NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MOJA ya sheria kongwe na inayotajwa kutokwenda sambamba na uhuru wa vyombo vya habari, ni ile nambari 5 ya mwaka 1988 ya Magazeti, Vitabu na Mawakala wa Habari Zanzibar.
Ni miaka 36 sasa, sheria hii inaendelea kutumika Zanzibar, na kutajwa kuathiri na kutishia utendaji kazi wawaandishi wa habari visiwani.
HISTORIA
Sheria hiyo tokea mwaka 2010, ilianza harakati za kutaka kufutwa, kwa wadau wa habari kujikusanya pamoja, ili sasa iwe na sheria moja ya habari.
Kwa wakati huo, tasisi za Baraza la Habari Tanzania ‘MCT’ –ofisi ya Zanzibar, vyama vya waandishi wa habari, taasisi za haki za binadamu na wizara husika, zilianza harakati hizo.
Mara kadhaa, kulikuwa na taarifa kuwa, mwaka ujao au mwakani Zanzibar itapatikana sheria mpya ya habari, ambayo itakuja kufuta sheria ya Magazeti nambari 5 ya mwaka 1988 na ile ya Tume ya Utangaazji nambari 7 ya mwaka 1977.
Ilikuchakua takriban miongo miwili, kupita bila Zanzibar kuwa na sheria mpya, ingawa kwa Tanzania bara, wao walifanikiwa kufuta sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, na kuwa na sheria ya Huduma ya vyombo vya habari ‘MSA’ ya mwaka 2016.
Aliyewahi kuwa Katibu mkuu wizara ya Habari Ali Mwinyikai, alisema iko siku Zanzibar, itakuwa na sheria bora na iliyorafiki kwa waandishi wa habari.
Hata aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa shirika la Magazeti ya serikali Zanziba Abdalla Mohamed Juma, aliwahi kusema, sheria ya magazeti, iliyopo sasa, haiendani na upevukaji demokrasia na uhuru wa habari.
Kwa miongo miwili, wadau wa habari juhudi zao za kuwa na sheria mpya ya habari ziligonga ukuta, na harakati hizo zikaanza tena baina ya miaka ya 2018/2019.
YANAYOWASKUMA WADAU KUFUTWA KWA SHERIA YA MAGAZETI, VITABU NA MAWAKALA WA HABARI NO 5, 1988.
Sheria hii yenye vifungu 81 na sehem 10, sasa inatimiza miaka 36, tokea kutungwa kwake, na kwa maana nyingine, vipo vifungu zaidi ya 40, ambavyo vyengine vinahitaji kufutwa.
Vifungu vyingine vikihitajika kufanyiwa marekebisho na vyingine, vilivyobeba maneno makali kama uwezo wa waziri, waandishi kudhibitiwa na kufanya uchochezi.
Kwenye sheria hii, ambayo kwa sasa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, wanaharakishwa kufutwa kwa sheria hiyo na kuwa na sheria bora na rafiki.
VIFUNGU KANDAMIZI KWA UHURU WA HABARI
Moja ya kifungu ambacho, kwa sasa wadau wanataka kifutwe ni kile cha 43, ambacho chenyewe, kinaeleza ‘uwezo wa ofisa aliyeidhinishwa’.
Ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, ofisa aliyeidhinishwa ni Polisi mwenye cheo cha Msaidizi Ofisa Mkaguzi au mwenye cheo cha juu ya hapo.
Mkufunzi Mshauri na mchambuzi wa sheria za habari Zanzibar Hawra Shamte anasema, kwa sasa sheria hiyo na hasa kifungu cha 43 wanakiona, hakina mantiki.
‘’Makosa yote yanayotokana na waandishi wa habari yana sura ya madai na, sasa iko wapi nafasi ya Polisi kuingia, kupekua kwenye vyombo vya habari,’’anahoji.
Ukali wa mchambuzi huyui, unajidhihirisha kwenye kifungu hicho cha 43 (1) na (2) ambavyo vimeeleza wazi mamlaka ya ofisi huyo wa Polisi.
‘’Mfano kifungu (2) (a) kinaeleza uwezo wa ofisi huyo kuwa ‘anaweza kuingia sehemu yoyote, jengo, chombo cha ardhini, angani ambamo anaamini kwa maoni kuwa, mna vifaa vya habari, vilivyopangwa au vitakavyopangwa kukusanyia habari,’’
Hata kifungu kidogo cha 2 (b) kikaongeza kuwa, ofisi huyo anaweza ‘kuchunguza mchakato wowote ambao unaonekana kuelekea kukusanya au kutoa habari yoyote ’.
Kubwa zaidi ambalo ni ukiukwaji wa uhuru wa habari, kifungu cha (c) kinampa uwezo ofisi hiyo ‘kumtaka mwandishi wa habari yeyote, kutoa vitendea kazi vyake, gazeti au waraka ambao, uko chini yake kukabdhi kwake’.
Kifungu 2 (d) ofisi huyo amepewa mamlaka ya ‘kunakili sehemu yoyote ya vitendea kazi vya waandishi wa habari au akiamiani tu kufanya hivyo, kuna uhusiano na uchunguuzi wake juu ya kosa chini ya sheria hii’.
Kubwa zaidi, pia ofisi hiyo kwenye kifungu hicho cha 43 (2) (e) anaweza ‘kuagiza taarifa zenye uhusiano na uchunguuzi wake kutoka kwa mtu yeyote, ambae anaamini aliajiriwa au ataajiriwa katika jengo alilokuwa akitunza kumbu kumbu’.
Pamoja na uwezo huo, ambao wadau wa haki za uhuru wa habari wanaona ni uminywaji wa haki za waandishi wa habari, sasa kifungu cha 44 kimekuja kumlinda.
