Skip to main content

WADAU WA ELIMU PEMBA: WATAKA SERA IJAYO YA ELIMU IKIREJESHEE HADHI CHUO CHA UALIMU NKURUMAH

 




NA HAJI NASSOR, PEMBA

WADAU wa elimu kisiwani Pemba, wamependekeza kua sera mpya ijayo ya elimu, ilazimishe kukirejeshea hadhi na uasili wake Chuo cha uwalimu Nkurumah, ili kupata waalimu wenye sifa na uwezo zaidi wa kufundisha.

Walisema kwa sasa kuna waalimu waliosoma sana na na sio waliosomea, jambo linalochangia kushuka kwa hadhi ya elimu Zanzibar, ikilinganishwa na muongo mmoja uliopita.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika miji ya Chake chake, Wete na Micheweni wadau hao walisema, ni vyema sera ikatambua na kukirejeshea hadhi hicho hicho cha waalimu.

Walisema, chuo hicho kilitoa mafunzo ya kina kwa waalimu na kuwajenga kiuwezo hata kama hawakua na elimu ya juu mfano wa shahada na uzamilivu.

Mmoja kati ya wadau hao mwalimu mstaafu skuli ya Uweleni, Mohamed Ussi Shaame, alisema chuo hichoo kilikuwa mwarubaini wa kuipandisha hadhi elimu ya Zanzibar.

“Kwenye sere mpya ya elimu ijayo ni vyema ikatamka wazi wazi, suala la kukifufua kimafunzo na kimasomo chuo cha ualimu cha Nkurumah, ili tuzalishe wanmafunzi bora,’’alipendekeza.

Mkuu wa shirika la Maktba kisiwani Pemba, Mwache Mohamed Bakar, alisema moja ya eneo muhimu la kulirekebisha ni uwepo wa mafunzo bora ya waalimu.




Aidha alisema jengine linalofaa kuingizwa kwenye sera mpya ijayo ni kulazimisha kwa kila skuli iwe na maktaba yake na yenye vitabu vyote husika.

“Lakini hata sera itamke na ilazimishe kusijengwe wala kufunguliwa skuli yoyote pasi na kuwepo kwa matundu ya vyoo yanayokwenda samba mba uwiyano wa wanafunzi,’’alipendekeza.

Nae Mzazi Bimkubwa Juma Abass wa Chumbageni Mkoani, alipendekeza suala la ujenzi wa skuli lazima uzingatie mahitaji na matakwa ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Nae Siti Makame Ali ambae ni mjumbe wa PACSO alipendekeza kuwa, vyumba vya madarasa yawe na vifaa kamili ikiwa ni pamoja na meza na viti.

Kuhusu urejeshaji wa viboko (bakora), alipendekeza viwepo lakini kama adabu mbadala kwa wanafunzi, na iwe baada ya kupewa maonyo na maelekezo na waalimu.

Akizungumza kwenye mkutano wa siku mbili kwa wadau wa elimu wa Mkoa wa kusini Pemba, Mwenyekiti wa PACSO Mohamed Ali Khamis, alisema wameamua kufanya uchechemuzi wa sera ya elimu, ili wananchi watoe maoni yao.




Alieleza kuwa, PACSO imekuwa na utamaduni ya kuisadia serikali katika kuifikia jamii iliyokubwa zaidi, ili kuona maona yao wanayatoa kuelekea kupata sera mpya.

Mratibu wa miradi kutoka PACSO Mohamed Najim Omar, alisema mara watakapokamilisha ukusanyaji maoni, watayafikisha wizara ya elimu, kama sehemu ya maoni yao.

“Moja ya jukumu kubwa la asasi za kiraia, ni kuisaidia kazi serikali kuu, kwani nasisi tunakundi kubwa la jamii, na ndio maana tumeshafanya mikutano kadhaa ya kupokea maoni,’’alieleza.

Kaimu Mratibu wa Idara ya Mpingo, sera na utafiti wa wizara ya elimu Pemba Adam Kombo Nassor, alisema wanachokifanya PACSO kwao ni msaada mkubwa, katika uandaaji wa sera mpya ya elimu.

“Ni kweli sera inayotumika sasa ya mwaka 2006, imeshajaa changamoto, sasa wizara iko mbioni kukusanya maoni ili kisha baadae  kuwa na sera ambayo ndio muongozo wa elimu,’’alieleza.

Utafiti mdogo uliofanywa hivi karibuni na PACSO juu ya sera ya elimu inayotumika sasa ya mwaka 2006, ambapo waliwahoji watu 50 kwa kila wilaya kisiwani Pemba, ilibaina watu 162 kati ya 200  waliotakiwa kueleza nini maana ya sera hawakuwa na uwelewa.

Aidha utafiti huo ukabaini kuwa, watu 183 kati ya 200 waliohojiwa hawajui taratib za kuanzia mwanzo hadi mwisho za upatikanaji sera.

Watu wengine 138 walisema ushirikishwaji wao katika sera ya mwaka 2006 ni katika mikutano na ujenzi wa vyumba vya madarasa pekee.

                          Mwisho        

 

Comments