NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WANAWAKE
wajawazito nchini, wametakiwa kuchukua tahadhari zaidi ya kujikinga na maradhi
mbali mbali ya mripuko, ikiwa ni pamoja na matumbo ya kuharisha, kwani kinga za
miili yao hupungua nguvu kwa kule kubeba ujauzito huo.
Ushauri huo umetolewa na daktari wa afya ya uzazi kituo cha
Afya Wambaa Mkoani Mafunda Mohamed Khamis, alipokuwa akizungumza na mwandishi
wa habari hizi, juu ya tahadhari zaidi, kwa mama wajawazito kujikinga na
magonjwa ya mripuko.
Alisema, kitaalamu mjamzito na hasa ikiwa afya yake sio ya
kawaida anakuwa rahisi kukumbwa na magonjwa ya mripuko, ikiwemo kuharisha ikiwa
hatochukua tahadhari zaidi.
Alieleza kuwa, mwanamke wa kawaida ambae hana ujauzito au
mwengine yeyote, anaweza kuchelewa kidogo kuandamwa na magonjwa ya kuharisha,
hata ikitokezea amekula tunda lisilooshwa na lina bektiria.
“Ni kweli mama mjamzito anatakiwa kuchukua kinga mara mbili
ikiwemo kupenda kutembea na viatu, kulala kwenye chandarua, kunywa maji safi na
salama kwa wingi na hata kupendelea kukosha matunda kabla ya kuyala,’’alieleza.
Aidha daktari huyo alisema, kila mtu anapaswa kuchukua
tahadhari, ili kuikinga afya yake na magonjwa mbali mbali hasa ya mripuko,
lakini mama mjamzito ni zaidi.
Alielezwa kuwa, magonjwa kama ya kuharisha, corona, macho tongo,
homa ya mapafu, homa ya matumbo, kipindu pindu, kuharisha damu na hata maradhi
ya vikope, ni magonjwa yanaweza kumpata mtu yeyote.
“Mama mjamzito huwa tunawasisitiza zaidi kuchukua tahadhari
na magonjwa ya mripuko, maana akiathirika yeye, na kilichomo tumboni kuna
uwezekano mkubwa pia,’’alieleza.
Mwanaisha Makame ambae ni mjamzito alisema, tokea wiki mbili
za mwanzo baada ya kujigundua ana ujauzito, amekuwa akinywa maji yaliomchemsha,
ikiwa ni njia moja yapo ya kujikinga na magonjwa yatokanayo na maji machafu.
“Niliambiwa wakati nilipohudhuria kliniki kuwa, maji yana asilimia
kubwa ya kufuatana na magonjwa kama ya mripuko kam vile homa ya mapafu,
kuharisha damu na kipindu pindu, sasa lazima nijikinge,’’alieleza.
Nae Husna Haji Kassim wa Mtambile, alisema ijapokuwa
magonjwa kama minyoo na malaria sio ya mripuko, lakini amekuwa akijinga, ili
yasiwe sababu ya kujitokeza magonjwa mengine.
“Elimu ya kujikinga na magonjwa ya mripuko tumekuwa tukipewa
sana kila tunapohudhuria kliniki, changamoto wakati mwengine na hali ya
umaskini ndio kikwazo,’’alieleza.
Hivi karibuni, akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya
siku na unawaji mikono duniani, mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni ‘WHO’
Vendelin Tarmo Simano, alisema njia moja ya kukabiliana na maradhi ya mripuko,
ni jamii kuwa rafiki wa maji.
“Maji ndio yanayoweza kusababisha magonjwa yote tusipofyanya
rafiki, lakini pia ndio kinga ya magonjwa kama vile kuharisha, homa ya mapafu, kipindu
pindu na macho tongo kama hatukuwa makini,’’alieleza.
Hivyo, ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kutumia maji safi
na salama iwe kwa kunywa, kunawish mikono na sabuni za maji ili kujikinga na
maradhi mbali mbali ya mripuko.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Waziri wa Afya Pemba Dk. Shoka Mohamed Yakoub, alisema wizara
imekuwa ikitumia vituo vya afya na kliniki, ili kuwapa uwelewa mama wajawazito.
Nae Mkuu wa kitengo
cha Homa ya Ini, Kifua kikuu na Ukoma Pemba, Hasnuu Fakih Hassan, aliitaka
jamii kuchukua tadhari ya magonjwa ya mripuko.
Hata hivyo Mkurugenzi Kitengo
cha Elimu ya Afya Zanzibar Halima Ali Khamis alisema, miongoni mwa maradhi 10
yanayochukua nafasi ya juu Zanzibar, yale ya mripuko na yamo.
Mwisho
Comments
Post a Comment