NA NAFDA HINDI, ZANZIBAR
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali ameishauri Serikali pamoja na Taasisi binafsi kuandaa Sera na Sheria za nchi kwa kuzingatia usawa na jinsia zote ili kuwepo usawa wakati wa teuzi mbali mbali zinazofanywa.
Akizinduwa waraka maalumu naoainisha changamoto zinazowakumba wanawake na watu wenye ulemavu katika kugombea nafasi za Uongozi hafla iliyofanyika Ofisi za ukumbi wa bima Mperani mjini Unguja.
Dk.Mzuri amesema kwa miaka mingi wanawake na watu wenye ulemavu wamekosa nafasi muhimu katika ngazi za maamuzi jambo ambalo linawanyima haki yao ya msingi ya kidemokrasia ya kutoa mawazo yao na uhuru wa kujieleza.
“Elimu ndio ngazi kubwa ya kuwapeleka wanawake katika Uongozi kwa miaka mingi iliyopita walinyimwa fursa ya elimu na baadhi ya wazee ama walezi kutishwa na kuwa na dhana potofu ya kuharibiwa watoto wao katika masuala ya udhalilishaji na kwa bahati mbaya fursa hizo kupata wanaume pekee,” alisemai.
Aidha Dk. Mzuri ameiomba Serikali pamoja na Mrajisi wa vyama vya siasa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na vitimaalum licha ya kwamba nafasi hizo zimesaidia wanawake kujifunza masuala ya siasa kivitendo na kujenga weledi katika Uongozi.
“Viti maalum vimesaidia kuwainuwa wanawake wengi kujiamini na kujifunza katika Bunge na Baraza la Wawakilishi ila muda mwengine vinafaidisha wachache mpaka wengine wanaitwa malkia wa viti maalum (Qeens of special Seat), hivyo miaka mitano inatosha kujifunza,” alieleza DkMzuri.
Mapema akiwasilisha waraka huo maalum Mkurugenzi kutoka Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud amesema katika warakahuo wamewasilisha baadhi ya Sheria zinazowakwaza wanawake na watu wenye ulemavu zinazoonekana kupitwa na wakati kwa mazingira ya sasa.
“Tunatakauwepo sheria zinazozungumza wazi na kumlazimisha mtu yeyote kuhakikisha katika kila nafasi ya Uongozi, mwanamke anapewa nafasi sawa na mwanamme,” alifafanua Mkurugenzi huyo wa ZAFELA.
Amesema baadhi ya Sera na Sheria zilizopo kwa sasa zinamapungufu hivyo endapo zitafanyiwa marekebisho zitaleta mabadiliko katika makundi maalum pamoja na wanawake katika kufikia usawa wa hamsini kwa hamsini katika ngazi za maamuzi.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) Salma Saadat amesema ipo haja ya kufanya utetezi wa pamoja ili kutoa nafasi ya ujumuishaji wa watu wa makundi maalum kushiriki katika nafasi za Uongozi.
“Mpaka sasa kwenye Baraza la Wawakilishi tuna wajumbe watatu tuwe wenye ulemavu jambo ambalo linaonesha kuwa bado ushiriki wao ni mdogo hivyo kukosa ujumuishi na ushiriki wao kikamilifu katika upatikanaji wa haki zao,”alisema Salma Saadat Haji.
Aidha Mkurugezi wa Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira Pemba (PEGAO) Hafidh Abdi Said amesema jamii inahitaji Amani na Utulivu pamoja na mshikamano kwa watu wote hivyo muda umefika kwa wanawake kupewa nafasi za Uongozi kwa sababu historia inaonyesha wanawake hufanya vizuri katika eneo hilo.
Nao wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za Uongozi wamesema wamefarajika kupewa mafunzo yanayohusu Uongozi na Kuiomba Serikali kuzichukuwa changamoto zilizowasilishwa katika waraka huo na kuzifanyia kazi kwa vitendo ili kuleta mabadiliko nchini.
Baadhi ya Sheria zilizotajwa zinazoweka vikwazo ni pamoja na Sheria ya Ushirikishwaji katika Siasa (Perticipation of Political Party), Sheria ya Uchaguzi (Election Act) No 4,2018, Sheria ya Utumishi wa Umma ( Public Service),No 2,2011, Zanzibar Civil Status Regulation Agency Act No 3,2018.
Waraka huo maalum umetayarishwa kwa pamoja na Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA,ZNZ), JumuiyayaWanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya utetezi wa Mazingira Pemba (PEGAO) na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) wanaotekeleza kwa pamoja mradi wa kuwajengea uwezo wanawake kugombea nafasi za Uongozi (SWIL) unaofadhiliwa na Ubaloziwa NORWAY.
Comments
Post a Comment