IMEANDIKWA NA TATU MAKAME
MAHUJAJI watarajiwa wameaswa kuacha kushughulikia simu wanapokuwa katika ibada ya Hijja, ili waweze kuitekeleza kwa utulivu, unyenyekevu na kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ali Abdulghulam Hussein, wakati akifunga mafunzo kwa Mahujaji watarajiwa iliyofanyika katika Ukumbi wa Shantimba, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja yaliandaliwa na Taasisi ya Khairat Hajj and Umra Travel.
Alisema, ni muhimu kwa mahujaji kufuata miongozo wanayopewa na viongozi wa Hijja na kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu ibada hiyo, ikiwemo kutumia simu bila ulazima au kujihusisha na mambo yasiyo na tija.
“Niwaase mahujaji watarajiwa msijishughulishe na mambo yasiyo na faida kama kuangalia michezo wakati wa ibada, hilo linaweza kuharibu utekelezaji wa nguzo ya tano ya Uislamu,” alisema Abdulghulam.
Aidha, aliwataka kuwa wavumilivu katika kipindi chote cha ibada hiyo ili waweze kuitekeleza kikamilifu na kufikia malengo ya safari yao ya kwenda Makka, nchini Saudi Arabia.
Alisisitiza kuwa, Hijja ni fursa adhimu ya kumkaribia Mwenyezi Mungu na kupata nafasi ya kuwaombea dua viongozi wa nchi, familia na jamii kwa ujumla.
“Hakuna sehemu ambayo mtu anakuwa karibu zaidi na Mola wake kama katika nyumba tukufu ya Makka, tumia fursa hiyo kuomba dua kwa ajili ya nchi na familia zenu,” aliongeza.
Pia aliwataka waandaaji wa safari za Hijja kuweka mipango madhubuti ya usafiri ili kupunguza usumbufu kwa mahujaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Khairat Hajj and Umra Travel, Alhajj Suleiman Mohamed Rashid alisema, mahujaji 50 wanatarajiwa kusafiri Mei 12 mwaka huu kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar.
Alisema mwitikio wa wananchi umeongezeka kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa Mahujaji, hususan watumishi wa umma wanaokaribia kustaafu.
Alisisitiza umuhimu wa Mahujaji kusafiri na kutembea kwa vikundi wanapokuwa katika mji mtukufu wa Makka ili kuepuka changamoto kama kupoteana.
Akitoa mafunzo ya mwongozo wa Hijja, Sheikh Khamis Salim Ali aliwataka Mahujaji kuzingatia taratibu zote za kidini na kisheria, ili kuhakikisha wanapata radhi za Mwenyezi Mungu.
“Niwakumbushe kufuata maelekezo yote mliyopatiwa na kuepuka yaliyokatazwa ili kulinda ubora wa ibada yenu ya Hijja,” alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya Mahujaji watarajiwa waliwahimiza Waislamu wengine kujiandaa mapema kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo wakiwa na afya njema na maandalizi ya kutosha.
MWISHO.

Comments
Post a Comment