WADAU WATAKA SHERIA ZINAZOGUSA TASNIA YA HABARI KUFANYIWA MAREKEBISHO, WASEMA ZIMEEGEMEA SERIKALINI ZAIDI
NA MWANDISHI MAALUM, ZANZIBAR
KILA raia katika nchi hii anastahili kupata haki zake
za msingi za kila siku awe mtu mwenye ulemavu au asiye na ulemavu, Mwanamke na
mwanamme, watoto, wazee na vijana.
Hivyo basi panapozungumzwa haki ni kwamba makundi yote
yana haki katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa mfano katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na ile ya Zanzibar zimezungumzia waziwazi haki za msingi kwa raia wote
bila ya ubaguzi.
Hivi karibuni Wanaharakati na wadau wa masuala ya habari
walipitia baadhi ya sheria zinazohusiana na habari ikiwa ni pamoja na kuangalia,
kujadili, kushauri na kupendekeza utendaji mzuri wa usimamizi wa mchakato mzima
na mwenendo wa sheria zinazogusa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla.
SHERIA
ZINAZOGUSA TASNIA YA HABARI
Miongoni
mwa sheria hizo ni kuangalia Mianya ya kisheria katika Sheria ya Usajili wa
Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa
marekebisho na Sheria No.8 ya 1997 sambamba na Sheria ya Tume ya Utangazaji ya
Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka
2010.
Kama
inavyoeleweka kuwa Haki ya Uhuru wa kujieleza Ibara
ya 18 ya katiba ya Zanzibar 18(1) imezungumza Bila ya kuathiri sheria
zinazohusika za nchi, kila mtu anayo haki ya uhuru wa maoni na kutafuta,
kupokea, kutoa au kusambaza habari na mawazo yake kupitia chombo chochote cha
habari bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana haki ya mawasiliano yake
kutoingiliwa.
Hivyo wadau
hao walisema neno “bila kuathiri sheria za nchi” irekebishwe kwa sababu
inaondosha uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari.
Akitoa
maoni yake mwandishi mkongwe na mkufunzi wa mambo ya habari hapa Zanzibar Salim
Said Salim, alisema kuwa kifungu hichi kinaonesha ni namna gani jinsi sentensi
hii inavyokiuka uhuru wa kujieleza kuhusiana na sheria nyingine za nchi.
“Ipo haja
ya kuangaliwa upya kifungu hichi kwani kinanyima haki za raia kujieleza na
kutoa maoni yao”, alisema.
Kuhusana na
Uteuzi wa Msajili Kifungu cha 3 – Waziri,
kwa taarifa katika Gazeti la Serikali, atamteua Msajili wa Vitabu na Magazeti
kutekeleza majukumu na kutekeleza mamlaka aliyopewa Msajili na Sheria hii na
kanuni zozote zitakazotungwa chini yake, na anaweza kuteua Naibu Msajili ambaye
atapatikana kwa maelekezo ya Msajili.
Kwa
mukhtadha huu Sheria inampa Waziri mamlaka ya kuteua Msajili wa Vitabu na
Magazeti. Lakini iko kimya juu ya sifa na uzoefu.
Hivyo Said
Salim alisema Msajili asihusishwe katika uteuzi wa naibu msajili na kusema kuwa
ni vyema kwa nafasi ya Msajili itangazwe na achaguliwe kwa mujibu wa sifa.
Mfano awe mwanasheria au mtu mwenye taaluma ya habari na mawasiliano ya umma.
Sambamba na
hilo, lakini wadau kwa pamoja walisema ni vyema sifa za msajili zinapaswa
kuainishwa katika sheria.
“Kazi ya
uteuzi wa Naibu Msajili pia ifanywe kwa kuzingatia weledi (sifa zake zielezwe
kwenye kanuni) Iwe ni nafasi itakayojazwa kwa mtu kuomba na kufanyiwa usaili”,
alisema.
