IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA
WATU wenye ulamavu kisiwani Pemba, wamepongeza hatua ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutaka kuvikodisha visiwa vinane vidogo vidogo, kwa dola za Marekani milioni 271.5 wastani wa shilingi bilioni 600.357.
Wamesema hatua hiyo inaonesha, nia ya dhati ya serikali ya kutaka kuwainua wananchi kiuchumi, jambo ambalo walisema ni vyema nao, wakaangaliwa kunufaika na uwekezaji huo.
Walieleza kuwa, hatua hiyo ya serikali inayoongozwa na Dk. Mwinyi, wameifurahia mno, na sasa kilichobakia kwa watendaji sekta ya utalii, kuweka mazingira rafik kwa ajili yao.
Wakizungumza na mwandishi wa habari, kufuatia kusambaa kwa taarifa ya uwekezaji ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ‘ZIPA’ Sharif Ali Sharif, walisema hofu yao, ni kusahauliwa katika uwekezaji huo.
Mmoja kati ya hao Hidaya Mjaka Ali, alisema uwekezaji huo ikiwa watashirikishwa kikamilifu, unaweza kuwa na maana pana kwao, ikiwa ni pamoja na ajira za kudumu.
“Sisi watu wenye ulemavu mara zote tumekuwa tukisahauliwa kushirikishwa katika utekelezaji wa sera mbali mbali, na kisha hukumbana na changamoto kama za miundombinu rafiki,’’alieleza.
Mjumbe wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Bimkubwa Mohamed Ali, alisema watu wenye ulemavu na hasa wanawake, wamekuwa wakiandamwa na changamoto ambazo zinaweza kuzuilika kabla.
“Hatua ya Dk. Mwinyi mpaka kuwashawishi wawekezaji na kuonesha nia ya uwekezaji ni nzuri, lakini lazima sera ziwalazimishe wawekezaji, kutushirikisha na sisi watu wenye ulemavu,’’alishauri.
Mkurugenzi wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar mwalimu Ussi Khamis, alisema bado sheria nambari 9 ya mwaka 2006 ya watu wenye ulemavu Zanzibar, haijatekelezwa ipasavyo, hasa eneo la miundombinu.
‘’Kuanzia vifungu vya 6 hadi cha 8 vya sheria hii, inafafanua suala la ajira kwa watu wenye ulemavu, sasa kama haki au fursa katika ajira za kitaifa watu wenye ulemavu, wasiaachwe nyuma,’’aliependekeza.
Mdhamini Kamisheni ya Utalii Pemba Hamad Amin, amesema watu wenye ulemavu, wana haki sawa na wengine, na niwakati nao kujipanga, ili kunufaika na uwekezaji huo.
“Kundi la watu wenye ulemavu, halitosahauliwa katika kushirikishwa na uwekezaji wa visiwa vidogo vidogo, maana zitakuwepo ajira kwa mujibu wa mazingira yao, samba mba na ujasiriamali watanufaika,’’alieleza.
Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ‘ZIPA’ Sharif Ali Sharif, alivitaja visiwa hivyo vinane kuwa ni Changuu, kinachoekezwa kwa dola zisizopungua milioni 20 kupitia kampuni ‘Changuu Lodge Ltd’.
Kisiwa cha Bawa kitaekezwa na kampuni ‘Bawe Retreat Ltd’ kwa mtaji wa dola milioni 30, ambapo kisiwa cha Chapwani kitaekezwa na kampuni ya ‘Zan Texas Ltd’ kwa dola milioni 20 na kisiwa cha Snake dola milioni 10, kupitia kampuni hiyo.
Aidha Mkurugenzi huyo, alikitaja kisiwa cha Kwale kikiwa na uwekezaji kupitia kampuni ‘Group Eight Holding Ltd’ sawa na mtaji wa dola milioni 68.
Kisiwa cha Misali Pemba, kitaekezwa na kampuni ‘East African Investment Ltd’ kwa mtaji wa dola za Marekani milioni 83, wakati visiwa Pamunda ‘A’ na ‘B’ vimechukuliwa na kampuni ya ‘Tulia Zanzibar Beach Resort’ kila kimoja kwa dola milioni 15.
“Kisiwa chengine ni Pungume Unguja kilichopewa mwekezaji kupitia kampuni iitwayo ‘Emperial East African Ltd’ kikiwekezwa kwa dola milioni 10.5,’’alieleza Mkurugenzi huyo.
Rais wa Zanzbar Dk. Hussein Ali Mwinyi, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka 2020 hadi Disemba 2021, ZIPA imesajili miradi 120 ya uwekezaji, yenye mtaji wa dola za Marekani milioni 877.
Miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 7000, na tayari wawekezaji wameshajitokeza katika visiwa vidogo vidogo 10, vilivyotangaazwa kukodishwa.
“Miradi hiyo itakuwa ya hadhi ya juu, na sasa ‘ZIPA’ imefanikiwa kukusanya dola za Marekani milioni 14, ikiwa ni malipo ya awali kutoka kwa wawezkezaji hao,’’alifafanua.
Kuhusu uwepo wa kituo cha huduma za uwekezaji ‘one stop center’ Dk. Mwinyi alisema, zimeimarishwa na mwekezaji hupatiwa cheti cha uwekezaji ndani ya siku tatu na kibali cha kazi kwa siku moja.
Comments
Post a Comment