NA HAJI NASSOR, PEMBA
MJASIRIAMALI wa mboga na matunda ya biashara ikiwemo ndimu, Mkubwa Ali Mkubwa wa Vitongoji wilaya ya Chakechake Pemba, amesema anawashangaa vijana wanaopanga foleni kusubiri ajira ya serikali, na kukipa mgongo kilimo.
Alisema huu sio wakati kwa vijana kupanga foleni kwenye ngazi za maofisi ya serikali, kwa kusubiri ajira zisizotosha, na badala yake wakijpanga vyema kwenye kilimo, wanaweza kupata mafanikio ya haraka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi shambani kwakwe Makaani Shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake, alisema hakuna serikali inayowatosheleza wananchi wake kiajira, hivyo ni vyema kwa vijana wakajikusanya ili kuendesha kilimo.
Alisema kwenye kilimo sifa yake kubwa hakuna kusubiri mwisho wa mawezi matumizi yake, bali ni wakati wowote, baada mazao kupevuka, jambo ambalo ndio njia rahisi ya kupungaza ukali wa maisha.
“Mimi hata leo ukiniambia niache kilimo niendele serikali, wala sikukilizi, maana sasa ndimu, tungule, vitango, vitunguu maji, mchicha na migomba ndio utajiri wangu’’,alifafanua.
Mjasiriamali huyo anaemiliki shamba la mchanganyiko wa mboga mbali mbali , lenye ekari zaidi ya mbili na nusu, alieleza kuwa, kwa msimu mmoja wa uvunaji, hujipatia wastani kati ya shilingi milioni mbili (2,000,000), na kwa msimu wa mwaka huu malengo yake yamepata mtikisiko kutokana na soko kuanza kupwaya.
Alieleza kuwa, kwa sasa ndimu zenye thamani ya zaidi ya shilingi 600,000, vitango vyenye thamani ya shilingi 200,000, tungule zenye thamani ya shilingi 800,000 na gunia mbili na nusu za vitunguu maji anavyotarajia kuvuna, soko lake anamashaka nalo.
“Unajua kila msimu wa uvunaji kipindi kama hichi, huwa tayari wateja wameanza kujitokeza hadi kufuata bidhaa huku kwenye shamba, lakini kwa msimu huu, mambo sio mazuri na hasara iko njiani kunifika,’’alieleza.
Katika hatua nyengine, mjasiriamali huyo ameziomba taasisi zenye kutoa mikopo kwa wafanyabiashara, kuacha kuweka riba, kwani kufanya hivyo, huwakosesha wengine haki hiyo.
Hafife Juma Hamad aliejiriwa na mjasiriamali huyo alisema, maisha yake yamebadilika kiasi, hasa kwa vile hana wasiwasi wa kusaidia familia yake kifedha.
“Hukaa wee, lakini kisha hulipwa kati ya shilingi 150,000 hadi shilingi 200,000 ambapo malipo hayo hutegemea na mavuno yalivyo, ambpo kwangu mimi hii ni faraja,’’alifafanua.
Nae Saada Ali Mkubwa, alisema mjasiriamali huyo, kwake amekuwa mkombozi, kutokana na kumsaidia kupata ajira kwenye sekta ya kilimo.
“Mimi hapa nipo kiajira, lakini pia najifunza jinsi ya kilimo cha kisasa kupitia mjasiriamali huyu, lakini soko ndio tatizo, maana mboga zisiponunuliwa na sisi hata kipato chetu hushuka,’’alifafanua.
Aidha waajiriwa hao wamesema malengo yao ya baadae sio kubakia hapo, bali na wao ni kuanzisha mboga mboga kama hizo, kwa vile wamekuwa pia wakipata ujuzi wa namna bora ya kilimo.
Sheha wa shehia ya Vitongoji Ayoub Suleiman Salim, amemtaka mjasiriamali huyo, kujiunga na vikundi vya saccos, ambavyo hutoa fedha bila ya riba.
“Kama anaona mabenki na taasisi nyengine zinatoa mikopo yenye riba, basi ajiunge na vikundi vya kuweka hisa, wapo wengi waliochukua mikopo mpaka shilingi 800,000 hadi shilingi milioni moja na sasa wako vizuri,’’alifafanua.
Mjasiriamali huyo alieacha kazi ya ujenzi wa nyumba na kujiingiza kwenye kilimo cha mboga mboga, alianza na mtaji wa shilingi 500,000 na kwa sasa ameshachimba kisima na kwa mwaka wa kwanza alipata mvuno ya shilingi 600,000 mvuno wa pili shilingi milioni mbili, na mvuno wa tatu alipata shilingi 1,000,000 na kwa sasa anategemea kuvuna mazao yenye thanani ya shilingi 1,000,000 ingawa inategemeana na soko.
Tayari serikali ya awamu ya nane, imetenga shilingi bilioni 81 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali kadhaa wa Zanzibar, ili kuinua mitaji na vipato vyao.
Comments
Post a Comment