Skip to main content

Mafuta ya Muhina Pemba yapata soko Tanzania bara hadi Muscat Oman

 


IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTI aina mu-hina asili yake ni ukanda wa pwani, ambao ni Dar es salaaam, Tanga na Zanzibar.
Watu wengi wa ukanda huo, hukuta wamepanda uani mwa nyumba zao, ni kama sehemu ya busatani ingawa kisha hugeuzwa urembo.
Baada ya matengenezo ya hapa na pale, majani na Mu-hina hutumika kuwekwa kwenye ngozi husani mikononi na miguuni, wengine hata kwenye nywele na kucha.
Sio watu wa ukanda wa pwani pekee tu, wanaotumia hina, lakini hata nchi kama za Misri, Kaskazini mwa Afrika, Asia, Pakistani, India urembo huo ni maarufu.
Kwa watu wa ukanda wa pwani Zanzibar ikiwemo, hufanya sherehe za hinna, kwajili ya mabinti ambao hutarajia kuingia katika ndoa.
Ambapo sherehe hii huiita "Bridal heena night" ambazo awali ilikuwa ni tamaduni tu za watu fulani, lakin kwa sasa imekuzwa na kuwa ya kisasa zaidi.
MTI WA MU-HINA
Ni mdogo wa wastani, ambapo ukiutazama unafana na mti wa Mchongoma, kwa muonekano wa majani yake kama hufanana, tofauti ya majani ya hina ni ya kijani sana.
Imezoeleka kuwa, baadhi wa akinamama ambao hutoka kujifungua hupendelea kupaka hiina, kipindi ambacho wanakuwa wanatoka arobaini za uzazai.
Mu-hina hustawi na kumea zaidi kwenye kivuli na eneo lenye unyevu uyevu, na hustahamili ukame kutokana kwa vile una umbile la kama mti wa maweni.
MATUMIZI MENGINE YA HINA KWA NCHI TOFAUTI
Mjani yake huchumwa au hukatwa matawi yake, na kisha yakakaushwa juani, ambapo baadae majani hayo husagwa na kuwa laini mno.
Unga wa hina hutiwa ndani ya bakuli ukaongezwa na ndimu kisha hupakwa kwa kutumia vidole vya mikono au kijiti chemba mba.
Kwa mfano nchi ya India wanaitumia , wakiamini kuwa hina aliyopakwa bi harusi, ikichelewa kutoka huashiria ndoa ya furaha na kupendwa, na ikiwahi kutoka maana yake haitakua na furaha.
Wenzetu wa Saudia Arabia wao kule bi harusi, anapakwa na ndugu yake wa karibu, mwenye ndoa ya furaha, la si hivyo atamletea ishara mbaya.
Nchi kama Somalia, hina huvaliwa na wanawake mikononi kipindi cha harusi, Eid, Ramadhani au sherehe nyingine za kifamilia.
Huku nchi kama ya Tunisia wanasherehekea hina kwa siku saba, ambapo siku ya tatu bi harusi anavaa nguo za mila huku akipakakwa mikononi na miguuni.
Tanzania na Zanzibar hutumika kwa urembo wa bi harusi, miguuni, kucha na hata kwenye nywele, kama urembo kwa mume wake na sana sana pande za pwani.
HESHIMA YA MATUMIZI
Hina ni pambo zito sana na lenye maana kubwa kwa watu wa Pwani, kwani ni kichocheo kizito cha mapenzi, kachumbari yenye mshawasha na kipambo chenye kuchochea.
Nakshinakshi na kuonyesha furaha na pongezi, wakati mwengine huwa ni ishara ya wapendanao kuzidisha, mahaba, huba na mbolea ya mapenzi.
Hata watoto wanaopakwa hina, ingawa hawachorwi maua ya aina yoyote, bali hupakwa tu, kawaida kwenye nyayo na mikono zaidi wakichorwa machenza.
Kwa miaka zaidi ya 25 iliyopita, hata watoto wa kiume walikuwa wakipakwa mpaka siku ya ambayo wamemaliza ujando (kutahiriwa).
MBUNIFU ZULEKHA ABADAA HEMED WA MAFUTA HINA
Anasema alikaa zaidi ya mwezi mmoja, baada ya kuona wanawake wamekuwa watumiaji wa wakubwa wa hina, nae alizaa ubunifu wa kipekee.
Anasema watumiaji walio wengi, waliozea kuona matumizi ya hina yale ya kwaida, ingawa sasa alibuni kuwa ni mafuta mgando na ya maji ya mti aina ya Mu-hina
NAMNA YA KUTENGENEZA MAFUTA YA MU-HINA
Kwanza anaanza kuchuma au kukata matawi na mu-hina na kisha majani yake, kuyakausha kwa jua, ingawa anasema ukipata jua la siku moja, ni bora zaidi.
“Ukipata jua la siku moja, huwa ile rangi ya kijani iliyomo ndani ya majani, haipungui na ndio nzuri kuelekea kwenye utengenezaji wa mafuta ya majani ya mu-hina,’’anasema.
Mbunifu huyo anasema, baada ya kuwa na unga wako uliochungwa vyema na kuwa laini, mitihili ya unga wa ngano, unauweka pembeni.
Anafafanua kuwa, hapo sasa kinachofuata ni kuwa na mafuta ya chikichiki na kuyachemsha kwenye sifuria hadi yachemke sana.


