NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
NI takriban miaka 20 sasa, shauku ya waandishi wa habari pamoja na watetezi wengine wa haki za binaadamu Zanzibar, kuona nchi yao inapata sheria rafiki za habari imekuwa ikitimizwa kwa maneno.
Viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini, wamekuwa wakitoa ahadi lakini utekelezaji wake unasuasua.
Tangu alipoingia madarakani, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akionesha kutambua umuhimu wa sekta ya habari kuwa na sheria bora na rafiki.
Akiwa amekalia kiti cha Ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Dk. Mwinyi hakuchukua muda alitoa matamshi yenye mtazamo wa kupendelea waandishi wawe na uhuru zaidi wa kufanya kazi zao.
Mara baada ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutoa ripoti ya utendajikazi wa vyombo vya habari, mwaka 2021/2022, ikieleza kuwa Zanzibar inahitaji sheria “mpya kabisa” za kusimamia sekta ya habari.
Serikali ilijikuta inakumbushwa jukumu au wajibu wa kufanyia kazi suala hilo, kwa kuwa limepigiwa kelele kwa muda mrefu bila ya mafanikio.
Harakati za waandishi na wadau kutaka mageuzi ya sheria zilianza tokea mwaka 2002, na zilipitia kwenye nyanja mbali mbali.
Ni hapo, Dk. Mwinyi alipojibu kutambua “sheria za habari za Zanzibar ni za muda mrefu na Serikali anayoiongoza ipo tayari kushirikiana na wadau wa habari, kuzifanyia kazi kulingana na mapendekezo yatakayotolewa.
Ilipofika mwaka 2023, kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mei 3, Rais Mwinyi aliiambia hadhara kwamba, serikali itaendelea kuheshimu na kuthamini haki ya uhuru wa habari na kujieleza.
Maadhimisho yalifanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege nje kidogo ya mjini wa Unguja.
“Serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vyote vya habari, katika kuhakikisha inatatua changamoto zinazowakabili wanahabari,” alisisitiza.
Mbele ya Rais, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, akikazia muelekeo wa Rais, alisema mchakato wa sheria ya habari Zanzibar umefikia asilimia 80, kubwa akawaomba wadau wawe na subra.
“Serikali yenu ni sikivu, tunawahakikishia kuwa na sheria nzuri zitakazokidhi matakwa ya sasa, tutawasilisha Baraza la Wawakilishi na taratibu nyingine ziendelee,”alisisitiza.
Kuonesha kuwa serikali inakumbuka kilio cha waandishi wa habari, kutaka sheria rafiki za kusimamia sekta ya habari, na kwamba haijasahau wajibu wake wa kuona hilo limetimia.
Serikali ilirudia msimamo wake wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani Mei mwaka 2024.
Katika maadhimisho yaliyoandaliwa na kuratibiwa na serikali kupitia Wizara ya Habari, tarehe 4 Mei, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Hamad Rajab akimwakilisha Waziri Tabia, alisema mageuzi ya sheria ni lazim.
“Serikali itahakikisha mageuzi ya sera na sheria za habari nchini yanaenda sambamba na kanuni pamoja na maadili ya vyombo vya habari,”alisisitiza.
Kauli hiyo ilizingatia kauli mbiu ya kitaifa ya wadau wa habari Zanzibar ya mwaka huu 2024, iliyosema, ‘Uhuru wa Vyombo vya Habari, Mageuzi ya Sera na Sheria za Habari Zanzibar.”
Kaulimbiu hii ilitiliwa mkazo na mantiki yake kufafanuliwa vizuri Mei 23 mwaka jana, wakati wa wadau wa taasisi za habari na washirika wao, katika utetezi wa haki za binaadamu.
“Kwa sasa sheria ya habari, ipo kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali na tunatarajia hivi karibuni itapelekwa Baraza la Wawakilishi, kama mswaada na tunaomba walioko huko waichangie vizuri,’’alifafanua.
Utambuzi wa uhuru wa vyombo vya habari, unaanzia Umoja wa Mataifa, ambako mwaka 1948 Baraza lake la Usalama lilipitisha azimio lililojenga msingi wa imani, kwamba ni muhimu haki na uhuru wa vyombo vya habari.
Ikijumuisha uhuru wa kupata habari na ule wa watu kujieleza, ukaheshimiwa na kulindwa, kama ilivyo kwenye Ibara ya 19 ya tamko hilo.
Zanzibar ilikuja kutambua rasmi haki na uhuru wa habari ilipoandika katiba yake ya pili mwaka 1984, baada ya kufutwa kwa Katiba ya kwanza ya mwaka 1963 na kuweka dhima katika Ibara ya 18.
