa haina salio je…nifanye nini,’’aliuliza kituo cha Polisi na kujibiwa kuwa kama anataka haki ya mdogo wake, simu isikauke salio.
Wiki tatu baada ya kumuona mtuhumiwa akiwa anatembea mitaani, alifika tena kituo cha Polisi na kuwaeleza, na hapo alitaka kupewa hati ya kumkamata na kuikataa.
“Kwa uchungu…. wale askari walinataka kunipa hati ya kumkamata ‘warantee’ lakini nikawaambia mimi sina uwezo wa kumkamata mtuhumiwa hiyo ni kazi yenu,’’alisema.
Alitamani kuachana na kesi hiyo, ingawa alipata msaada kwa jumuia za watu wenye ulemavu na kutakiwa kuendelea kuitafuta haki ya mdogo wake.
Mwezi Novemba mwaka jana, baada ya kukaa kwa muda na ukimnya ukitawala, alifika tena kituo cha Polisi na kuwaeleza kuwa mtuhumiwa yupo mtaani.
“Mara hii nilambiwa gari haina mafuta, hivyo kama anaweza kuchangia itakuwa kazi rahisi kumfuatilia mtuhumiwa huyo kijiji cha Wawi, ingawa alishindwa kutoa fedha hizo,’’analalamika.
Wiki moja baada ya kurudi kituo cha Polisi, alisikia kuwa tayari mtuhumiwa ameshakamatwa, na alipofuatilia alilithibitisha hilo na kisha kupelekwa rumande.
“Kpindi cha Corona nasikia yalipata dhamana, lakini katoroka hadi leo hii, na kesi yangu sijui ilipofika maana sijawahi kuitwa mimi wala mdogo wangu mwenye ulemavu hadi sasa,’’anasema.
Kadhia kama hii hata mazazi wa mtoto mwenye ulemavu wa viungo, aliyepewa ujauzito na askari wa chuo cha Mafunzo kambi ya Kengeja wilaya ya Mkoani, nae analia na vyombo vya sheria.
Mtuhumiwa huyo askari wa chuo cha Mafunzo Suleyom Idd Saleh miaka 30, alimpata ujauzito mtoto huyo mwenye ulemavu wa viungo na akili.
Baada ya tukio, wazazi wanadai kuliitishwa vikao vya siri, baina ya upande mmoja wa familia na wakuu wa kambi ya Kengeja, ili kesi hiyo isipelekwe kwenye vyombo vya sheria.
Baba wa mtoto huyo, alishafuatwa zaidi ya mara mbili na upande wa kambi ya Chuo cha mafunzo, kwamba kesi hiyo iishie kwa wao kufunga ndoa.
Ingawa baadae kesi hiyo ilifikishwa mahakamani, miezi mitatu baada ya kubainika na ujauzito wa miezi sita, kisha alijifungua na mtoto kupita.
Njama za mtuhumiwa huyo za kutaka kufunga ndoa na mwanamke huyo mwenye ulemavu wa viungo, ambae pia alikuwa jirani yake, zilifanikiwa na sasa wanaishi mke na mume.
Mwanasheria kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba Ali Amour Makame, aliyekuwa akiisimamia kesi hiyo, anasema imeshafutwa mwishoni mwa mwaka jana.
“Kesi ya yule mwanamke mwenye ulemavu ambae alipewa ujauzito na askari wa chuo cha mafunzo Kengeja, imeshafutwa maana waliitwa wazazi zaidia ya mara tano wafike mahakamani kutoa ushahidi, lakini hawakutokeza,’’anabainisha.
VYOMBO VYA SHERIA
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba Richard Tedei Mchomvu, anasema changamoto kubwa kwa wenye ulemavu baada ya kudhalilishawa, ni kukosa taaluma ya kuyaripoti matendo hayo.
Anasema, madawati ya jinsia ya Jeshi la Polisi, ni kweli wengi wao hawana uwelewa kuwasiliana na wenye ulemavu wa mfano wa usikivu au matamshi, ingawa wamekuwa wakisaidiwa na jamaa zao.
