NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
….kilimo ni maji,
na maji ni kilimo…
Maji ndio mama wa taifa wa kilimo, bila ya maji hakuna kilimo.
Akasema, kama
mataifa yana baba wa taifa, basi kwenye kilimo, baba wa taifa ni maji.
Kelvin John Musetepe
wa Burundi mtaalamu wa kilimo cha umwagiliaji, mwaka 2000, alimwambia Waziri wa
kilimo nchini humo, kama hakuna maji, basi hakuna kilimo.
Waziri huyo, alikuwa
ameshaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri wa maji, miezi mitatu iliyopita, jambo
lililomkasirisha.
Rais wa awamu ya
nane ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, wakati akilihutubia Baraza la Wawakilishi,
aliiagiza wizara husika, kuhakikisha huduma ya maji, iko vizuri.
‘’Sasa huduma ya maji
sio tu kwa ajili ya matumizi ya ndani, kama kupikia na kunywa, sasa ni kwa
ajili ya kuendeleza kilimo kwa manufaa mapana,’’akafafanua.
Akaenda mbali zaidi
kuwa, bila ya kuwa na maji endelevu, hakuna kuvuna matunda na mazao ya uhakika Zanzibar.
Mpaka mwaka 2025,
kupitia mradi wa uhuishaji na uimarishaji wa huduma za maji Zanzibar, matangi 15
yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 134 yalishajengwa.
Taarifa ikafafanua
kuwa, eneo jingine ni uchimbaji wa visima 64 yenye uwezo wa kuzalisha lita 177,000,000
kwa saa, vinaendelea kutumika Zanzibar,
Taarifa ya wizara
ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar ya mwaka 2022/2023 ilisema,
visima vitano katika bonde la wakulima Cheju, vimeshachimbwa, kwa ajili ya umwagiliaji.
Ikafafanua kuwa, visima
vyingine 20 katika mabonde ya wakulima ya Kibokwa, Kilombero na Cheju, vimewekewa
pampu, kwa ajili ya kusukumia maji, kwenye mashamba yao.
Kimataifa, lengo la
sita, kati ya yale Malengo Endelevu 17 ya dunia, linagusia maji safi na salama,
kama lilivyo la 14, lililosisitiza, kuendelea uhai wa katika maji.
WAKULIMA KILIMO
MSITU UNGUJA NA PEMBA WANASEMAJE
Wanaufaika 2,749 wakiwemo
wanawake 2,086 na wanaume 663 wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko tabianchi, ‘ZANZ
ADAPT’ wanaendesha kilimo msitu.
Shehia ambayo ilitoa
wanufaika wingi ni Uzi Unguja kuwa na 636, wakiwemo wanawake 508 na wanaume
128, ikifutiwa na Unguja Ukuu, iliyobeba wanufaika 385, ikiwa na wanawake 222
na wanaume 163.
Shehia ya Kambini Pemba,
inao wanaufaika 374, Mchanga mdogo 253, Kiuyu Minungwini 305, Chwale 271, Ng’ambwa
266, na Bungi wanufaika 259.
Mradi huo wa ‘ZANZ
ADAPT’, wa miaka mitano, utatia nanga mwaka 2029 utekelezaji wake, umekusanya
wanufaika wanawake 2, 086 na wanaume 663 kwa Unguja na Pemba.
Ambapo awali,
walishapewa mafunzo kwa miezi zaidi ya 18 iliyopita, na Jumuiya ya Uhifadhi ya
Misitu Pemba ‘CFP’ wakishirikiana na Jumuiya ya kimataifa kama hiyo ‘CFI’.
Mkurugenzi wa ‘CFP’
Mbarouk Mussa Omar, baada ya mafunzo hayo ya kilimo msitu, walengwa hao wa
mradi walitakiwa kwenda kuanza uotesha wa miti ya chakula na biashara.
Mradi huo upo kwa
wananchi wa shehia nane, za Uzi, Bungi, Unguja Ukuu na Ng’ambwa kwa Unguja na
Mchanga mdogo, Kambini, Chwale na Kiuyu Minungwini kwa Pemba.