Sambamba na
hayo lakini kifungu cha 27 (2) Hakimu yeyote anaweza kutoa hati kumuidhinisha
afisa polisi yeyote wa cheo cha Inspekta, kwa msaada au bila msaada kuingia na
kupekua mahali popote pale ambapo inashukiwa kuwa kuna gazeti linachapishwa
kinyume na Sheria hii linafanya kosa
chini ya Sheria hii au kanuni zozote zilizotungwa ama limefanya,
linafanya au linakaribia kufanya kosa, hivyo anaweza kukamata gazeti lolote
linalopatikana humo ama kwa kushuku kuwa
kuna gazeti lilichapishwa au linachapishwa pamoja na ushahidi mwingine wowote
wa kutenda kosa chini ya Sheria hii au kanuni zozote zilizopo/zitakazopatikana.
“Kifungu
hiki hakipo sawa na ni cha ukandamizaji wa uhuru wa habari. Hili ni suala
ambalo lalamiko linapaswa lipelekwe katika Bodi ya Ushauri (huduma za habari)
litolewe uamuzi, ikishindikana lipelekwe mahakamani na hapo ndipo mahakama itoe
hati ya upekuzi. Polisi wa ngazi yoyote
asichukue jukumu la kupekua na kukamata kabla ya lalamiko kuthibitishwa”,
alisema Jabir Yunus.
Alisema
kuwa Katika zama hizi za utandawazi, kifungu hiki hakistahili kuwapo kwa kuwa
hakina maslahi na uhuru wa vyombo vya habari.
Aidha wadau
hao walitilia mashaka kifungu cha 30 (i) ambacho kinasema kuwa Endapo Waziri
anaona kuwa ni kwa manufaa ya umma au kwa maslahi ya amani na utulivu, anaweza
kuamuru kufungiwa kwa gazeti... na gazeti hilo litakoma kuchapishwa kuanzia
tarehe iliyotajwa.
“Waziri
amepewa mamlaka makubwa ya kuamua kufungia magazeti. Mamlaka haya yalipaswa kupewa Bodi ya Huduma za Habari baada ya
Waziri kuitaarifu bodi kuhusu uamuzi wake wa kulisimamisha/kulifungia gazeti,
hivyo walisema kifungu hiki hakina maslahi na uhuru wa habari.
Aidha Makosa
ya uchochezi na kashfa yaliyopo Kifungu
cha 48 - kinaeleza makosa ikiwa ni pamoja na uchochezi na kashfa kwa mtu yeyote
ambaye anachapisha, kuchapisha, kuuza, kusambaza au kutoa chapisho lolote la
uchochezi na baada ya kukutwa na hatia mtu huyo faini au kifungo au vyote
viwili faini na kifungo vitatolewa na uchapishaji huo utatolewa. itakabidhiwa
kwa serikali.
Kifungu
hiki kinapunguza sio tu uhuru wa vyombo vya habari lakini pia kinahatarisha
uhuru wa kujieleza kwa jumla. Inapendelea zaidi upande wa maslahi ya Serikali
na kuzalisha maslahi ya kisiasa.
Hivyo
waliomba Maudhui ya kashfa ya vyombo vya habari yadhibitiwe kwa njia ya kiraia
badala ya jinai.
Masharti ya
Kashfa yametangazwa na Mahakama ya Afrika Mashariki kwa vile ni miongoni mwa
masharti yanayokiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuhusiana
na Upatikanaji wa taarifa hakuna kifungu cha Sheria haijatoa sehemu ya ufikiaji
wa habari ambayo ni muhimu vile vile.
“Tunapendekeza
kiwepo kifungu maalum kitakachozungumzia upatikanaji wa habari, walisema wadau
hao wa habari.
TAMWA ZANZIBAR
Mapema Dk
Mzuri Ali Issa, akitoa maoni yake katika moja ya mkutano wa majadiliano ya sheria
mpya ya habari uliofanyika alisema ingawa uhuru wa habari upo lakini unatolewa
kwa njia moja na kunyang’anywa kwa njia nyengine.
“Kweli
uhuru wa habari upo, lakini upande mwengine haupatikani hivyo sheria mpya ni
lazima iweke mazingira mazuri kwa maslahi ya pande zote mbili ya serikali na
wanahabari”, alisema.
Kwa upande
wa sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 kama
ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 wa Muundo wa Tume Kifungu cha 6(1) Tume ya Utangazaji ni lazima
ioneshe vyombo vya habari na mambo yote ya kijinsia.
“Ziko picha
zinaoneshwa kwenye televisheni zinawadhalilisha wanawake, baadhi ya mambo
hayonekani hivyo kama tume iangalie hilo na kuwachukulia hatua za kisheria
wahusika”, alisema.
“Waziri
amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe zaidi ya wanne wa Tume; hakuna pahali
palipopendekezwa uwakilishi wa wadau wala jinsia Ni vizuri kama kabla Waziri
hajateua wajumbe wa Tume apate mapendekezo ya wadau. Kadhalika sifa za wajumbe hawa ziainishwe
kwenye Kanuni”, alisema Dk. Mzuri ambae ni Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar alisema
Suala la jinsia liangaliwe kwa umuhimu wake.
Pia Dk. Mzuri aligusia kuhusiana na Tume ya uchaguzi, alisema
haijawahi tume hiyo kuongozwa na mwanamke, na ni makamu amewahi kutokea kwa
nafasi hiyo na kati ya makamishna saba nafasi huwa ni moja tu kwa mwanamke
katika vipindi vyote vya tume hiyo.
Sambamba na hilo, lakini alisema kuwa kiujumla wake tume hiyo
imekuwa na watendaji wengi wanaume kuliko wanawake jambo ambalo mambo mengi
yanayowahusu wanawake hutatuliwa na wanaume hasa katika mchakato mzima wa
uchaguzi.
“Wanawake, vijana, watu wenye ulemavu wanakosa nafasi katika
uandikishaji, na mambo yote ya uchaguzi jambo ambalo linnahitaji kuangaliwa kwa
umakini hasa katika uteuzi na uajiri”, aliongeza Dk. Mzuri.
“Lazima kuwe na mwongozo maalum katika kila hatua ya
uchaguzi kuanzia uandikishaji, utoaji wa elimu ya uraia, uteuzi wa wagombea,
usimamizi wa uchaguzi, upigaji kura, utoaji wa matokeo na hali ya usalama na
kwamba suala la usawa wa kijinsia na ujumuishi liongoze mchakato wote wa
uchaguzi kabla, wakati na baada”, aliongeza Dk. Mzuri.
Wadau
walisema Tume imepewa mamlaka makubwa ya kuelekeza juu ya aina ya maudhui
ambayo vyombo vya habari vya kielektroniki vinapaswa kuyashughulikia. Hivyo,
mamlaka haya iliyopewa Tume yanaweza kuathiri uhuru wa vyombo vya habari.
Kazi ya
Tume katika sehemu hii inapaswa kuwa ni kushauri tu kuhusu ubora wa maudhui ya
kurushwa hewani badala ya kuelekeza.
BARAZA LA HABARI TANZANIA (MCT)
Nae Shifaa Said Hassan, Afisa mdhamini wa Baraza la
Habari Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar, alisema sheria ya Tume ya uchaguzi
Zanzibar (ZEC) alisema ina mapungufu sambamba na kupendekeza baadhi ya mambo
kufanyiwa kazi na ZEC kwa lengo la kuleta uwiano wa kijinsia.
“Kwa mfano wanahabari ndio wanaoaminiwa kwenye jamii,
hivyo wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi bila
ya vikwazo, lakini hapo katikati hukutana na vikwazo vingi hata wakati mwengine
havimo kwenye sheria”, alisema.
Aliongeza kuwa Utafiti mdogo wa kupitia Sera ya Jinsia
na Ujumiushi (Gender and Social Inclusion Policy) ya (ZEC) ya mwaka 2015
umebaini kuweko kwa mapungufu yaliyosabisha wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu kutoshiriki ipasavyo katika mchakato wa chaguzi zilizopita, ambayo
yanapaswa kufanyiwa kazi ili sheria iwe na mashiko.
ASASI
YA VIJANA ZANZIBAR WANAZUNGUMZAJE (ZYF)
Dadi Kombo, alisema kuwa sera hiyo si rafiki sana kwa
kuwa kwenye Makamishna hakuna kijana ambae yuko katika nafasi hizo muhimu za
juu.
“Kundi la vijana ndilo kubwa na la wanawake hapa
Tanzania mbali na zile nafasi za muda za tume hasa wakati wa uchaguzi basi
makundi hayo mawili hakuna yanavyofaidika kwa kuwa nafasi nyingi zimehodhiwa na
wanaume na watu wa rika kubwa”, alisema.
