NA HAJI NASSOR, PEMBA
IDARA ya Katiba na
Msaada wa Kisheria Zanzibar, imeshauriwa kuandaa mazingira rafiki, ili
kuwafikia watu wenye ulemavu kuwapa elimu, ushauri na msaada wa kisheria.
Ushauri huo umetolewa na msaidizi wa sheria kutoka wilaya ya Micheweni
Saleh Hamad Juma, alipokuwa akichangia taarifa ya maadhimisho ya tatu ya wiki
ya msaada wa kisheria kwenye mkutano uliofanyika Gombani.
Alisema, kundi la watu wenye ulemavu na hasa kwa mazingira
yao, wamekuwa wakisahauliwa mno na hawafikiwi ipasavyo na msaada, ushauri wa sheria.
Alisema, suala la kuitisha mkutano pekee kwenye maeneo husika
bila ya kuzingatia mazingira rafiki ya watu wenye ulemavu, wataendelea kukosa
msaada wa kisheria, ambao ni haki yao.
Kwa upande wa Mjumbe wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar Ayuoub Juma Shaame, aliishauri Idara hiyo kuweka wakalimani maalum, kwenye wiki
ya msaada wa kisheria, ili kuwasaidia viziwi.
“Pamoja na kuimarisha mazingira kwa ajili ya watu wenye
ulemavu, lakini msisahau kuweka wakalimani kwenye shughuli za utoaji wa msaada wa
kisheria, ili wenzetu viziwi wapate taarifa,’’alishauri.
Mapema akifungua mkutano huo wa robo mwaka wa kuratibu
masuala ya msaada wa kisheria, Afisa Mdhamini wizara ya Katiba na sheria Pemba
Halima Ali Khamis, alisema Idara hiyo, imekuwa mstari wa mbele kuwafikia
wananchi.
Alisema Idara hiyo kupitia Mkurugenzi wake Hanifa Ramadhan
Said, imekuwa ikiyafikia makundi kadhaa ndani ya jamii, kuwapa ushauri na msaada
wa kisheria bila ya malipo.
“Lazima nimpongeze Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na msaada wa kisheria, amekuwa halali ili kuhakikisha jamii inapata haki zao za kisheria,’’alieleza.
Mapema Mkurugenzi wa Idara hiyo Zanzibar Hanifa Ramadhan
Said, alisema awali mkutano kama huo, ulikuwa ukifanyika Unguja pekee, ingawa
kwa mwaka huu unafanyika na Pemba.
Alisema, Idara imekuwa ikifanyakazi kwa karibu mno na
wasaidizi wa sheria waliopo kila jambo la uchaguzi, ili kuhakikisha jamii hailalamikii kwa
kukosa uwelewa wa msauala ya kisheria.
Akiwasilisha taarifa ya maadhimisho ya tatu ya wiki ya msaada
wa kisheria, Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na msaada wa sheria Pemba
Bakar Omar Ali, alisema kwa upande wa Pemba wiki hiyo ilifanyika Micheweni.
Alisema wananchi 3,160 walifikiwa na elimu ya msaada wa
sheria, wakiwemo wanawake 1, 483 na wanaume 1, 677 ambapo hilo ni baada ya
Idara, kushirikiana na wanasheria wengine katika kambi hiyo.
Akiwasilisha muhutasari wa rasimu ya ripoti ya mwaka msaada
wa kisheria ya mwaka 2020/2021, Afisa Sheria wa Idara hiyo Zanzibar Ali Haji Hassan,
alisema wananchi 4,339 walifikiwa kupata msaada na ushauri wa kisheria
Zanzibar.
Alisema kwa mwaka 2019/2020 waliofikiwa ni wananchi 1,346
ambapo inaonesha utendaji kazi wa kukua hasa kutokana na ushairikiano uliopo, wa
watoa msaada wa sheria na wasaidizi wa sheria.
Wakichangia katika mkutano huo, washiriki ambao ni watoa
msaada wa kisheria na wasaidizi wa sheria, walisema bado elimu zaidi
inahitajika kwa jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzbar ‘ZLSC’
tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, alisema kazi inayofanywa na Idara hiyo ni kubwa,
na inafaa kuungwa mkono.
Nae Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya
Chake chake ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema wakati umefika kwa wiki ya
msaada wa kisheria, kufikia kila wilaya.
“Hata kama ile siku ya wiki ya msaada wa kisheria itakuwa ni
siku tatu, tuangalie uwezekano kila wilaya, wananchi wafaidike nayo kuliko
kwenda wilaya moja pekee,’’alishauri.
Mkutano huo ulifungwa na Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na msaasa wa kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan, aliyesisitiza ushirikiano baina ya watoa msaada wa sheria, wasaidizi wa sheria na viongozi wengine.
Mwisho
Comments
Post a Comment