Kifungu hichi (1) kinaeleza kuwa, ‘mtu yeyote atakayempinga, kumzuia, au kumkwaza kwa ofisa huyo atakuwa ametenda kosa’
Na adhabu kwa kosa hilo lipo kifungu cha 73, ambapo ni faini ya shilingi 200,000 au kifungo cha miaka miwili chuo cha mafunzo au adhabu zote mbili kwa pamoja.
WADAU WA HABARI WANASEMA JE?
Mkurugenzi wa Jamii tv ya mtandaoni, Ali Massoud Kombo, anasema kifungu hicho sio rafiki, na hakitarajii kukiona kwenye sheria mpya ijayo ya habari.
Anasema, studio na vyumba vya habari ni ofisi nyeti kama zilivyonyingine, hivyo utaratibu wa kuingia, uwepo kama zilivyo ofisi nyingine.
‘’Mbona Ikulu, wodi ya wazazi, kambi za Jeshi na hata chuo cha mafunzo kuna utaratibu wake, na sio ofisa yeyote tu Polisi tena kwa maoni yake aweze kuingia,’’anahoji.
Mmiliki wa mawio tv online Suleiman Rashid Omar, anasema kifungu hicho hakifai kuwepo, maana kinahalalisha ukandamizaji wa uhuru wa waandishi wa habari.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania ‘MCT’ Ernest Sungura wakati akizungumza na wanachama wao kwenye mkutano mkuu wa 27 uliofanyika ofisi ya MCT Tegeta, alisisitiza vyombo vya dola kuwaachia waandishi watekeleze kazi zao.
‘’Kuwapasha habari wananchi juu ya matukio ya ndani na nje ni haki kikatiba, sasa kama kuna sheria au kifungu kinampa uwezo mkubwa Polisi, kuingia na kufanya atakavyo sio sahihi,’’anasema.
Aliyekuwa Mratibu wa TAMWA -Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, anasema uhuru wa waandishi wa habari, ni mbolea kwa taifa kutimiza malengo yake.
‘’Lakini sheria yetu ya Mgazeti nambari 5 ya mwaka 1988 ya Zanzibar na hasa kifungu cha 43 kinaipinga hata katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyotoa haki ya kutoa maoni,’’anaeleza.
Mjumbe wa Kamati tendaji wa Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAZA’ Hidaya Mjaka Ali, anasema sheria bora ni chachu ya kupata waandishi wa habari bora.
Mkurugenzi wa vijana Pemba Ali Mussa anasema wanawategemea mno waandishi wa habari, kuwaibulia changamoto za vijana na kuwaonesha njia.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa kuskazini Pemba Juma Saadi Khamis anasema, sio maeneo kama vyumba vya habari kuwa ofisa, anaweza kuvamia ikiwa hakuna uhalifu.
Aliyekuwa Mdhamini wa Baraza la Habari Tanzania MCT-Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema sheria hiyo imeshapitwa na wakati na moja ya vifungu vibaya ni cha 43.
Mchambuzi wa sheria za Habari Zanzibar Hawra Shamte anasema, kwenye nchi zinazojali kwa vitendo utawala bora na utawala wa sheria, suala la kupata na kutoa habari haliwekewi masharti mazito.
Mkuu wa taaluma wa Chuo cha uandishi wa habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar Imane Duwe, anasema dunia ikisherehekea ukuaji wa teknologia kwenye eneo la habari, lazima waandishi wawe huru.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar ‘ZPC’ Abdalla Abudull-rahman Mfaume na mwenzake wa PPC Bakari Mussa Juma, wanasema vifungu ambavyo vinampa wasi wasi waandishi wa habari, havina nafasi Zanzibar.
NINI KIFANYIKE?
Aliyekuwa Kaimu Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Pemba Safia Saleh Sultan, anasema lazima kwenye sheria ijayo ya habari, kifungu hicho kifutwe.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wasioona ‘ZANAB ‘Pemba Suleiman Mansour, amesema suala la vyumba vya habari au wao wenyewe kupekuliwa lisiwe la kila ofisa wa Polisi.
‘’Sheria ijayo ya habari, sitamani kurejeshwa kwa kifungu hichi, maana kwa upande mwingine ni kudhoofisha juhudi za waandishi katika kazi zao,’’anasema.
Afisa Mdhamini wizara ya Habari Pemba Mfamau Lali Mfamau, anasema ukandamizwaji wa waandishi wa habari, hudhoofisha maendeleo ya taifa.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mjaja, anasema sheria bora ya habari huchangia kuwa na jamii bora, na inayofanya uamuzi sahihi.
Zuhura Juma Said mwandishi wa habari wa shirika la Magazeti Pemba, anasema sheria hiyo ya Magazeti, Vitabu na Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988, imekuwa kikwazo kwao.
Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzur Issa Ali, anasema ujio wa sheria mpya ya habari vifungu vinavyompa uwezo mkubwa waziri visiwmo.
‘’Ndio maana TAMWA -Zanzibar kwa kushirikiana na wafadhili wetu Shirika la Internews Tanzania tunaomradi wa miezi minne, ili kuwawezesha waandishi, kusukuma upatikanaji wa sheria mpya habari Zanzibar,’’anasema.
WIZARA YA HABARI ZANZIBAR
Tabia Maulid Mwita, anasema mchakato wa upatikanaji wa sheria bora na rafiki Zanzibar, umewiva maana mswada wa sheria ambayo imejali maoni ya wadau, itafikishwa Baraza la wawakilishi wakati wowote.
Mwisho
Comments
Post a Comment