Miaka minne baadaye, yaani mwaka 1988, ilitunga sheria ya kwanza ya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu na. 5 ya mwaka 1988.
Ikapata marekebisho ya kwanza kupitia Sheria Na. 8 ya mwaka 1997, ambapo sheria nyingine maarufu ni iliyohusu utangazaji ambayo ni ya Tume ya Utangazaji Zanzibar Na. 7 ya mwaka 1997.
Ni msimamo wa waandishi na taasisi za kibahari kwamba sheria hizi haziendani na mazingira ya sasa.
Ni kongwe zinazopingana na dhamira na dhima ya kuheshimu na kulinda haki na uhuru wa habari.
Sheria hizi zinatajwa kuzorotesha wananchi kufaidika na uhuru unaokusudiwa na umoja wa mataifa.
Kwa mfano, kifungu cha 27(2) cha Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya 1988 kinasema.
“Hakimu yeyote anaweza kutoa hati kumuidhinisha Afisa wa Polisi mwenye cheo cha Inspekta kwa msaada au bila msaada, kuingia na kupekuwa mahali popote pale inaposhukiwa’’.
Kwamba kuna gazeti linachapishwa kinyume na sheria hii, au kanuni zozote zililotungwa, ama limefanya au linafanya au linakaribia kufanya kosa, hivyo anaweza kukamata gazeti lolote.
Kifungu kikafafanua kuwa, linalopatikana humo ama kwa kushuku kuwa kuna gazeti lililochapishwa au linachapishwa pamoja na ushahidi mwingine wowote, kwa kutenda kosa chini ya sheria hii.
Kwa muktadha huo, kifungu cha maneno yaliyotumika yana utata ndani yake, maana hayaeleweki sawasawa kwa sababu kimekusanya maneno mengi na tata, yasiyofahamika.
Hawra Shamte, mwandishi mwandamizi nchini, akigusia ubaya wa kifungu hicho, anasema, “kinampa mamlaka Hakimu atowe kibali kwa Inspekta wa polisi kupekuwa jengo kwa kushuku tu,’’anasema.
“Hichi kifungu hakiko sawa na kina dalili za ukandamizaji wa uhuru wa habari, kwa sababu hatwendi kwa dhana na shuku, hivyo tunashauri kifutwe,” anasema.
Malalamiko pia yanaihusu sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar Na. 7 (1997), kwamba inawapa viongozi wa serikali mwanya wa kuingilia shughuli za utangazaji.
Mwandishi mwandamizi wa habari nchini, Salim Said Salim anasema, sheria hii inaipa nguvu Tume ya Utangazaji, kufungia na kufutia leseni vyombo vya utangazaji, hivyo kwenda kinyume na viwango vya kimataifa.
Mwanasheria na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Said Ali, anasema Sheria ya Tume ya Utangazaji, inatoa mamlaka makubwa kwa viongozi serikalini, kuchukuwa maamuzi yoyote anayoona yanafaa.
“Kifungu 27(2), Waziri amepewa mamlaka ya kuchukua maamuzi yoyote, mfano kama ana tofauti binafsi na mtu fulani ambae ni mmiliki wa chombo, anaweza akaitumia vibaya sheria,"anasema.
Mwandishi Masanja Mabula wa Channel Ten kanda wa Pemba, anahofia kuendelea kwa sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar, kutasababisha waandishi kutofanya kazi kwa uhuru.
Mwanasheria Shadida Omar kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania (THRDC), anasema ili kuona uhuru wa kujieleza unafanikiwa, waandishi wanadhima ya kupaza sauti wakiwa huru.
“Hapa kwetu Zanzibar zipo sheria nyingi zinabadilishwa mara kwa mara, inashangaza hizi sheria zinazohusu habari zinacheleweshwa, wakati inajulikana wazi kuwa ni za zamani,”anahoji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Habari Zanzibar (ZAMECO) Abdalla Abdull-rahman Mfaume, anasema jitihada zinahitajika kwa waandishi kuendelea kudai sheria mpya ya habari.
JUHUDI ZA TAMWA
Mwneyekiti wa Program ya uchechemuzi wa upatikanaji wa sheria mpya za habari kutoka TAMWA Zanzibar Zaina Mzee, anasema hawalali mpaka sheria mpya ipatikane.
Walichokifanya kwanza, ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari na wadau, ili kuzijua sheria hizo na kuvijua vifungu vyenye utata.
‘’Lakini sio vyenye utata pekee, hata ambavyo vinakinzana na uhuru wa habari na kujieleza, maana tusipokuwa na waandishi huru hakuna maendeleo,’’anasema.
Hata hivyo, anaishauri serikali iongeze kasi katika mpango wake kazi, wa kuwa na sheria mpya ya habari, na kuzifuta zilizopo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment