WAHAMASISHAJI jamii wa wanawake kudai haki zao na kushiriki katika masuala ya uongozi Pemba wameitaka jamii katika Kisiwa cha Kojani Wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba kutoa kipaumbele kwa watoto wa kike kwa kuwajengea uwezo wa kushiriki kugombania nafasi mbalimbali za uongozi mapema ili kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadae nchini.
Wakizungumza na wanajamii wakati wa mkutano wa wahamasishaji hao ambao ni utekelezaji mradi wa kuhamasisha wanawake kudai haki zao na kushiriki katika masuala ya uongozi unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway, walisema ni vyema kwa jamii hasa akina mama kuwashajihisha watoto wao wa kike kugombania nafasi mbali mbali za uongozi hata wakati wakiwa bado Skuli.
Husna Ali Said, Mwenyekiti wahamasishaji jamii Wilaya ya Wete alieleza kuwa kwa muda mrefu wanawake Zanzibar wamekuwa nyuma katika nafasi za uongozi kutokana na kukosa misingi sahihi inayowaandaa kuwa viongozi mapema na hivyo kupelekea mambo yao mengi kutolewa maamuzi na wanaume.
Kutokana na hilo aliwataka wanawake na jamii ya kisiwa hicho kujenga utaratibu wa kuwatia moyo na kuwahimiza watoto wao kuwa wanaweza kuwa viongozi tangu wakiwa wadogo ili wakue na ujasiri na sio kuwakatisha tamaa.
Aidha mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa suala la uongozi sio lazima kusoma sana bali linahitaji mtu kujitambua na kutumia haki yake kusimamia maadili ya jamii pamoja na kufanya uchambuzi sahihi kwa yale ambayo anayawakilisha kwa jamii husika.
Alieleza, "ukifuatilia kwenye taasisi na hata jumuiya mbalimbali ambazo zimeanzishwa katika jamii zetu hata kama idadi kubwa ya wanachama watakuwa ni wanawake lakini utakuta nafasi kubwa pekee ambayo mwanamke anapata kuiongoza ni mshika fedha tu, jambo ambalo sio sahihi hata kidogo."
Maalim Mohammed Said ambae ni mhamasishaji jamii alifahamisha kuwa iwapo watoto wa kike watajengewa uwezo kwa kuandaliwa kuwa viongozi tangu wakiwa wadogo itawasaidia kujenga ujasiri wa kusimama kutetea haki zao katika kila nyanja na kuondoa mfumo dume.
Nao baadhi ya akinamama walioshiriki mkutano huo walisema changamoto kubwa ambayo ipo katika Kisiwa Cha Kojani ni wanawake wengi ambao wanaishi huko hawajui kusoma wala kuandika na hivyo kupelekea ugumu kwao kushiriki katika mambo ya uongozi.
"Uongozi tunautaka sana, lakini kikwazo chetu sisi wanawake wengi wa hapa Kojani hatujui kusoma wala kuandika sasa twakwazika sana kwasababu huwezi kuongoza watu ikiwa wewe mwenyewe hujui hata kushika kalamu," walieleza.
Kufuatia mkutano huo, wahamasishaji jamii wameahidi kufikisha changamoto zilizobainishwa na wananchi hao kwenye ngazi husika ili kuzitaftia ufumbuzi na kufanikisha lengo la upatikanaji wa haki za Wanawake katika ngazi mbalimbali kwenye jaamii.
Comments
Post a Comment