Skip to main content

Raya Suleiman Hamad: ulemavu wa viungo haukuwa tatizo kutumikia nafasi ya uwakilishi

 


IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

“KWANGU mimi ulemavu wa viungo, haikufika siku nikaujutia, bali ulizaa fursa wakati nikiwa Mwakilishi viti maaluma kwa miaka 10,’’ ndio maneno ya Raya Suleiman Hamad Mwakilishi, mstaafu viti maaluma kwa wenye ulemavu.
Mstaafu huyo ambae anatimiza miezi 768 zenye siku 23,040 zinazounda miaka 64 ya kuishi kwake duniani tokea alipoliona jua mwaka 1957, alizaliwa kijiji cha Ole Kiyanga wilaya ya Chake Chake Pemba.
Elimu yake ya Madrassa, aliipata kijiji cha Ziwani wilayani humo, ambapo hilo lilitokana, baada ya baba yake mzazi kufariki, yeye akiwa mdogo.
Hivyo mama yake alihama Ole na kuhamia kijiji cha Mleteni shehia ya Ziwani wilayani humo, ambapo ndipo alipopelekwa madrassa kujipatia elimu ya Kur-an kama ilivyo ada kwa watoto wa kiislamu.
Mama Raya ambae ni mwenye ulemavu wa viungo, akiwa Ziwani kwa kumfuata mama yake kwa kuolewa, baada ya kuhitimu elimu hiyo, mama yake aliachika tena, na Raya alihamia shehia ya Wawi pia wilaya ya Chake chake.
Akiwa kwa bibi yake mzaa mama, alipoanza safari ya kielimu, na kuanza skuli ya msingi ya Wawi, na anasema alichelewa kupelekwa skuli kutokana na ulemavu wake.
“Unajua wazazi wakituona kama vile sisi hatuna haki ya kusoma, hivyo nilikuwa nimeshakuwa mkubwa, lakini nilipelekwa skuli kuanza darasa la kwanza, karibu nna miaka 10,’’anakumbuka.
Safari ya kusaka elimu, kwanza aliishia mwaka 1971, akiwa anayo madarasa nane kichwani mwake, na hapo alijona ni mwanamke wa shoka.
“Kwa ulemavu wangu nilionao na kufanikiwa kuhitimu darasa la nane ‘8’, mimi nilikuwa msomi mkubwa hasa kwa wakati huo,’’anafafanua.
Baada ya kuhitimu elimu yake ya darasa la nane, Raya alianza harakati za kujiendeleza, ingawa sasa alipewa mafunzo mbali mbali na taasisi za watu wenye Ulemavu Zanzibar.
Moja kati ya mafunzo ambayo yalimuezesha kuanza kujitegemea, ni elimu ya biashara ambayo, baadae alikuwa na uwezo wa kuomba mkopo kuendeleza bishara zake.
Mwaka huo huo, ndio alibahatika kufunga ndoa na mwaka mmoja baadae, alipata mtoto wake wa kwanza, na sasa akiwa nao saba.
Shughuli kubwa za Raya tokea anapotokea ni ufumaji wa makawa ya njiti, mikoba ambayo, ndio aliojiaminisha kuwa, yalimpa kipato cha kuendesha maisha yake.
“Ni kweli nilikuwa na muume, ambae alikuwa akinihudumia kila kitu, lakini mwanamke ni kujishughulisha, na mimi ndio nilivyokuwa tokea asili,’’anasema.
Maisha ya biashara yalimnogea, maana alihamia kwenye biashara ya chakula kama vile maandazi, ambayo ilitokana na mafunzo aliyopewa.
“Niliwahi kuchukua mkopo wa shilingi 75,000 ili kuendeleza biashara, na nilifanikiwa hadi kujenga nyumba yangu ambayo sasa ndio ninayoishi,’’anasema.
Lakini hata kilimo cha mpunga, migomba na mihogo ilikuwa ni pamoja na shughuli zake nyingine, akisema kuwa anaamini kilimo ndio kila kitu.
Kwa wakati huo mama huyo, aliendeleza dini yake ya kiislamu, baada ya kuanzisha madrssa iliyosheheni wanafunzi mchanganyiko zaidi ya 100.
Huku akiendeleza shughuli za biashara, kilimo, ususi wa mikoba na makawa, sambamba na kuwa ni mwalimu mkuu wa madrssa yake, hadi mwishoni mwa mwaka 2004.
RAYA KWENYE SIASA NA UONGOZI
Kabla ya kuingia ndani ya siasa na Chama chake cha Mapinduzi CCM, kwanza alishawahi kupewa mafunzo kadhaa, kutoka kwa Jumuiya watu wenye Ulemavu Zanzibar ‘UWZ’.
Mafunzo hayo pamoja na mambo mengine, yalihusisha kuwajengea uthubu wao wenye ulemavu, namna ya kushirikia kwenye siasa na uongozi.
Baada ya kukolea vyema mafunzo hayo, alijimwaga uwanjani kwa kuanza kuchukua fomu za kuwania uwakilishi wa viti maalum ndani ya CCM, na hasa nafasi za watu wenye ulemavu.
“Hongera chama changu cha CCM, kwa hivi viti maalum kuvigawa baina ya sisi wenye ulemavu, vijana na sasa naskia kuna na viti vya wasomi,’’anasema.
Aliachukua fomu na kuirejesha wilaya ya Wete, na hapo sasa ngarambe ya kampeni kwa wajumbe husika ilianza, kwa kishindo.
“Mimi sikujali ulemavu wangu, na wala haukuwa shida kwamba eti niujutie, nilipita kila kichochoro na ulemavu niliuwacha nyumbani, nikapiga kampeni,’’anasimulia.
Hatowasahau akina bi Mwandawa na Salma Saadat kwa mafunzo mbali mbali ya kuwajengea uwezo, ambayo ndio yaliyompa uthubutu, hadi kuingia baraza la Wawakilishi.
Mwaka 2005, baada ya kuchukua fomu ndani ya chama chake cha CCM, ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni siasa za ushindani na zenye joto la aina yake.
“Siasa ya mwaka 2005, ilikuwa ngumu, maana ukionekana unashangilia chama tawala, ujitayarishe na kuzomewa, kugomewa au kuonekana wewe sio wa maana, hivyo wengi walikuwa woga,’’anasema.
“Nilikuchukua fomu chamani kwangu siku hiyo na kuijaza na kuirejesha siku hiyo, na kisha fomu zetu sisi wenye ulemavu huwa zinapitishwa CCM makao makuu Tanzania bara,’’anaeleza.
Pamoja na hilo, Raya alikwenda kwa wanaccm wenzake wa wilaya ya Wete, kwa ajili ya kupigiwa kura na kuibuka na kura za ushindi 34 kati ya wajumbe wote 37.
Safari ya kuingia baraza la Wawakilishi kwa viti maalum hasa wenye ulemavu kwa bi Raya ikawa haijamaliza, kwani safari sasa ikawa ni ya kwenda Dodoma makao makuu.
Anasema hata pale Dodoma, shughuli ya kuomba kura na kupiga kampeni ili wajumbe wampe ridhaa, iliendelea kwa muda wa siku tatu na haikuwa rahisi.



Ulemavu wake haukuwa tatizo, na alikuwa akimfika kila mmoja kumuomba kura, ili amshinde mpinzani mwenzake kutoka kisiwani Unguja.
Kumbe hapa, inafahamika kuwa, kati ya wajumbe hao wawili, anatakiwa mmoja tu kuingia baraza la Wawakilishi, ili akawawakilishwe kundi la watu wenye ulemavu.
“Mimi nilikuwa na Katibu wangu mkuu wa UWZ bi Mwandawa, ndie ambae aliyekuwa mshindani wangu, na mwisho wa siku kati ya kura 120 nilipata kura 100,’’anasilimulia.
Hapo Bi Raya akaibuka kidedea na dua zake baada ya kurudi Pemba, ni kukiombea dua chama chake cha CCM, kishinde uchaguzi mkuu, ili naye aingie barazani kwa mgongo wa viti maalum.
BAADA YA KUINGIA BARAZANI
Bi Raya alianza kulikanyaga zulia jekundu la Baraza la Wawakilishi, Nomvemba mwaka 2005, na hapo alikuwa mgeni mno kwa wiki tatu za mwanzo.
“Kwa hakika wiki tatu za mwanzo zilikuwa ngumu kwangu, maana ule mfumo wa kutembelea kitimwendo, na wenzangu wote wako sawa, nilijihisi vibaya kidogo,’’anasema.
Lakini hatomsahau spika wa wakati huo Pandu Ameir Kificho, ambae alimpa nguvu, ari na hasa kumtangaaza mara kwa mara, akitaka haki na fursa zake ziheshimiwe.
Alifanyakazi vyema ndani ya miaka 10 ya nafasi hiyo, na alipata ushirikiano wa hali ya juu, kuanzia walinzi wa baraza la Wawakilishi, wawakilishi wenzake na hata alipochaguliwa kwenye kamati mbali mbali.
Uwezo wake wa kuhoji fedha, masuli ya msingi na nyongeza yalimfanya alitawale vyema baraza hilo, sambamba na kutetea watu wenye ulemavu.
Nilishiriki vyema kuuchangia na kuukosa msaada wa sheria ya nambari 9 ya mwaka 2006, hadi pale rais wa Zanzibar kwa wakati huo Amani Abeid Karume alipoisaini.
“Niliingia barazani wakati mwafaka, maana ndio mwaka ambao nilishiriki kwa vitendo kuichangia sheria yetu, na ile sheria naikumbuka moja ya vifungu nilivyochangia, na kupita ni kile cha 43,’’anasema.
“Nilipendekeza kuwa, iwe ni kosa kumfanyia dhihaki, kejeli ya sauti, mwendo, ishara mtu mwenye ulemavu jambo lolote la dharau, na kilipita leo najivunia,’’anakumbuka.
Sheria hiyo pia uzuri wake walipitisha uwepo wa Mfuko wa Maendeleo wa watu wenye ulemavu, kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 38, ambapo ulitaja kuwa utaongozwa na Mkurugenzi chini ya usimamizi wa Baraza.
Anasikitishwa na kifungu cha 6 cha sheria hiyo, kwamba hakijatekelezwa ipasavyo, juu ya suala la kuondoa ubaguzi wa ajira kwa wenye ulemavu.
Akisema kuwa, kifungu hicho kimeshafafanua kuwa, kusiwe na muajiri atakayewabagua moja kwa moja au vyenginevyo mtu mwenye ulemavu, katika ajira.
“Jambo ambalo mimi naliona bado, kwenye nafasi za ajira kundi la wenzetu mwenye ulemavu halijapewa kipaumbele, na sheria hiyo kutotekelezwa ipasavyo,’’anafafanua.
Jengine analolikumbuka kulisemea ndani ya baraza la Wawakilishi, ni kero la kurejeshwa nyumbani watoto waliokosa sare, jambo ambalo kisha lilitolewa tamko.
“Wakati huo waziri wa Elimu alikuwa Haroun Ali Suleiman, aliniskiliza na kutoa uamuzi kuwa, waalimu wasiwarejeshe nyumbani watoto kwa kukosa sare,’’anasema.