Hapo unatakiwa iwe umeshaweka tayari majani yako ya miti yenye harufu kama vile mrehani, mlangi langi, mpachori, mkiluwa na kuchesha pamoja ili kupata ile harufu yake.
“Majani ya mti haya ni kwa ajili ya sasa kutafuta manukato ya mafuta yako, maana harufu ndio inayoleta utamu ndani ya mafuta haya,’’anafafanua mbunifu huyo.
Mchanganyo wa unga wa hina, mafuta ya chikichi yenye maua au majani hayo ya miti kama mlangi langi, sasa hufanyika kuelekea kuwa na mafuta na hina.
Wakati wa mchanganyo huo, ambao unafanyika unaweza pia kuingiza hata majani ya hina mbichi, ukipenda kwa ajili ya kuongeza ujani ndani ya mafuta hayo.
“Hii hina mbichi, sio lazima ukipenda tu ni kama kuvaa nguo yako safi ukaipiga pasi au ukaifukiza udi, ni mapambo tu ya mafuta yangu,’’anafafanua.
Unga wa hina sasa unapochanganya na hina na harufu ya miti ulioamua kuichagua, unarejesha tena jikoni, ingawa hapa sasa unaacha kuchemka kwa dakika zisizozidi tano.
“Hapa inabidi kwanza, uwe na moto mdogo mdogo sana, na usizidishe dakika tano mchemko wake, huku ukizingatia kama unataka mafuta ya mgando au ya maji,’’anasema.
Jengine ambalo huwa ni jambo muhimu kwa ajili ya kunogesha mafuta yako ni kuweka nta ‘be wax’ ambayo hutokana na baada ya mavuno ya asali.
“Hii nta, iko ya aina mbili, moja ‘be-wax’ na ‘micro-wax’ ambapo hapa kama ukiukosea huu wa be-wax mafuta yanaweza kuwa sio maji wa la mgando,’’anabainisha mbunifu huyo.
VIKOROMBWEZO VYENGINE VYA MAFUTA YA HINA
Mbunifu na mjasiriamali huyo wa shehia ya Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, Zulekha Abdalla Hemed anasema kila kitu kina kachumbari yake.
Kwenye mafuta haya ya majani ya mu-hina aliyoyabuni, hutia mafuta kama lozi, mzaituni pamoja na mafuta ya mkunazi na mengine ya kunukia.
Anasema hayo yote hayadhuriani na mafuta yake bunifu ya majani ya hina, bali hukoleza ladha, harufu, umadhubuti na ubora wa mafuta yake.


