Skip to main content

FATMA SULEIMAN, MWENYE ULEMAVU ALIYEFANYA MAAMUZI YA KIMAENDELEO

 

NA ZUHURA JABIR

 

Katika jamii, mara nyingi mafanikio hupimwa kwa kiwango cha elimu, mali au nafasi aliyonayo mtu. Hata hivyo, kuna watu ambao maisha yao yanatufundisha kwamba mafanikio makubwa huanza pale mtu anapoamua kujiamini, kupambana na changamoto na kutokubali mazingira yamzuie kufikia ndoto zake.

 

Hii ni simulizi ya Fatma Suleiman Mussa, mwanamke mwenye ulemavu anayeishi Jumbi, Zanzibar, ambaye licha ya changamoto alizokutana nazo tangu akiwa mtoto, ameamua kutumia uwezo alionao kujiajiri, kusaidia familia yake na kuwa mfano kwa wanawake wengine wenye ulemavu. Safari yake imejaa changamoto, lakini pia ni ushahidi kwamba ulemavu si mwisho wa ndoto.

 

SAFARI YA ELIMU NA MAISHA

Fatma ni mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne, wote wakiwa wa kike. Alianza elimu ya msingi katika Skuli ya Tunguu na baadaye aliendelea hadi kidato cha pili mwaka 2015. Alipata nafasi ya kuendelea na kidato cha tatu katika Skuli ya Kibele, lakini changamoto mbalimbali zilimfanya ashindwe kuendelea na masomo.

 

Hata hivyo, mama yake hakukubali kuona ndoto ya mwanawe ya kupata elimu ikizimika. Alimtafutia fursa nyingine ya masomo Mazizini, ambako Fatma aliendelea na masomo katika Kiembe Samaki na hatimaye akafanikiwa kuhitimu kidato cha nne.

 

Baada ya kumaliza masomo, Fatma alianza kujifunza ujasiriamali, ikiwemo utengenezaji wa sabuni, dawa za chooni na Jiki. Hakusimama hapo. Alijikita pia katika uwakala na baadaye akaanzisha duka pamoja na mume wake.  Kwa Fatma, mafanikio hayakuwa jambo la kusubiri, bali safari ya kuendelea kujifunza na kujaribu fursa mbalimbali.

 

Ulemavu wa Fatma ulitokea akiwa na umri wa miezi sita, wakati bado akiwa kitandani. Hali hiyo ilimfanya kwa nyakati fulani ajione hawezi kufikia baadhi ya malengo yake.  Lakini alipofikisha miaka 20, alianza kujitambua zaidi na kuelewa kwamba ulemavu haupaswi kuwa sababu ya kukataa tamaa.

 

Katika safari hiyo, mama yake alikuwa nguzo muhimu. Fatma anakumbuka maneno ya mama yake yaliyompa nguvu ya kuendelea kupambana:

 


Hakuna kukataa tamaa. Leo nipo, kesho sipo. Usiwe tegemezi kwa watu.

Maneno hayo yameendelea kuwa sehemu ya msukumo wa maisha yake. Badala ya kuangalia kile ambacho hawezi kufanya, Fatma aliamua kuangalia kile anachoweza kufanya na kukiendeleza.

 

UFUMAJI NA BIASHARA ILIYOMPA MATUMAINI

Mwaka 2021, Fatma alianza kujifunza na kufanya ufumaji wa mikoba kwa kutumia shanga. Ujuzi huo aliupata kutoka kwa dada yake na baadaye akaendelea kuukuza kwa juhudi zake mwenyewe.

Leo anatengeneza mikoba ya shanga na bidhaa nyingine mbalimbali. Aidha, anauza udi, haliud na mafuta ya pafyum. Baadhi ya bidhaa hizo alianza kuzifanya takribani miezi mitatu iliyopita baada ya kujifunza kupitia mitandao ya kijamii.

 

Kwa mujibu wa Fatma, sababu kubwa ya kuingia katika biashara ni kutafuta kipato cha kujikimu, kuondokana na utegemezi na kujiepusha na maisha ya kuomba msaada kila mara.

 

Nilitaka kujitegemea na kujiepusha kuwa ombaomba kwa watu. Nikaona nina uwezo wa kufanya kazi na kujenga maisha yangu kupitia biashara.

Walisema siwezi, lakini sikuacha

 

Safari ya ujasiriamali haijawa rahisi kwake. Anakabiliwa na changamoto za ukosefu wa mtaji, kupata wateja, mazingira yasiyokuwa rafiki kwa mtu mwenye ulemavu na wakati mwingine kukutana na watu wanaomdharau au kumwona hawezi kufanya biashara kutokana na hali yake.

Lakini Fatma hakukubali maneno hayo yawe hukumu ya maisha yake.

 

Sikukubali maneno yao yanivunje moyo. Niliendelea kujifunza kwa bidii na kuamini uwezo wangu. Leo bidii yangu imeonyesha kwamba ulemavu si kikwazo cha kufikia malengo yangu.