ALIYOFANYA NJE YA BARAZA AKIWA MWAKILISHI
Aliyafanya mengine ndani ya kipindi chake cha miaka 10, akiliwakilishi kundi la watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuviwezesha kifedha vikundi vya watu wenye ulemavu vya Unguja na Pemba.
“Watu wenye Ulemavu kijiji cha Bungi Unguja, niliwanunulia vyerehani maalum na kuwafungulia sakosi ya kuweka na kukopa, ili wajiendeleze,’’anasema.
Lakini hata kwa upande wa Pemba, baada ya kuunganisha nguvu na TASAF, walinunua vyerehani 10, na kufungua kiwanda cha ushoni pamoja na gharama za vitambaa na mikasi.
Hata watoto wenye ulemavu na wengine wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa mwaka huo wa 2008 aliwagharamikia ada ya kuingia skuli.


“Watoto zaidi ya 200 wanaoanza darasa la kwanza na wale waliokuwa wakirejeshwa skuli kwa ukosefu wa sare, niliwahudumia, ili waendelee na masomo,’’anakumbuka.
Katika eneo jengine anasema, suala la mtu kuwa mlemavu na hasa mwanamke, hakuna uhusiano wa kukoseshwa haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa.
Anasema kundi la watu wenye ulemavu, bado halijapewa kipuambele katika masuala ya siasa na uongozi, kwa kuonekana hawawezi jambo ambalo, sio sahihi.
“Kama kura za watu wenye ulemavu wasiokuwa na ulemavu wanazitaka, basi wakumbuke kuwa, hata mwenye ulemavu nae anahitaji siku moja apigiwe kura,’’anasema.
CHANGAMOTO ZAKE KWA UJUMLA
Kwanza baraza la Wawakilishi la sasa anasema haliko rafiki kwa watu wenye ulemavu, kutokana na eneo la ukumbi wake kuweko juu.
Hili linaweza kumpa wakati mgumu mtu mwenye ulemavu, jambo ambalo anasema, alilikemea bila ya mafanikio katika kipindi cha miaka yake mitano ya mwisho.
Jengine ni kutopewa kipuambele watu wenye ulemavu, hasa katika sekta ya ajira, jambo linalowazidisha unyonge na kujiona ni wenye kutengwa.
WANAOMFAHAMU RAYA
Hidaya Mjaka Ali anasema, enzi za uongozi wake, aliwafanyia mengi, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha miongoni mwa makundi ya watu wenye ulemavu.
Salum Abdalla Salum, anasema bi Raya alikuwa na kasi na hamu ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanafikia ndoto zao na kuondokana na utegemezi.
“Alianzisha kituo kikubwa cha ushoni Ole, ambapo wapo wengine kuanzia mwaka huo wa 2010 hadi leo wanajiendeleza na wamejiajiri wenyewe, hili sio jambo dogo,’’anafafanua.
Akizungumza hivi karibuni kwenye uzinduzi wa muongozo kwa kuelekea uchaguzi mkuu kwa ajili ya wanawake na wanawake wenye ulemavu, Afisa Mdhamini Afisi ya Makamu wa Kwanza wa rais Pemba, Ahmed Abubakar Mohamed, ameipongeza Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), kwa kuandaa muongozo huo.
Akiwasilisha muongozo huo, mshauri elekezi Salim Othma Hamad, alisema bado vyama vya siasa, havijazingatia ipasavyo kundi la wanawake na wtu wenye ulemavu.
Safia Saleh Sultan na Sabah Mussa Said, walisema bado elimu inahitajika ili kulithamini kundi la wanawake na watu wenye ulemavu.
Ikumbukwe kuwa, kati ya majimbo 18 ya uchaguzi kisiwani Pemba, ni Jimbo la Pandani pekee, ambalo linaongozwa na mwanamke kwa nafasi ya ubunge, ambapo kwa uwakilishi ni majimbo ya Chambani, Konde, Wete na Gando.