ALIUTOLEA WAPI UBUNIFU HUU?
Mjasiriamali huyo ambae pia ni mwalimu wa vikundi mbali mbali vya wanawake na wanaume, alisema aliuzaa mwenyewe baada ya kufikiria kwa muda.
Anasema ijapokuwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA- Pemba wamekuwa nae bega kwa bega, kwa kumuezesha utengenezaji wa bidhaa kama mikoba ya kisasa, sabuni za miche, ufugaji na kilimo cha mboga mboga.
Ubunifu huo hakuupata kwenye mitandao ya kijamii, hakuhadithiwa na mtu, hakuona pahali popote, bali aliubuni mwenyewe.
SOKO LA MAFUTA HAYO LIKOJE?
Upishi wake wa kwanza, miaka mitatu iliyopita, baada ya kubuni mafuta hayo, alianza kutumia yeye na familia yake, na walimueleza kuwa ni mazuri.
Anasema kwa siku ya kwanza, alizalisha mafuta hayo ya maji na kila aliyekuwa akiyatumia, aliona mabadiliko ya nywele zake, kama vile kutokatika na kuvimba.
Mbunifu huyo anasema kuanzia hapo, sasa alikusanya vifaa vyake vote na kuanza kazi rasmi na alibahatika nyungu yake ya pili kuipelekea Unguja kwenye maonyesho ya wajasiriamali.
“Kwenye maonyesho yale, ndio yalionifungulia soko la mafuta haya, na kuanzia hapo, sasa ikiwa mimi sina muda hata wa kunywa maji, mara napokea simu mtu anataka vichupa 40, au 50,’’anasema.
Alichogundua walio wengi wamekuwa wakiyanunua kwa ajili ya wao, nao kwenda kuyauza tena, hivyo soko lake limetanuka haraka hasa kuanzia mwishoni mwaka 2019.
Sasa mbunifu huyo anawateja na mawakala kwenye mikoa yote ya Unguja na Pemba, baadhi mikoa ya Tanzania bara kama Dar-es Salaam na Pwani na hata Maskti Oman.
“Juzi tu nimesafirisha mafuta ya zaidi ya shilingi 500,000 kuyapeleka Oman, ambapo chanzo yake kuna mtu mmoja aliyanunua kwangu na leo soko limeongezeka,’’anafanua.
Zulekha, anasema sasa mafuta hayo haangalii soko la ndani bali anafanya mbinu kuona ana wateja hadi Uengereza, Marakeni, Saudia, India kwani wapo watanzania maeneo hayo.
NAMNA YA MATUMIZI
Anasema ni matumizi yake ni kama mafuta mengine, anayonunua madukani, kwamba unapaka kwenye nywele na hata kwenye ngozi.
Anashauri kuwa, unaweza kununua mafuta ya maji kwa ajili ya kusukia kwa wanawake na kisha kununua ya mgando kwa ajili ya kulazia nywele.
“Mapambo na urembo, na urembo ni mapambo, hivyo mafuta ya mgando hasa kwa ajili ya kulazia nywele, aidha baada ya kusukwa au kuzifunga,’’anafafanua.
“Haya mafuta hata wanaume, watoto na wajawazito wanaweza kutumia, na hayana madhara maana sijawahi kupata simu kuwa yamemdhuru mteja wangu,’’anasema.
FAIDA ZA MAFUTA HAYO KWENYE NYWELE
Moja anasema kwanza ni kutoa ukurutu na uga uga ulioshinda kwenye kichwa.
Jengina faida kubwa ni kwa nywele kuwa nyeusi zenye mng’aro unaovutia na kupendeza na kuficha zile nywele nyeupe ‘mvi’ sambamba na kurefusha nywele.
“Haya mafuta yako mfano wa mbolea, maana ukiyatumia nywele humea, huondokana na kukati katika ovyo, hurefuka na kutulia kichwani kama zilizopandwa.


