NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
KWA zaidi ya miaka 15 sasa wadau wa habari wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka sheria mpya na bora ya habari Zanzibar.
Wadau mfano Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, Baraza la Habari Tanzania (MCT), na hata ZAMECO wamekuwa wakiungana na waandishi wa habari kuhakikisha sheria moja ya habari inapatikana.
Afisa Program wa uchechemuzi wa sheria za habari Zanzibar kutoka TAMWA-Zanzibar Zaina Mzee, anasema moja ya sababu ya kutaka sheria mpya ya habari, ni kuona zile mbili zilizopo zinafutwa.
‘’Ipo sheria ya Tume ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, pamoja na marekebisho yake, pamoja na ile ya sheria nambari 5 ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988, ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 1997.
Anasema sheria hizo, zimekuwa na vifungu ambavyo sio rafiki kwa kuimarisha uhuru wa habari, pamoja na uhuru wa kujieleza katika jamii.
Anaeleza kuwa, pamoja na ukongwe wake sheria hizo mbili kuu, zinazosimamia vyombo vya habari, zimekuwa zikiwabana waandishi katika kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuuhabarisha umma.
‘’Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwenye kifungu cha 18(2) kimeweka wazi suala la kupata, kusambaza habari habari tena bila ya kujali mipaka ya nchi,’’ anasema ilivyoeleza sehemu ya katiba.
Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali anasema kuwa, kwa wakati uliopo sasa Zanzibar na duniani kote, suala la kuwepo vifungu vinavyobana uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza havina nafasi.
‘’Kwa mfano kwenye sheria mbili hizo, vipo vifungu vilivyompa uwezo mkubwa Waziri wa kulifungia au kuzuia uchapishaji wa gazeti, akihisi kwa maoni yake, kunataka kuchapishwa habari iliyokinyume na maadili,’’ anasema.
Mwandishi Salim Said Salim, anasema huu sio wakati tena wa sheria zinazoongoza vyombo vya habari, kumpa uwezo mkubwa Mkurugenzi, au Waziri.
‘’Inashangaaza kuona katika sheria za habari, hadi leo kuna maneno kama waziri anaweza, Mkurugenzi akihisi, Polisi anaweza kupekuwa, haya yote yanaleta ukakasi kwenye kazi za vyombo vya habari,’’anasema.
Mwandishi Khadija Kombo wa ZBC Pemba, anasema ukakasi wa sheria za habari hapa Zanzibar, wakati mwingine huwarejesha nyuma waandishi, kuibua changamoto za wananchi.
‘’Inawezekana waandishi wa habari wanataka kuibua changamoto kubwa inayowahusu wananchi, lakini vipo vifungu ambavyo vinatishia utendaji wao wa kazi,’’ anasema.
Meneja wa redio Jamii Mkoani Said Omar Said, anasema uwepo wa vifungu kandamizi kwenye sheria za habari, wakati mwingine huwakosesha kujiamini waandishi katika utendaji wa kazi zao.
Mkurugenzi Uratibu wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar ofisi ya Tanzania bara Juma Khamis Juma, anasema kwenye utekelezaji na tafsiri za vifungu vya sheria, hakutakiwi kuwepo neno lenye utata.
‘’Kwa mfano neno waziri anaweza, ‘akiona inafaa,’ ‘akihisi’ na mengine yanayofanana na hayo, huwa ni hatari kuwapo kwenye maelezo ya utekelezaji wa sheria,’’ anasema.
Hata Mkufunzi Mshauri Haura Shamte wakati akiwasilisha vifungu vya sheria za habari vyenye hofu na uhuru wa waandishi alipokuwa Pemba, alisema kuwa sheria hizo sio rafiki kwa waandishi.
‘’Haiwezekani kuwa hadi leo, tuwe na sheria inayompa uwezo mkubwa mtu mmoja kwa sababu ya cheo chake, au kuwapo kwa maneno yanayokinzana na msingi wa demokrasia,’’anasema.
Wananchi Khamis Iddi Mabrouk na mwenzake Issa Haji Khamis wa Kangagani Mkoani, wanasema waandishi wasipokuwa huru, hata wananchi hawatokuwa huru, hawatakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi wa mambo yanayowahusu kwa sababu ya kukosa taarifa za ukweli na uwazi.