WAKULIMA WALITII
AGIZO HILO?
Makala hii
ilizungumza na wakulima wanufaika wa shehia ya Mchanga mdogo wilaya ya Wete,
akiwemo Fatma Bakari ambae kwa sasa, anayomashamba matatu.
‘’Baada ya mafunzo,
kweli niliingia shambani na kuanza kupanda mitondoo 500, migomba 200, minanasi
200, miparachichi 50, na nimeshaanza kuvuna ndizi,’’anasema.
Kwake, jambo la
shilingi 50,000 hadi shilingi 100,000 wala sio jambo la kuutesha moyo wake,
kama ilivyo kabla ya kujiingiza kwenye kilimo hicho.
Mkulima Mtumwa
Makame Shaame wa kijijini hapo, anasema ameitikia wito huo, akiamini kwanza
atapata fedha za baada ya kuuza bidhaa zake, huku akikabiliana na mabadiliko tabianchi.
‘’Kwa hakika mradi
huu, umekuja kutupa uwezo na mbinu za kukabiliana na mabadiliko tabianchi, huku
tukijihakikishia chakula na fedha,’’anaeleza.
Mwenyewe amepanda
mitondoo 50, migomba 150, minanasi 80, mihogo mashina 200 ambapo ameshaanza
kuuza na kujiingizia fedha.
‘Sasa najiona
mwanamke shujaa, maana najiendesha kwa kipato cha kilimo msitu, na huku nikijihakikishia
chakula na matunda,’’anasema.
Sasa amekuwa hana hofu
na michango ya familia, fedha za akiba na matumizi madogo madogo, mana suala la
shilibgi 40,000 hadi shilingi 50,000 sio ajenda kwake.
Hata Zaituni Hassan
Ali, anasema sasa anaona njia ya kujihakikishia kipato imeshachomoza, baada ya
kupewa mafunzo na kuanza kilimo msitu.
‘’Na mimi nalima
kilimo msitu ‘mchanganyiko’ faida yake, yamo mazao ya muda mfupi kama ndizi na
muhogo, ya muda wa kati, kama mananasi na yale wa muda mrefu, kama miti ya
ujenzi,’’anaeleza.
‘’Kwangu sasa kumiliki
shilingi 30,000 hadi shlingi 200,000 najiamini maana kila siku 90, naingia
shambani kuvuna mazao,’’anafafanua.
Wao wanaona
kizinngiti kubwa, kwenye kilimo chao ni ukosefu wa huduma ya maji ya umwagiliajai,
licha ya ahadi waliopewa na CFP, kwamba bado haijawafikia.
Wanakiri kuwa,
kipindi cha jua, miti husinyaa na kupoteza mwelekeo, jambo linalowafanya baadhi
yao kukata tamaa, kuendelea na kilimo hicho.
CHANGAMOTO YAO YA
UKOSEFU WA MAJI ‘CFP’ WANAYO?
Uongozi wa Jumuiya
ya uhifadhi wa misitu Pemba ‘CFP’ umeanza kutekeleza ahadi ya uchimbaji wa
visima, kwa ajili ya wakulima wa kilimo msitu, kama walivyowaahidi.
Mkurugenzi Mtendaji
‘CFP’ Mbarouk Mussa Omar, anasema, tayari wameshaanza zoezi la uchimbaji wa
visiwa, unaolenga kuwasaidia wakulima hao.
Tena, wameanzia
katika shehia ya Kiuyu Minungwini, na kwa hatua za awali, kisima kimoja, chenye
kuzalisha wastani maji lita 50,000 kwa saa kimeshakamilika.
Kisima hicho,
kimeshajengewa mnara wenye urefu wa mita nne, ambao utakuwa na matenki manne,
yenye kuhifadhi maji ujazo wa lita 20,000 ni lita 5,000 kwa tenki.
Kisima hicho kwa
sasa wanaendelea kufanya mazungumzo na Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ kwa
ajili ya kuwahakikisha upatikanaji wa huduma ya umeme.