Alisema kama wao wadau walibaini mapungufu mbalimbali
ikiwamo kutokuwa na mwongozo na mpango mkakati wa kuitekeleza sera ya jinsia na
ujumuishi ambayo imeundwa maalum kwa ajili ya kuangalia ujumuishi na haki za
kijinsia.
Aidha alisema, vijana na watu wenye ulemavu
zinazingatiwa katika mchakato mzima wa uchaguzi ili demokrasia siyo tu itendeke
bali ionekane kuwa inatendeka.
Dadi alisema ili kuhakikisha usawa wa kijisia na
ujumuishi unafikiwa kwa kila hatua ya uchaguzi ZEC inapaswa kukutana na wadau
wa masuala ya jinsia, vijana na watu wa makundi yote pamoja na wanahabari mara kwa
mara ili kuona hali ikoje na kuweka mpango wa utekelezaji ili pia kusaidia
katika ukusanyaji wa takwimu kama sera na sheria zilivyosema kuwa ZEC itakuwa
na mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa takwimu (Systematically Data Collection).
JUMUIYA
YA WANAWAKE WENYE ULEMAVU ZANZIBAR (JUWAUZA)
Mwenyekiti
wa JUWAUZA, Salma Saadat alisema pia katika utafiti wamebaini uwepo wa kamati
ya maadili ya ZEC, ni wa muda mfupi, huundwa wakati wa uchaguzi na uhai wake
humalizika mara tu baada ya uchaguzi kwisha.
Aidha
alisema kamati hiyo haijawekewa mwongozo wa kushughulikia malalamiko wala
haina mwongozo wa kutatua vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu na wanahabari wakati wa uchaguzi.
“Kuna wanawake au wanahabari walifanyiwa vitendo vya
udhalilishaji wakati wa uchaguzi lakini hawajui waende wapi kupeleka kesi zao,
kwa sababu kamati haina mwongozo wa kutatua kesi za mtu mmoja mmoja.
Hivyo alipendekeza sera na sheria ziweke miongozo na
mpango kazi ili ikidhi haja kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
kushiriki ipasavyo katika mchakato mzima wa uchaguzi kama wapiga kura,
wagombea, wafuatiliaji ilani na sera za vyama na hata kuhakikisha kuwa usalama
wao unalindwa vyema.
Mapema Afisa
mwandamizi wa JUWAUZA, Haura Shamte, alisema kuwa sera ya Tume ya uchaguzi ni
nzuri sana nay a kupigiwa mfano si kwa Afrika hata duniani kwa ujumla.
Alisema
nchi kadhaa zimekopia namna ya uzuri wa sera ya Tume ya uchaguzi Zanzibar,
lakini utekelezaji wake bado ni mdogo ukilinganisha na uzuri wake.
“Sera yetu
ya uchaguzi Zanzibar ni nzuri, lakini haitekelezwi hivyo tutapeleka mapendekezo
yetu ikiwa ni pamoja na kutaka makamishna wa tume kuongezeka idadi ya
wanawake”, alisema.
Aidha
alisema kuwa wanakusudia kuishawishi tume kungalia nafasi mbalimbali kama za
rasilimali watu juu ya kuwashirikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
hasa ikizingatiwa kuwa ni taasisi muhimu inayowagusa watu wengi.
MTANDAO
WA JINSIA ZANZIBAR (ZGC)
Asha Aboud Mzee ambae ni Mwenyekiti wa Mtandao wa
jinsia Zanzibar (ZGC) alisema wakati umefika sasa tume kuitathmini sheria ya
habari, Tume ya utangazaji nay a Baraza la wawakilishi namna ya ufanyaji kazi
wake.
Alisema yapo mambo mengi yanayohitaji kuhimizwa
utekelezwaji wake jambo ambalo litaonesha namna ya ushiriki wa makundi yote
katika tume ya uchaguzi.
“Wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wanahabari
wanaotupa taarifa wanakosa nafasi katika mambo yengi na yanapokuwa hayo ni ya
muda mfupi tu hivyo tunaomba sera na sheria yake penye mapungufu itekelezwe kwa
udhati kabisa na kuwekwa takwimu sahihi za ushiriki wa makundi hayo”, alisema.
