NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKURUGENZI Baraza la Manispaa ya Chake chake Maulid Mwalim Ali, amewataka watumishi wapya wa umma kisiwani Pemba, kutotegemea waganga wa kijienyeji, kutafuta vyeo katika ofisi zao, na badala yake wafanye kazi kwa bidii kwani ndio msingi mkuu.
Alisema, huu sio wakati tena wa kuelekea kwa wapigamrali, ili kusaka vyeo, bali mchawi wa hilo ni kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi na bila ya ubaguzi.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo jana, ukumbi wa Manispaa hiyo alipokuwa akiyafunga mafunzo ya siku mbili, kwa watumishi wapya wa umma, kuhusu uthibitisho wa kazi baada ya kuajiriwa.
Alisema, nidhamu, utendaji kazi uliotukuka, heshima na kutoa huduma bora, ndio chanzo cha wao kupanda daraja katika maeneo yao ya kazi.
‘’Niwaombe sana watumishi wenzangu wa umma, kuhakikisha mnakwenda kufanyakazi kwa bidii na nidhamu, kwani huo ndio msingi mkuu wa kupanda daraja,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo, amewataka watumishi hao wapya, kujenga umoja na mshikamano miongoni mwao, ili kufanikisha kazi zao.
Hata hivyo, amewakumbusha kuzisoma kwa umakini sheria na kanunuzi za utumishi wa umma, ili wajuwe kwa undani haki na wajibu wao.
Akiwasilisha mada ya maadili kwa watumishi wa umma Mkuu wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar ‘IPA’ tawi la Pemba, Juma Haji Juma, alisema msingi mkuu wa maadili ni kujielekeza katika utendaji wa kazi.
Alisema msingi mwingine ni kujielekeza kwa mpewa huduma, tena iwe kwa hali ya juu, kwa wakati na bila ya kujichelewesha wakati uliopangwa.
Aidha Mkuu huyo wa Chuo cha IPA, aliwafahamisha watumishi hao wapya wa umma kuwa, msingine mwingine wa maadili ni wajibu wa kuitumikia mamlaka ya nchi.
‘’Kwa mfano kutii maagizo na miongozo ya serikali iliyopo madarakani ni jambo la lazima, katika kufikia azma ya maadili kwa mtumishi wa umma,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, amewaonya watumishi hao kutotumia lugha za kejeli, matumisi, ubaguzi na watumie lugha za kupembejea.
‘’Mjue kuwa mnaiwakilisha serikali kuu, mkitumia lugha chafu mnaiwakilisha vibaya, lakini lugha laini na nyororo ndio zitawaridhisha wateja hata kama wamekosa huduma husika,’’alifafanua.
Mapema Afisa kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar ‘ZSSF’ tawi la Pemba Said Bakar, alisema yapo mafao kadhaa ikiwemo ya kuumia kazini, ulemavu na wanachama waliojifungua kwa kufuata uzazi wa mpango.
Alieleza kuwa, ni wakati sasa kuzifahamu sheria za utumishi na kujua namna ya kudai mafao ya kuumia kazini ikitokezea, jambao ambalo watumishi waliowengi hilo hawalifahamu.
Kwa upande wake Wakili wa kujitegemea Suleiman Omar Suleiman, aliwataka watumishi wa umma kuzisoma kanuni za utumishi wa umma na sheria zake, ili wajuwe haki na wajibu wao.
‘’Ni vigumu kudai haki zenu hasa zilizojificha, kama mtakuwa wazito wa kuzisoma sheria na kanuni zinazowaongoza, katika kipindi chote cha utumishi wa umma,’’alifafanua.
Mapema washiriki hao walisema mafunzo hayo ni mazuri, ingawa yanahitaji uendelevu kila baada ya muda, ili kuhakikisha wanazielewa.
Mwisho
Comments
Post a Comment