Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA ZNZ) Dkt. Mzuri Issa amesema ni muhimu kuwa na sheria bora za habari ambazo zinapelekea kuwepo kwa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza kwa jamii.
Amesema hayo wakati wa mkutano
wa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya tume ya utangazaji ya Zanzibar
(No. 7, 1997), ambao uliwashirikisha kamati ya masuala ya habari (ZAMECO), Asasi
za kiraia na Tume ya kurekebisha ya Sheria uliofanyika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini.
Dkt. Mzuri
aliongeza kuwa ipo haja ya kufanyiwa marekesbiso sheria hiyo ili kutoa
fursa ya uhuru wa kujieleza ambao ndio chanzo kikuu cha maendeleo ya nchi.
“ Uhuru wa habari na haki ya
kupata habari pamoja na uhuru wa kujieleza ni mambo ya msingi katika maendeleo
ya nchi na inaleta furaha ya mtu binafsi”,
amesisitiza Dkt. Mzuri Issa.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa tume ya kurekebisha sheria Zanzibar, Ndugu Khadija Shamte
amesema kuwa muda umefika sasa kuwa na sheria zinazokwenda na wakati na tume
iko tayari kushirikiana na wadau kwenye kupokea maoni ya kurekebisha sheria ili
kutoa fursa kwa vyombo vya habari kukua na kuwa na ushindani katika kusambaza
taarifa.
“Tunahitaji kushirikiana kwa
pamoja na mwisho kupata sheria bora na nzuri ambayo italeta mabadiliko katika
tasnia ya habari Zanzibar”, Khadija Shamte, Mwenyekiti Tume ya Kurekebisha
Sheria.
Wakizungumza katika mkutano huo
wadau wa habari Zanzibar wamesisitiza tume kuifanyia kazi mapendekezo
yote yaliyotolewa na hatimaye kupatikana kwa sheria yenye kukidhi vigezo na
inayoikwenda na wakati.
Mwenyekiti wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Zanzibar, Zanzibar Press Club (ZPC), Abdullah Mfaume
amesema mapendekezo ya sheria ya habari inarahisisha upatikanaji wa habari
katika ukusanyaji, usambazaji wa taarifa kwa waandishi wa habari na itakuwa
tija na maslahi kwa jamii.
Ameiomba Tume ya kurekebisha
Sheria pamoja na watendaji wengine kuitumia ZAMECO katika kujadili sheria zozote
zinazohusiana na masuala ya Uandishi wa habari ili kupata taarifa zaidi
kuhusiana na hali halisi na masuala mbali mbali yanayoathiri sekta hiyo.
Mkutano huo wa siku moja unaojadili Sheria zinazohusu
habari umeandaliwa na Chama cha Waandishi wahabari Wanawake Tanzania Zanzibar,
TAMWA ZNZ chini ya Ufadhili wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth.
Comments
Post a Comment