Hidaya Mjaka Ali wa Vitongoji mwenye ulemavu wa viungo, anasema, wanavitarajia mno vyombo vya habari, kuibua changamoto za kundi lao, ingawa kinyume chake ni kukosa haki zao.
Mwanasheria wa serikali wa kujitegemea Khalfan Amour Mohamed, anasema kwamba, sio sahihi kifungu hicho kuwepo kwa sababu, kuweka sentensikama ‘kwa maoni yake’ katika sheria, ni hatari sana kwa mustakabali wa demokrasia na haki za wananchi.
VIFUNGU VYA SHERIA ZA HABARI VINAVYOUTETEMESHA UHURU WA HABARI ZANZIBAR
Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, kwenye kifungu chake cha 13 (5) kimeutia doa uhuru wa habari Zanzibar.
Kikaeleza kuwa, ‘’mtu yeyote asiyeridhika na uamuzi wa Tume kutoa au kataka maombi, anaweza kukata rufaa kwa Waziri kwa namna ya njia itakavyoelezwa na kanuni,’’kinaeleza.
Ambapo hapa, muomba leseni, anapokataliwa na Katibu Mtendaji wa Tume, akate rufaa kwa Waziri, ambae ndie aliyemteua au kusababisha kupatikana kwa Katibu huyo.
Kifungu kingine chenye maneno yenye ukakasi kwa ukuaji wa uhuru wa habari ni cha 27 (1), ambapo waziri husika au mwingine aliyeidhinishwa, anaweza kutoa amri kumtaka mpewa leseni, atangaze jambo lolote ambalo kwa maoni ya Waziri, lina maslahi kwa umma au usalama wa taifa.
Hapa wadau wa habari wanasema, kifungu hicho kipo kishari shari, maana kimebainisha uwezo wa Waziri, kumlazimisha mpewa leseni kutangaza jambo ambalo anaona tu ni kwa maslahi ya umma au usalama wa taifa.
Aliyekuwa Mdhamini wa Baraza la Habaeri Tanzania ‘MCT’ Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema neno kwa maslahi ya umma, sheria hiyo haijalitafsiri, hivyo waziri anaweza kutumia mwanya huo, kutangaza jambo analoona yeye kuwa ni maslahi ya umma.
Hata Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema, neno usalama wa taifa, sheria hiyo kwenye vifungu vyake 30 na sehemu sita halikutajwa.
‘’Hapa mpewa leseni, amewekwa njia panda, maana Waziri akiamka vibaya anaweza kutumia mwanya huo, na kutoa tangazo ambalo halina maslahi na nchi, huku sheria ikimlinda,’’anasema.
Afisa Programu kutoka TAMWA Zanzibar Zaina Mzee, anasema kupata habari ni haki ya kikatiba, sheria zinazosimamia ni vyema zisiwe na maneno au maelezo yanayoashiria kumpa mtu mmoja uwezo, kama vile anajiamulia kufanya mambo yake binafsi.
Mwandishi wa Mwanahalisi mtandaoni Jabir Idrissa, anasema athari kubwa inayotokana na sheria hiyo kandamizi ni wawekezaji katika sekta ya habari, kukosa hamu ya kuwekeza (kwanini wanakosa hamu hiyo? Dadavua), na kundi kubwa la vijana kukosa ajira.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar ‘ZPC’ Abdalla Mfaume, anasema kazi yao kubwa ni kuzisemea sheria na vifungu kandamizi, ili waandishi wa habari wafanyekazi zao kama ilivyo, kwa makundi mengine.
Rahma Suleiman mwandishi wa Gazeti la Nipashe, anashauri kuwa waandishi na wadau wa habari, waungane kushinikiza mswada wa sheria ya Huduma za Habari unapelekwa Barazani.
WIZARA YA HABARI
Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni Tabia Maulid Mwita, anasema anaamini kuwa Muswada wa sheria mpya ya Habari Zanzibar wakati wowote utapelekwa Baraza la Wawakilishi kujadiliwa.
‘’Na hata maoni ya wadau yamo kama yalivyopendekezwa, hapa kubwa naomba niendelee kuwepo katika nafasi hii, ili nihakikishe hilo linafanyika kwa haraka,’’anasema.
MWISHO.
Comments
Post a Comment