Kwa upande wa kisiwa cha Unguja, wanawake wameibuka na ushindi kwenye majimbo manne ‘4’ ya uwakilishi, wakati kwa nafasi ya ubunge kati ya maijimbo 32, wanawake ni watatu ‘3’, na hakuna mwakilishi wala mbunge wa Jimbo mwenye ulemavu.
TAMWA
Moja ya tasisi ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha, wanawake wanakuwa na uwezo wa kudai haki zao katika uongozi, siasa na demkorasia ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar.
Na ndio maana sasa inaendesha mradi wa miaka wa miaka minne, ambao pamoja na shughuli zake, lakini unataka kuona baada ya mradi kutia nanga, sasa wanawake wanaweza kudai haki zao.
Kwa mfano Mratibu wa Mradi huo wa ‘SWIL’ kutoka TAMWA Salma Amir Lusangi, anasema wanawake wanayo haki ya kuingia kwenye kamati kuanzia ya shehia.


Akaongeza hata kamati za skuli, kamati za maendeleo za majimbo, wilaya, mkoa hadi taifa ambapo bado katika maeneo hayo mfumo dume unanguruma.
“Mradi huu unataka kuona wanawake wanaingia kila eneo, maana hakuna katiba, sheria, maadhimio wala matamko ya kimataifa ambayo yamemzuia mwanamke kuwa kiongozi,’’anasema. Tamwa Zanzibar
Ndio maana Mratibu wa TAMWA-Pemba Fat-hya Mussa Said anasema ili kufikia malengo hayo, waliamua kuwashirikisha wandishi wa habari ili kuona, wanaamasha wanawake kudai haki zao.
Akizungumza kwenye mafunzo ya siku mbili yaliofanyika ofisi ya TAMWA-Pemba, anasema zipo mamlala hazijawajibika vyema, na ndio maana wanawake wamekuwa wakikoseshwa haki zao.
“Kwenye siasa wanaume wameshika ngazi za juu, kwenye jumuiya pia na hata kamati za sheha, skuli, usheha, ukatibu mkuu na mengine, kama vile wanawake hawapo,’’analalamika.
Mwandishi Mchanga Haroub Shehe, anasema bado mamlaka hazijawajibika ipasavyo na ndio maana wanawake hawaonekani kwenye nafasi kadhaa.
MWISHO

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da...

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 m...

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’...

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa uf...

…….SUZA WATOA USHAURI WA ADHABU YA KUNYONGWA

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ WANAFUNZI wanaosomea uwalimu Chuo cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ kampasi ya Benjamin Wiliam Mkapa Wete Pemba, wamependekeza adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mtu atakaetiwa hatiani, kwa kosa la dawa za kulevya. Walisema, haiingii akili kuona, mahkama imeshamtia hatiani mtu kwa kukutwa na dawa za kulevya, ambazo huathiri nguvu kazi ya taifa na kisha, kupewa hukumu ya kifungo pekee. Wakizungumza leo Juni 26, 2024 kwenye kongamano la vyuo vikuu, juu ya masuala ya msaada wa kisheria, kuelekea wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar, lililofanyika Chuoni hapo, walisema wakati umefika sasa kutolewa kwa hukumu hiyo. Walipendekeza kuwa, ni vyema kwa mtu anayetiwa hatiani asibakie chuo cha Mafunzo pekee kuitia tena hasara serikali kwa chakula na wakati mwingine matibabu, wakati tayari ameshasababisha madhara, kwa vijana. Mshiriki Juma Nafasi Juma, alifafanua kuwa kama mtu ameamua kuliumiza taifa kwa kuingiza, kusafirisha, kusambaaza dawa za kulevya, hivyo n...