TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 06/03/2023
DCU
Toweni Vibali vya Miradi Haraka - Dkt Mngereza
Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji ameitaka
Kamati ya Udhibiti na Usimamizi Ujenzi (DCU) kutochelewesha kutoa vibali vya
miradi ili ujenzi wa miradi hiyo utekelezwe kwa muda uliyotakiwa.
Dkt. Mngereza aliyasema
hayo jana baada ya kupokea maoni ya wajumbe katika kikao cha 74 cha kamati hiyo
kilichofanyika katika ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi “B” Mkoa wa
Mjini Magharibi Unguja, alisema maombi ya vibali vya miradi yasikae muda mrefu
yawe yamejibiwa ili ujenzi wa miradi uanzwe kutekelezwa kwa wakati.
Pia aliitaka kamati hiyo
kuanzisha utowaji wa vibali vya ujenzi kwa njia ya mfumo wa Habari, Mawasiliano
na Teknolojia (ICT) ambapo utawezesha kamati hiyo kufanya majukumu yao ipasavyo.
“Vibali vya miradi
visikae muda mrefu havijatolewa, kuwe na time frame, pia kuwe na land forum, mfikirie
kuanzisha mfumo wa ICT na mkimfanye kazi kwa mashirikiano itasaidia kupunguza
malalamiko” Alisema Dkt. Mngereza.
Aidha Dkt. Mngereza alisisitiza umuhimu wa
kuitumia ardhi vizuri. Alisema ardhi ikitumika kwa mujibu wa matumizi
yake ndio maendeleo ya kiuchumi Zanzibar yatafikiwa kwani mipango bora katika
sekta ya ardhi ni kwaajili ya huduma za makaazi na kiuchumi ndio adhma ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Sambamba na hayo Katibu
Mkuu huyo alisema wizara yake itajenga
nyumba za Maendeleo sehemu mbali mbali ambayo wameyaainisha ila hakusema eneo
lipi litakuwa la kwanza kujengwa, bali
alieleza muda sio mrefu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi itasaini
mkataba wa ujezi wa nyumba za mkopo wa
bei nafuu.
Naye Mkurugenzi Idara ya
Ardhi kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar Ndg. Mtambua Hamziji Haji aliunga
mkono hatua ya kuanzishwa Jukwaa la Ardhi (Land Forum) kwani litaweza kusaidia watendaji wa sekta ya hiyo kuzungumza kwa kina
na kila mmoja atazungumza kinachomhusu katika majukumu yake.
“Bora kuwe na Land forum
kwasababu DCU wao wanalenga kukusanya mapato na kusahau matumizi bora ya ardhi
wakati ardhi ikitumika vizuri mapato yatapatikana kwa mujibu wa matumizi yake,
sisi Kamisheni ya Ardhi tunasimamia matumizi bora ya Ardhi” Alisema Haji.
Kwa upande wao wajumbe
wa Kamati ya Udhibiti na Usimamizi
Ujenzi (DCU) wamelalamikia ukosefu wa fedha katika kutekeleza majukumu yao
kwani wanakusanya fedha kutokana na utowaji wa vibali vya ujenzi na kuingiza
katika mfuko mkuu wa Serikali lakini fedha hazirudi (return) hali ambayo
inapelekea kutokutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kikao hicho cha Kamati ya
Udhibiti na Usimamizi Ujenzi (DCU) kimeandaliwa na Mkurugenzi Mipango Miji Muchi Juma Ameir
ambae ndie mwenyekiti wa kamati hiyo.
Mwisho
Comments
Post a Comment