Aidha Wadau wamependekeza Sera ya Jinsia na Ujumishi
ya ZEC ipitiwe tena pamoja na kuipangia mpango kazi ili iweze kutekelezeka,
jambo ambalo litaweka fursa sawa kwa makundi hayo.
KUFANYIWA
MAREKEBISHO YA KATIBA
Vile vile katika mapendekezo wadau wameomba katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 ifanyiwe marekebisho ili wanawake waweze kuteuliwa
kwenye nafasi ya Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa sababu katiba
iliyopo sasa haimlazimishi Rais wa Zanzibar kuzingatia usawa wa jinsia wakati
wa kuteua Makamishna wa Tume hiyo.
“Tunafahamu kuwa mamlaka ya uteuzi wa makamishna siyo
wa ZEC kwa kuwa imeainishwa katika Katiba ya nchi kwamba mwenyekiti na wajumbe
wengine wawili watateuliwa na rais, ambapo kati ya hao lazima mmoja awe jaji na
wajumbe wengine wanne watatoka katika vyama vya siasa.
“Ili kuhakikisha kwamba ZEC inasimamia vyema Sera yake
ya Jinsia na Ujumuishi ilisema kwamba mara kwa mara itakua inapendekeza kufanya
marekebisho ya katiba ili masuala ya jinsia na ujumuishi yaingie katika katiba
na kuifanya sera hii itekelezeke, hivyo tunashauri hatua hiyo ifanywe mapema
iwezekanavyo kabla ya uchaguzi mkuu mwingine kwa sababu kumalizika kwa uchaguzi
ni mwanzo wa uchaguzi mwingine,” alisisitiza Bi Asha Aboud.
SHERIA NA MIKATABA MBALIMBALI YA KIMATAIFA
Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar bado haijatekeleza vyema matakwa ya katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1982 juu ya haki na fursa sawa kwa baadhi ya mmabo hasa nafasi za
wanawake katika serikali na vyombo vya maamuzi.
Hayo yalikuja baada ya wanawake wengi
kunyimwa fursa ya kupata nafasi ya kugombea majimboni katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2020.
Hata hivyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akiwachagua wanawake kama
alivyoahidi katika teuzi zake mbalimbali za nyadhifa za juu serikalini.
Kwa mfano Ibara ya 8 kifungu cha 111 (b)
kinasema ni lazima kukuza katika ngazi zote za mfumo wa elimu, ikijumuisha
watoto wote wakiwa na umri mdogo, ikiheshimu haki za watu wenye ulemavu.
Pia ibara hiyohiyo kifungu cha 4 kinasema ili
kuhakikisha haki hii inapatikana nchi zilizoridhia mkataba zitachukua hatua
zinazofaa kuajiri watu maalumu, wakiwemo watu wenye ulemavu wenye utaalamu na
mkundi mengine ya pembezoni.
Aidha kifungu cha 5 kinaeleza nchi
zilizoridhia mkataba zitahakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kupata
haki yao ya kiraia ikiwemo hilo la kuchagua na kuchaguliwa bila ya ubaguzi kwa
misingi sawa na wengine, ili kufikia hatua hii nchi zilizoridhia mkataba zitahakikisha
kwamba mahitaji ya watu wenye ulemavu yanashughulikiwa.
Kimsingi mengi ya hayo yanahitaji kufanyiwa
kazi kwa weledi kabisa ili kuona makundi yote yanajumuishwa sambamba na
kuwawekea mazingira mazuri wanahabari ambao nao hawataathiri mitazamo ya
serikali kwa njia moja ama nyengine kwani lengo ni kuwa pande zote mbili
zifanye kazi kwa maslahi ya mapana ya nchi na wananchi wake.
Hivyo, ili kuleta mabadiliko, Serikali
inahitaji kuchukua juhudi za makusudi kuzifanyia kazi sheria kinzani
zinazohusiana na mambo ya habari kama sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar,
Sheria ya habari ya Zanzibar na sheria ya Baraza la wawakilishi ya Zanzibar
ambazo zote zina haki za msingi na kikatiba.
MWISHO
Comments
Post a Comment