NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
WAKAAZI
wa nyumba za Serikali zinazosimamiwa na Wakala wa Majengo Pemba, ambazo zipo
Uzunguni Wete wametakiwa kuhama, ili kupisha matengenezo ya nyumba hizo.
Akizungumza na baadhi ya wakaazi wa nyumba hizo, Afisa
Mdhamini Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Pemba, Bakar Ali Bakar
alisema, ni vyema wananchi wakahama katika nyumba hizo, kwani zinahatarisha
usalama wa maisha yao.
Alisema kuwa, kutokana na ubovu wa nyumba hizo haistaki tena
kuishi wananchi, hivyo ni vyema wakasikiliza maagizo ya Wizara kuhusu kuhama
eneo hilo, ili ziweze kufanyiwa matengenezo.
“Tuliwahi kuwapelekea barua ili wahame kwenye nyumba hizi
kwa sababu ni mbovu na tayari zimeshafanya mipasuko, hivyo ni hatari kwa maisha
yao, lakini baadhi yao bado hawajakubali kuhama”, alisema Mdhamini huyo.
Aliwaomba wakaazi hao kuridhia maagizo ya kuhama kwenye
nyumba hizo, huku Wizara ikiandaa utaratibu wa kuzijenga, ili kuepuka maafa
yanayoweza kutokea.
“Serikali ina azma nzuri kwenu, haina lengo la kuwafukuza
katika nyumba hizi lakini kutokana na majengo yalivyo sasa hakuna haja ya
kuishi hapa ni lazima kuhama”, alisema.
Mdhamini huyo alieleza kuwa, ubovu wa nyumba hizo kunaweza
kuwaletea athari kubwa wao na Serikali na kusababusha kugharimu maisha ya watu
pamoja kukosekana kwa rasilimali watu.
Kwa upande wao wakaazi ambao hawajahama katika nyumba hizo
walieleza kuwa, walikuwa wameshaanza kuhama ingawa kuna baadhi ya vitu
hawajamaliza na ndio maana muda mkubwa wanakuwepo eneo hilo.
“Hatuishi tena hapa na tumeshahamisha baadhi ya vitu vyetu ingawa
kwa vile tumezoea huwa tunakuja na kukaa mara moja tu, lakini sasa tutahamisha
kila kitu chetu na kuondoka”, walisema baadhi ya wakaazi hao.
Nae Injinia Said Malik Said kutoka Wakala wa Majengo Pemba
alisema kuwa, ni muda wametoa barua ya kuhama kwa wakaazi hao ingawa baadhi yao
wamekaidi agizo hilo.
“Tulifikiri tayari wameshahama, lakini nimeshangaa leo
kuwaona hapa, nyumba ni mbovu na tunawahamisha kwa usalama wao, ingawa bado
baadhi yao hawajalipa umuhimu suala hili”, alisema.
Alisema tangu watoe barua hizo, hawajawahi kudai kodi kwani
hawatakiwi tena kuishi hapo mpaka pale nyumba hizo zitakapomalizika kujengwa.
Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kupitia Wakala wa
Majengo Pemba inatayarijia kuzijenga nyumba zilizopo Uzunguni Wete ili ziwe na
hadhi ya kisasa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment