NA HAJI NASSOR, PEMBA
KAMATI ya Maendeleo ya kijiji cha
Mtega shehia ya Wawi wilaya ya Chake Chake, imeahidi kuwachukulia hatua za
kisheria, wananchi wote wenye tabia ya kuchimba mchanga kwenye barabara yao,
iliyoingia kijijini kwao.
Kauli hiyo
imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Khamis Haji, alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa habari hizi, juu ya tabia iliyojitokeza ya uchimbaji mchanga na
kusababisha mashimo kwenye barabara hiyo.
Alisema,
waligundua hilo baada ya kuitembelea barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 2.5,
ambapo alisema waligundua mashimo yenye kina kirefu, ambayo yanaweza
kuhatarisha uimara na uendelevu wa barabara hiyo.
Mwenyekiti
huyo alisema, lazima wawachukuliwe hatua za sheria, ambao watawakamata wakiichimba
barabara hiyo kwa kuchukua mchanga, kwa ajili ya ujenzi.
“Baada ya
hivi karibuni kuitembelea barabara hii nikiwa na wajumbe wa kamati hii,
tulikuta vishungu vya mchanga pembezoni mwa barabara yetu, na kwamba wapo
wanaoichimba kwa maslahi yao,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Mwenyekiti huyo alisema, ni vyema kila mmoja anayetumia barabara hiyo,
kuwa mlinzi kwa wananchi wanaoichimba barabara hiyo, kwani inapoharibika athari
yake huwa kwa wote.
Nae Makamu
Mwenyekiti wa kamati hiyo Omar Mohamed, aliwataka wale ambao hawajamaliza michango
yao, kuharikisha kufanya hivyo, ili zipatikane fedha kwa ajili ya ununuzi wa
kifusi.
Alisema,
waliamua kupanga mikakati ya kuchangisha fedha kwa kila nyumba shilingi 50,000
ili zipatikane kwa ununuzi wa kifusi ikiwa hatua kuikoa barabara hiyo.
“Kwa wale
ambao bado wanasua sua kwenye michango, lazima wajikaze, maana msaada wa kwanza
kwa ujenzi wa barabara hii ni wananchi wenyewe, na kisha ndio tutafute
wafadhali wengine,,’alieleza.
Nao mjumbe
wa kamati hiyo ya maendeleo, Rashid Khamis Mussa na Khalfan Khamis, waliwaomba
wabunge na wawakilisha kuwasaidia kifusi au fedha taslimu kwa ajili ya kuiokoa
barabara hiyo.
Walisema,
kama wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, basi ni vyema wakajitokeza na
kuwasaidia kifusi au rasilimali fedha, ili waondokane na ubovu wa barabara yao.
Baddhi ya
wananchi wanaotumia barabara hiyo, wameahidi kuwaelimisha wenzao, juu ya kuacha
kuchimba mchanga kwenye barabara hiyo, na watakapowakamata watawafikishwa mbele
ya kamati.
Khadija Omar
Said na Ismail Haji waliiomba kamati hiyo, kufanya ziara ya mara kwa mara
kwenye barabara hiyo, ili kusaidiana nao, kwa vile baadhi ya wachimbaji mchanga
wameshakuwa wasugu.
Nae Afua Ali
Bakari, alisema wapo baadhi yao wamekuwa wakitumia hata gari za Ng’ombe nyakati
za usiku wakati wanapochimba mchanga kwenye barabara hiyo.
Mhandisi
ujenzi wa barabara kutoka wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
kisiwani Pemba Khamis Massoud, aliutaka uongozi wa Kamati hiyo, kujitolea
usafiri wao na kuchukua kifusi kwenye kware zao.
Alisema, kwa
sasa gari zao za kusambaazi kifusi zinaendelea kutumika kwenye ujenzi wa
barabara mbali mbali, hivyo itakuwa vigumu kutumika sehemu nyingine na ambayo
haina dharura.
“Sisi baada
ya kupokea maombi yao kutaka kifusi, tumeshawaruhusu wakachukue kifusi, kama ni
Vitongoji au Pujini, lakini lazima wawe na gari zao maana za kwetu, zina kazi
maalum,’’alisema.
Barabara
hiyo yenye urefu wa kilomita 2.5 ambayo imeanzia kambi ya mwanzo wa Jeshi la
wananchi wa Tanzania Wawi na kuishia tawi la zamani la CUF, imeasisiwa na
wananchi wa kijiji cha Mtega shehia ya Wawi miaka 15 iliyopita.
Ambapo
uongozi wa kijiji hicho, tokea mwaka 2018, ulitangaaza kupokea michango ya
wastani wa shilingi 50, 000 kwa kila nyumba, kati ya nyumba 80, ili wajipatia
shilingi milioni 4 ingawa hadi sasa wameshakusanya shilingi 1,000,000.
Mwisho
Comments
Post a Comment