WATEJA WA MAFUTA HINA
Khadija Ali Yussuf, anasema sasa kwa muda mrefu hajashudia nywele zake zikibaki kwenye shanuo wakati anachozichana.
Anasema, hata kuziona tofauti kama vile kurefuka, kunenepa na kuwa laini ambayo hayo aliyaona baada ya kutumia mafuta hayo kwa siku 14 pekee.
“Kama kuna mtu mara kichwa kinamuwasha, nywele hukatika ovyo ovyo, ana ukurutu sugu, vidonda na mba, mwarubaini wa hayo ni mafuta ya hina,’’anasema.
Hasina Omar Mcha na Mwajuma Kombo Amran wa Malindi Unguja wanasema awali waliyaona mafuta hayo kwenye begi la wifi yao, mwaka mwaka jana.
“Haya mafuta yalikuwa vichupa viwili, baada ya wiki nilienda kumuomba na akanipa nikatumia nikayona pia ni dawa, kisha nikampigia simu mjasiriamali huyo na sasa natumia,’’anasema Hasina.
Hassan Mkame Omar wa Kengeja anasema awali alimnunulia mke wake, mafuta hayo ingawa siku moja nae alitumia na kuona ubora wake.
“Mabadiliko ambayo niliyaona siku hiyo moja tu kwanza, harufu nzuri, lakini wakati nakogoka nilitoka uchafu kichwani na kuanzia siku hiyo hadi leo natumia,’’anasema.
Lakini Khalfan Salim Khalfan anasema yeye baada ya kumuona mwanawe wa miaka mwili, bado ana nywele nyekundu alinunua mafuta hayo.
“Kweli baada ya kutumia mafuta haya, sasa mwanangu nywele zake zimekuwa nyeusi kama za kawaida, na wala akisukwa hazikatiki katiki ovyo,’’alifafanua.
Hivyo mteja huyo amewataka wenzake kuyatumia mafuta hayo, ambayo hayana chembe ya kemekali, na ni dawa hata kwa ngozi.
TAMWA
Afisa Uwezeshaji wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA –Pemba Asha Mussa Omar anasema wamekuwa wakiwawezesha wajasiriamali ili waweze kujitegemea.
“Hata huyo mbinifu Zulekha wa Kengeja nae ni miongoni mwa wanawake tuliowawezesha kwa njia moja ama nyingine, ikiwemo kumpeleka kwenye maonyesho na sasa ametanua soko lake,’’anasema.
Ambapo awali, walianza na uwekaji wa hisa, kisha utengenezaji wa mikoba ya ukili, na kisha kuanza kufuga kabla ya kuendesha kilimo mboga mboga na sasa akitimiza zaidi ya bidhaa saba akiwa na wenzake.
Mjasiriamali huyo, ni mmoja aliyekwisha wezeshwa na kupitia TAMWA, lakini wapo wengine zaidi ya 70 kisiwani Pemba
COSTECH
Moja ya jukumu kubwa la Tume ya Taifa ya Sayansi ya na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘COSTECH’ ni kuwaibua wabunifu hao, ili kuwapelekea watunga sera na watoa uamuzi.
Mwezi Disemba mwaka jana, Tume hiyo kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar, iliendesha mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari na watafiti, ili kutambuana.
Moja ya malengo ya mafunzo hayo, ni kuwaleta karibu waandishi na watafiti, ili kufanya kazi kwa karibu na kuwasaidia wabunifu, ili kupata taarifa za kitafiti.
Ndio maana wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Mdhamini wa Tume ya Mipango Zanzibar, kisiwani Pemba Dadi Faki Dadi, alisema tafiti zinaumuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Alisema tatfiti zilizofanywa na kisha kuishia kwenye makabati, haziwasaidii wananchi, hivyo ni wajibu wa watafiti hao, kukutana na waandishi wa habari, ili kuwawasilishia wananchi na watunga sera.
Kwenye mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Maarifa kutoka ‘COSTECH’ Dk. Bunini Manyilizu, alisema utafiti na sayansi ndio kila kitu, ikiwa taifa linataka kusonga mbele.
“Ni kweli zipo tafiti kadhaa zilizofanywa na watafiti, lakini kwa vile kuna mpasuko wa kutowasiliana na vyombo vya habari, hazisaidii, ndio maana ‘COSTECH’ ikandaa mafunzo haya,’’anasema.
Hivyo, anasema sasa anatarajia waandishi wa habari watawaibua watafiti, wabunifu, wanasayansi ili kutangaaza kazi zao.


MWISHO

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da...

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 m...

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’...

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa uf...

…….SUZA WATOA USHAURI WA ADHABU YA KUNYONGWA

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ WANAFUNZI wanaosomea uwalimu Chuo cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ kampasi ya Benjamin Wiliam Mkapa Wete Pemba, wamependekeza adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mtu atakaetiwa hatiani, kwa kosa la dawa za kulevya. Walisema, haiingii akili kuona, mahkama imeshamtia hatiani mtu kwa kukutwa na dawa za kulevya, ambazo huathiri nguvu kazi ya taifa na kisha, kupewa hukumu ya kifungo pekee. Wakizungumza leo Juni 26, 2024 kwenye kongamano la vyuo vikuu, juu ya masuala ya msaada wa kisheria, kuelekea wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar, lililofanyika Chuoni hapo, walisema wakati umefika sasa kutolewa kwa hukumu hiyo. Walipendekeza kuwa, ni vyema kwa mtu anayetiwa hatiani asibakie chuo cha Mafunzo pekee kuitia tena hasara serikali kwa chakula na wakati mwingine matibabu, wakati tayari ameshasababisha madhara, kwa vijana. Mshiriki Juma Nafasi Juma, alifafanua kuwa kama mtu ameamua kuliumiza taifa kwa kuingiza, kusafirisha, kusambaaza dawa za kulevya, hivyo n...