NA HAJI NASSOR, PEMBA
NAIBU Balozi wa Ireland nchini
Tanzania Mags Gaynor, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa umiliki wa
rasilimali ardhi kwa wanawake, uliokuwa ukitekelezwa na Mwemvuli wa asasi za
kirais Pemba ‘PACSO’ na kumalizika hivi karibuni.
Naibu Balozi
huyo alisema, kutokana na majibu ya wanufaika wa mradi huo alivyozungumza nao,
ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, na hasa kwa kuwafikia walengwa.
Alisema
mradi huo ulilenga kuwafikia wanawake ili kuwajengea uwelewa, juu ya umilikiwa
wa rasilimali ikiwemo ardhi, jambo ambalo sasa, limewanufaisha hasa kwa kuwepo
wanufaika waliopata haki zao.
Naibu Balozi
huyo aliyasema hayo ofisi za PACSO Chake chake Pemba, kwenye kikao cha tathimi
kilichojumuisha wanufaika wa mradi wa uongozi wa PACSO.
Alieleza
kuwa, kwa vile wapo wanawake kisiwani Pemba walionufaika moja kwa moja, ikiwa
ni pamoja na kurithi, kununua ardhi na kulalamikia ucheleweshaji urithi ni
hatua kubwa.
“Serikali ya
Ireland, imeridhishwa mno na mradi huu uliokuwa ukiendeshwa na ‘PACSO’ na
tutangalia uwezekano wa kuendeleza kuhusiasna na elimu kwa jamii,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Naibu huyo Balozi wa Ireland Mags Gaynor, alisisitiza haja kwa
wanufaika hao kuwafikishia wenzao elimu ya umuhimu wa umiliki rasilimali.
Alisema
kuwapa mradi huo PACSO rasilimali fedha hazikupotea, kutokana na kuwanufaisha
walengwa, waliokuwasudiwa ndani ya jamii husika.
Mmoja wa
wanufaika hao Fatma Khamis Juma wa Wawi, alisema awali hakuwa akiona umuhimu wa
umiliki wa rasilimali, ingawa baada ya mafunzo, sasa ameamka.
“Hata urithi
sasa tumesharithi, maana niliwaambia kaka zangu kuwa sasa turithi, na
tumesharithi baada ya kuwaelimisha ingawa walikuwa wazito,’’alieleza.
Mratibu wa
miradi kutoka PACSO, Mohamed Najim Omar, alisema licha ya mradi huo kuwa wa
miezi miwili, lakini umefikia lengo lao.
“Pamoja na
kwamba mradi ulikuwa wa miezi mwili, lakini wanawake kwa asilimia 60 na wanaume
asilimia 40, walifikiwa na kunufaika kwa kupata elimu,’’alieleza.
Nae Salama
Mtondoo kutoka Wete, alisema licha ya kuwa na kesi yake mahakamani ya
kutapeliwa na kiongozi wa serikali ardhi yake, lakini mafunzo hayo yamempa
hamasa zaidi.
“Mafunzo ya
umiliki wa ardhi, na hasa siku ile ya kuzitambua sheria za ardhi, kwangu
yamenipa uwelewa zaidi, wa kuendelea na kesi yangu,’’alieleza.
Sheha wa
shehia Vitongoji wilaya ya Chake chake, Ayoub Suleiman, alisema katika kipindi
cha mwezi Januari hadi Febuari alipokea malalamiko 40 ya wanawake juu ya ardhi.
“Baada ya
kupata mafunzo ya umiliki wa rasilimali hasa ardhi, sasa hata malalamiko katika
shehia yangu yameongezeka kutoka 25 ya mwaka 2021, hadi kufikia 40 kwa kipindi
cha miezi mwili kwa mwaka huu,”alisema.
Afisa
Mipango wilaya ya Chake chake Kassim Ali Omar, alisema wamepokea maombi 20 kwa
mwaka huu, ya wanawake wakiomba kununua na kuuza ardhi zao.
Katibu mkuu
wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, alisema mradi huo wanatarajia unawezaa mwengine
kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata.
Katika
utekelezaji wa mradi huo, awali kulifanyika uzinduzi wa mradi, kongamano,
mafunzo ya siku nne ya umiliki ardhi pamoja na kuzifahamu sheria za usimamizi
ardhi.
Mwisho
Comments
Post a Comment