Kauli hiyo inaonesha msimamo wake wa kutokuruhusu mtazamo wa wengine uamue thamani au uwezo wake.

 


UONGOZI UNAANZIA KATIKA KUJISIMAMIA

Kwa Fatma, mwanamke anayejiajiri na kusimamia maisha yake anaweza kuitwa kiongozi. Kwake, uongozi haupo kwenye cheo pekee, bali unaonekana katika uwezo wa kufanya maamuzi, kuwajibika na kuwa mfano kwa wengine.  Biashara imemfundisha kuwa kiongozi mzuri anatakiwa kuwa mvumilivu, kujiamini, kufanya maamuzi, kusikiliza wengine na kutokata tamaa anapokutana na changamoto.

 

Amejifunza kufanya maamuzi kuhusu biashara yake mwenyewe, kuanzia kuchagua bidhaa za kutengeneza, kupanga bei, kutafuta wateja hadi kusimamia kipato chake.

 

Nimejifunza kujiamini katika maamuzi yangu na kutokata tamaa ninapokutana na changamoto.

Kwa upande wake, misingi ya uongozi bora ni kujiamini, kuwa na hekima na busara, uaminifu, uvumilivu, heshima na kuwajibika.

 

CHANGAMOTO ZA WANAWAKE WENYE ULEMAVU

Fatma anaamini kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wanawake wenye ulemavu, hasa katika kupata mitaji, masoko, mafunzo na mazingira rafiki ya kufanya shughuli za kiuchumi.

Anasema wakati mwingine jamii haiangalii uwezo wa mtu mwenye ulemavu, bali huangalia ulemavu wake kwanza. Mtazamo huo, kwa mujibu wake, unaweza kuwanyima wanawake wengi fursa ya kujiajiri na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.

 

Tusiangalie ulemavu wetu tu, bali watuangalie kwa uwezo na kazi tunazoweza kufanya. Tunahitaji kupewa fursa, kuaminiwa na kusaidiwa ili tuweze kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii.

Fatma anaomba wanawake wenye ulemavu wawezeshwe kwa mitaji, mafunzo ya biashara na utengenezaji wa bidhaa, pamoja na kusaidiwa kupata masoko.

Anaamini kuwa mazingira yakiboreshwa na fursa zikawa sawa, wanawake wenye ulemavu wanaweza kukuza biashara zao, kuongeza kipato na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

 

USHUHUDA KUTOKA KWA WATU WALIOMZUNGUKA

Mume wa Fatma, Juma Shaaban, anasema anajivunia juhudi za mke wake katika kupambana na changamoto na kujitahidi kuijenga familia.

Fatma ni mfano kwa watu wengine wenye ulemavu kwamba wanaweza kujiamini, kufanya kazi na kujenga maisha yao. Namshukuru kwa kuwa mwanamke mwenye nguvu na anayepambana kwa ajili ya familia yetu.

 

Dada yake, Muzna Suleiman Mussa, anamuelezea Fatma kama mwanamke mwenye juhudi, uvumilivu na bidii katika kujenga maisha yake na familia yake.

Najivunia kuona anavyoendelea kupambana na changamoto na kutafuta njia ya kujitegemea.

 

Naye dada yake mwingine, Khaitham Suleiman Mussa, anasema Fatma hajawahi kuruhusu changamoto zimfanye akate tamaa.

Pamoja na changamoto anazopitia, kamwe hakuwahi kukataa tamaa. Anaendelea kupambana kufikia malengo yake. Kama mdogo wake, najivunia kuwa na dada kama yeye.

 

Kwa upande wa wateja, Mauwa Aliy Khamis anasema amemfahamu Fatma kupitia biashara yake na amemuona akifanya kazi kwa juhudi, akiwahudumia watu vizuri na kwa uaminifu.

Mteja mwingine, Ali Kombo Maalim, anasema Fatma ni mwanamke anayestahili kuwa mfano kwa wengine kutokana na bidii, ujasiri na moyo wake wa kujitegemea.

 

Ulemavu haumzui mtu kufanya kazi. Fatma anauwezo wa kufanya biashara na kutoa bidhaa zenye ubora. Najivunia kununua bidhaa kwake.

 

NDOTO YA KUWAWEZESHA WANAWAKE WENGINE

Pamoja na mafanikio aliyoyapata, Fatma bado ana ndoto kubwa. Anatamani kukuza biashara yake, kupata wateja wengi zaidi na kuongeza aina na kiwango cha bidhaa anazotengeneza.

Ndoto yake kubwa zaidi ni kuona biashara yake inakuwa na uwezo wa kuwapa wanawake wengine, hasa wanawake wenye ulemavu, nafasi ya kujifunza na kujiajiri.

 

Kwa mtazamo wake, mafanikio si kupata pesa pekee. Ni uwezo wa kujitegemea, kufanya kazi unayoipenda, kushinda changamoto na kuwa mfano kwa wengine.  Anasema mafanikio anayojivunia zaidi ni kujifunza ufumaji, kuanzisha biashara yake mwenyewe na kufikia hatua ya kujitegemea licha ya changamoto anazokutana nazo.

