Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi ameridhia kukutana na wanafunzi wenyeulemavu waliofaulu mitihani yao ya taifa ya kidato cha nne na sita angalau kwa kupata ufaulu wa daraja la pili badala ya kuonana na wanafunzi wote wanaopata daraja la kwanza kila mwaka.
Dk Mwinyi ameridhia ushauri huo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya muandishi mmoja wa gazeri la Nipashe kumshauri Dk Mwinyi kukutana na wanafunzi hao ili kuwafariji kama anavyowafaraji wanafunzi wingine.
“Ni kweli kila mwaka nawaita wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza kwa ajili ya kuwapongeza na kuwapa zawadi lakini kwa bahati mbaya huwa hakuna wenyeulemavu lakini kama wapo waliopata angalau daraja la pili hii itakuwa ni nafasi yao maalum nitakutana nao”anasema.
Kauli hiyo ya Dk Mwinyi imeungwa mkono na wanafunzi Abdulazizi Ali Khamis mwenye ulemavu wa Uziwi ambae amepata daraja la pili la ufaulu katika mitihani yake ya kidato cha nne mwaka huu.
Mwanafunzi huo anasema kwa mwanafunzi mwenyeulemavu hasa kiziwi kupata daraja la pili ni hatua ya kupongezwa kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo katika kupata elimu.
“Bado kuna uhaba mkubwa wa walimu wanaojua lugha ya alama na mwanafunzi kiziwi lugha ya alama ni njia moja wapo itakayomuwezesha kufanya vizuri katika mitihani”anasema.
Aidha anaiomba serikali kuongeza idadi ya walimu wa lugha ya alama Skuli ili wanafunzi viziwi kuwa na mawasiliano mazuri hasa mwalimu anapofundisha darasani.
“Bila ya kuwa na mwalimu wa lugha ya alama sisi viziwi tunakosa mawasiliano na kutofahamu kile ambapo amekifundisha mwalimu darasani”anasema.
Abdul -Azizi ni miongoni mwa wanafunzi 103 wa Shule ya Sekondari ya Dk John Joseph Magufuli visiwani Zanzibar, amefanikiwa kupata alama hiyo katika matokeo ya mitihani ya Kidato cha nne yaliotangazwa hivi Karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Licha ya ulemavu alionao Abdul-Azizi amewapita wanafunzi wezake wasio na ulemavu na ni mwanafunzi pekee kwa Zanzibar mwenye ulemavu wa uziwi aliepata ufaulu huo wa masomo ya sayansi.
Shule aliyosoma imetoa wanafunzi 9 waliopata daraja la pili la ufaulu akiwemo yeye, wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza ni mmoja, 28 daraja la tatu, 59 daraja la nne na sita daraja sifuri.
Anasema siri ya mafaniko yake ni juhudi zake za kusoma kwa bidii, juhudi za walimu wake, wazazi wake na wakalimani ambao walikuwa wakijitolea pamoja na ushirikiano kutoka kwa wanafunzi wezake.
MWISHO
Comments
Post a Comment