Hakimu wa mahakama ya watoto Pemba Luciano Makoye Nyengo, anasema changamoto inayojitokeza hadi kesi za watoto wenye ulemavu, kutofikia pazuri ni changamoto ya ushahidi.
“Ni kweli kwa hatua za awali, wanapohojiwa kituo cha Polisi huwa ndugu na jamaa zao wanasaidia kukamilisha maelezo ya mwanzo, lakini kisheria hawaruhusiwi kufika tena mahakamani,’’anafafanua.
Luciano anabinisha, kuwa sheria haimtambui mkalimani wa awali aliyesaidia kutoa maelezo kituo cha Polisi, na kisha kufika mahakamani, ikihofiwa kuegemea upande mmoja.
WANAHARAKATI
Hidaya Mjaka Ali, anasema sababu kuu ya watu waliobakwa na kutovifikia vyombo vya sheria, ni kutawala kwa rushwa kwa baadhi ya vyombo vya sheria.
Suleiman Mansour, anasema watoto wenye ambao wanabakwa hukumbana na kuzungurukwa na vikwazo, ikiwa ni pamoja na nenda rudi ya kila siku ya kituo cha Polisi.
WALIOFANIKIWA KESI ZAO KUFIKA MAHAKAMANI
Mzazi wa Kengeja wilaya ya Mkoani, alisema baada ya mtoto wake wa miaka 15 kubakwa, alifuatilia kwa muda siku nne kituo cha Polisi Kengeja na kumfuata kamanda wa Polisi mkoa mara tatu.
“Nilikaa kwa muda mrefu, kesi yangu haijafikishwa mahakamani, lakini sikukaa tu nilifuatilia kituo cha Polisi na kisha nilipoona haijafikishwa mahakamani, nilikwenda kwa kamanda wa mkoa,’’anasema.
Hata mzazi wa Wambaa ambae mwaka 2019 mtoto wake alibakwa, anasema alihamia kituo cha Polisi Mtambile hadi pake mtuhumiwa alipokamatwa.
“Mwaka huu mwanzoni, mshitakiwa ameshafungwa miaka saba, na alitulipa fidia ya shilingi 200,000 lakini hadi kufanikiwa hilo, nilikumbana na vikwazo, ikiwa ni pamoja na nenda rudi,’’anasema.
NINI KIFANYIKE
Asha Said Omar mwenye ulemavu wa viungo wa Mchanga mdogo, anasema ili kesi za watoto weye ulemavu zifikishwe kwenye vyombo vya sheria, ni vyema kuanzishwa madawati ya jinsia ngazi ya jimbo.
Omar Mjaka Ali wa Vitongozji anaona lazima kuwe na askari maalum wanaofuatilia kesi za udhalilishaji za watoto wenye ulemavu, ili kuwapunguzia vikwazo, wakati wanapofuatilia vyombo vya sheria.
Aliyekuwa Mwanasheria dhamana ofisi ya DPP Ali Rajab Ali, anasema, haki hutafutwa, hivyo wazazi na walezi waendelee kupambana na changamoto zilizopo.
SHERIA NA MIKATABA YA WATU WENYE ULEMAVU
Sheria ya watu wenye ulemavu nambari 9 ya mwaka 2006, kifungu cha 19 (a) na (b) kimeanisha haki ya kupata lugha ya alama bila ya malipo, huduma za kutafsiri, maandishi na nukta nundu.
“Watu wenye ulemavu pia wanahaki kuwa na msaidizi ndani ya mahakama na wakati wa mwenendo wa kesi kupewa msaada wa kisheria bila ya malipo,’’kimefafanua kifungu hicho.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu weye ulemavu, Ibara ya 5 imechambua usawa na kutogaliwa mbele ya sheria, kwamba watu wote wako wanaulinzia sawa.
Mwisho
Comments
Post a Comment