‘’Ni kweli uongozi
wa ‘CFP’ wakati waziri wa Kilimo alipowatembelea wakulima wa kilimo msitu
shehia ya Mchangamdogo, tuliahidi kuwapatia huduma ya maji, na sasa tumeshaanza
kutekelez ahadi hiyo,’’anafafanua.
Anaelekeza kuwa,
kwa hatua za awali, utahusisha kisima kimoja kimoja, kwa shehia zote nane za
Unguja na Pemba, ambazo mradi wa uhifadhi wa mazingira ‘ZANZ ADAPT’ unatekelezwa.
Ingawa baada ya
kupata mwelekeo wa visima vya awali vinane, mradi utaendelea na uchimbaji tena
wa visima vyingine kama hivyo.
‘’Kama mradi
utakwenda vyema, lengo ni kila shehia zinazotekeleza mradi huu, kuwachimbia visima
vitatu vitatu na miundombini yake, ili wakulima wa kilimo msitu, wawe na umwagiliaji
wa uhakia,’’anafafanua.
TAMWA WALIFANYAJE
KWENYE MRADI HUU
Kaimu Mratibu wa
Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba,
Amina Ahmed, anasema kwanza waliwajengea uwezo wanaufaika kuzungumza na vyombo
vya habari.
‘’Hapa lengo lilikuwa
ni kuwawezesha wanufaika hao, kuzungumza na vyombo vya habari, iwe pale
wanapokumbana na changamoto au manufaa ya kazi zao waweze kujitetea,’’anaeleza.
Eneo jingine waliwawezesha
waandishi wa habari, ili kuandikia fursa zilizomo kwenye mradi huo, ikiwemo wanufaika
wakati wanakabiliana na mabadilikotabia nchi, kujiongezea kipato.
Anaeleza kuwa,
ndani ya vikundi walivyovianzisha wanufaika, suala la uongozi, nafasi ya wanawake,
njia ya kujiingizia kipato na kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, liliandikwa.
MCHANGO WA SERIKALI
KUU KWENYE KILIMO
Aliyekuwa Waziri wa
Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, akisoma bajeti ya
mwaka 2025/2026, alisema mwaka 2021, sekta ya kilimo, imechangia
asilimia 24.6 ya pato la taifa, ikilinganishwa na asilimia 22.8 iliyoripotiwa
mwaka 2020.
Akafafanua, kwa mwaka 2024, sekta hiyo ilichangia
asilimia 24.3 ya pato la taifa, ikilinganishwa na asilimia 24.9 iliyoripotiwa
mwaka 2023, ambapo hiyo inaonesha kuimarika kwa sekta nyingine zinazohudumiwa
na sekta ya kilimo.
Ingawa akafafanua kuwa, uzalishaji wa mazao ya kilimo
umepungua kwa tofauti ya tani 144,870.8, kutoka tani 527,800 mwaka 2023,
ikilinganishwa na tani 382,929.2 mwaka 2024, upungufu huo umetokana na kuwepo
kwa vipindi virefu vya mvua na jua visivyotabirika.
Akabainisha kuwa, wizara imekuwa ikifanya jitihada za
kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, toka mwaka 2017, ambapo hadi sasa eneo
lililowekewa miundombinu hiyo, imefikia ekari 5,750, sawa na hekta 2,300.
Kwa upande wa mazao ya misitu, takwimu zinaonesha
kuwa mwaka 2024, matumizi ya kuni yamepungua kutoka mita za ujazo 25,909.7
mwaka 2023, hadi kufikia mita za ujazo 18,764.5 mwaka 2024.
Eneo jingine ni uzalishaji wa nguzo kubwa za miti,
umepungua kutoka mita za ujazo 2,084.8 mwaka 2023 hadi kufikia mita za ujazo
1,259 mwaka 2024.
Aidha Waziri huyo, amaesema kwa ujumla, matumizi ya
kuni yamepungua, kutokana na juhudi zinazochukuliwa ya kuhamasisha wanajamii,
katika uhifadhi misitu inayowazunguka na matumizi ya gesi.
Mwisho

Comments
Post a Comment