 

UJUMBE KWA WANAWAKE WENYE ULEMAVU

Fatma anatoa wito kwa wanawake wengine wenye ulemavu kutokata tamaa wala kujiona hawawezi.

Kila mtu ana uwezo wake. Changamoto hazimaanishi huwezi kufanikiwa. Jiamini, anza pale ulipo na endelea kujifunza. Mungu akipenda, juhudi na uvumilivu vinaweza kukufikisha kwenye mafanikio.

Anaamini kwamba mtu hapaswi kusubiri mpaka apate kila kitu ndipo aanze. Anachohitaji ni kujiamini, kuanza na kile alichonacho na kuendelea kuongeza ujuzi.

 

WITO KWA JAMII NA VIONGOZI

Fatma pia anaiomba jamii ibadili mtazamo kuhusu wanawake wenye ulemavu na kutambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya maendeleo.  Kwa viongozi, anaomba kuwepo kwa mazingira wezeshi zaidi, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mitaji, mafunzo ya ujasiriamali na masoko ya bidhaa zinazotengenezwa na wanawake wenye ulemavu.

 

Pia anataka wanawake wenye ulemavu wasikilizwe na kushirikishwa katika mipango ya maendeleo kwa sababu wana uwezo wa kufanya maamuzi, kuwajibika na kutoa mchango katika jamii kama watu wengine.

 


SHERIA INASEMAJE

1. Kifungu cha 4 Kanuni za msingi

Sheria Na. 9 ya 2010, Kifungu cha 4 kinaweka misingi ambayo Serikali na jamii wanapaswa kuzingatia kuhusu watu wenye ulemavu.

 

Misingi hiyo inajumuisha:

kuheshimu utu wa mtu mwenye ulemavu;

kutokubagua mtu kwa sababu ya ulemavu;

ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika jamii;

 

usawa wa fursa;

upatikanaji wa huduma na mazingira;

usawa kati ya wanaume na wanawake wenye ulemavu; na

kiwango cha msingi cha maisha na ulinzi wa kijamii.

Maana yake kwenye biashara: mtu mwenye ulemavu hapaswi kunyimwa fursa ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa sababu tu ana ulemavu.

 

HITIMISHO

Hadithi ya Fatma Suleiman Mussa si hadithi ya ulemavu pekee; ni hadithi ya moyo wa kupambana, kujiamini na kukataa kuruhusu changamoto kuamua mwisho wa maisha. Kutoka kwenye kukata tamaa akiwa mdogo hadi kujifunza ufumaji, kuanzisha biashara na kujitahidi kujitegemea, Fatma ameonyesha kuwa uwezo wa mtu haupaswi kupimwa kwa hali yake ya mwili.  Safari yake inatoa somo kwa jamii kwamba fursa inapopewa mtu, inaweza kubadilisha maisha yake; lakini fursa inaponyimwa kwa sababu ya ulemavu, jamii nzima hupoteza mchango wa mtu huyo.

Fatma anaendelea kuamini katika uwezo wake, kumtegemea Allah na kufanya kazi kwa bidii. Ndoto yake si kujikwamua yeye mwenyewe pekee, bali pia siku moja kuwawezesha wanawake wengine wenye ulemavu kujifunza, kujiajiri na kujitegemea.

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da...

Vikausha damu vya mjamzito hivi hapa, umo mchele, udongo, mkaa, chaki Uwezekano wa kuzaliwa watoto wenye udumavu, utapiamlo ni mkubwa

  NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@ ‘’KILA ninapobeba mimba nimezoea kula mchele kwa wingi naweza kusamehe pilau au biriani,’’ ndio maneno ya mwanzao ya Bahati Mohamed Ali (sio jina lake halisi). Nilimfuma akiwa barazani kwake, mjini Ole wilaya ya Chake chake, pembeni yake akiwa na kibakuli cha mwazi, kwa umbali utaona amejaza chakula aina ya pepe, kumbe ni mchele wa Mbeya. Hujichotea kidogo kidogo na kuushindilia mdomoni mwake, huku akiendela kupiga storia na wenzake, bila ya kujali kuwa ujauzito alionayo na mchele huo hauna mwisho mwema. Kawaida yake akiwa mjamzito, kila anapoamka asubuhi anaroweka mchele upatao robo kilo hivi…na baada ya kumaliza kupika, yeye huchukua mchele wake kutafuna (kula). Wakati mwenza wake na watoto wao, wanakula chakula cha mchana, Bahati yeye hukaa pembeni na kibakuli chake cha mchele akiendelea kubahatisha afya yake. ‘’Mimba nyengine hupenda sana kutafuna mchele wa Mbea na nyengine hupenda mchele wa mapembe, kwa kweli huwa nina hamu (kileo), kwan...

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’...

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 m...

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa uf...