NA HAJI
NASSOR, PEMBA@@@@
WIZARA ya
Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya ya Chake chake, imewataka wanafunzi kuwaripoti
mara moja, waalimu watakaoonesha dalili za kuchupa mipaka yao ya ualimu, na
kuelekea katika vitendo vya udhalilishaji dhidi yao.
Kaimu Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali wilayani humo, Khamis
Juma Yahya, alitoa agizo hilo leo Machi 8, 2023 wakati akizungumza na wanafunzi wa skuli ya
sekondari ya Dk. Omar Ali Juma, kwenye kampeni maalum, ya kuongeza uwelewa, kwa wanafunzi wa
skuli, madrassa, vyuo vikuu na klabu za sanaa, iliyoandaliwa na TAMWA-Zanzibar.
Alisema
waalimu nao ni binaadamu, kama walivyowengine, wanaweza kujisahau na kuanza
kuvunja maadili yao, hivyo ikijitokeza hayo, wanafunzi wasisite kutoa taarifa
za haraka.
Alieleza
kuwa, udhalilishaji hauna kabila, mtu maalum, umri, cheo wala wakati, hivyo
wanafunzi hawanabudi kuwa makini na waalimu, ambao watawataka kimapenzi.
‘’Niwakumbushe
jambo wanafunzi wangu, hata waalimu kwa vile ni binaadamu wanaweza kutaka
kuvunja maadili, sasa mkihisi kuna viashiria hivyo, toweni ripoti japo kwa
wazazi,’’alieleza.
Hata
hivyo, amewakuwambusha kuwa, kwa sasa kazi iliyoko mbele yao ni kusoma kwa bidii,
ili wajijengee misingi imara ya maisha yao ya leo na baadae.
Nae Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, aliwaonya wanafunzi hao,
kutokubali kuchezewa wala kuchezeana sehemu zao za siri.
Aliweleza kuwa, sehemu hizo ni mali ya mwanafunzi mwenyewe, na
kusiwe na mtu mwengine yeyote, atakaepata ruhusa ya kumchezea.
‘’Jitambue, jielewe, jiheshimu na ujue kuwa, sehemu zako zote
za siri ni mali yako, na jitahidi mno kuhakikisha, hakuna mwengine
anaezichezea,’’alifafanua.
Akizungumza miongoni mwa dalili za mtu aliyedhalilishwa ni
pamoja na kutopenda kujichanga na wenzake, kukosa uchangamfu, kukosa hamu ya
kusoma pamoja na kupata msongo wa mawazo.
Kuhusu kampeni hiyo, alisema lengo ni kuwafikia wanafunzi wa
skuli, walioko vyuo vikuu, madrassa na vikundi vya sanaa, ambapo mwisho,
hutakiwa kuvibua na kuviripoti vitendo vya udhalilishaji.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu skuli ya sekondari ya Dk. Omar, Said
Ali Makame, alisema elimu kama hiyo, huwapa uwelewa wanafunzi na waalimu kwa
ujumla.
‘’Niwaombe TAMWA, wasisite kuja mara kwa mara, maana sisi
waalimu tukisema na wageni kama hivi wakisema, inasaidia elimu hii, kufika
kuwafikia,’’alieleza.
Mapema Msaidizi wa sheria, Said Rashid Hassan, alisema kwa
vile dini zote zinapinga ukatili na udhalilishaji, ni wajibu wa jamii kulikataa
kwa vitendo jambo hilo.
Alifafanua kuwa, msingi imara wa kila mmoja hapa dunia na siku
ya malipo, ni kupata elimu na kuitumia kwa vitendo, hivyo ikiwa wanafunzi
watapuuza masomo yao, watakuwa wamejikosesha haki yao.
‘’Wazazi wanawajengea wamazingira imara, ikiwemo ya huduma za
kila siku, mavazi, chakula ili muhakikishe mnapata elimu, sasa sio wakati wa
kujihusisha na mapenzi,’’alieleza.
Wakili wa watoto wanaokinzana na sheria, kutoka Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba Siti Habib Mohamed, alisema
sheria ya Mtoto nambari 6 ya mwaka 2011 ya Zanzibar, bado haijaweka adhabu kwa
mtoto, anayefanya kosa la jinai.
‘’Kwa mfano mtoto ndiye anayefanya kosa, na anapelekwa
mahakamani, lakini mahakama inapomtia hatiani kama ni fidia au faini, anayelipa
ni mzazi,’’alifafanua.
Hata hivyo alieleza kuwa, ikiwa mzazi amekosa uwezo huo, mtoto
huyo hutakiwa afikishwe kwenye nyumba ya kurekebisha tabia, ambazo hadi sasa
serikali haijazijenga.
Katika hatua nyingine, amewaonya wanafunzi wa kike kuendelea
kushughulikia masomo yao, na kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya ngono.
Baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo, waliouliza maswali na kutoa
maichango yao, walipendekeza kwa sasa wanawake watakaochangia wenyewe kudhalilishwa,
nao waapate adhabu mahakamani.
Aidha wanafunzi hao, walitaka kujua, ikitokezea mtoto wa kike
amemfuata mwanamme masafa marefu, adhabu yake ikoje kwa mujibu wa sheria.
TAMWA-Zanzibar
kwa sasa inaendelea na kampeni ya kusaidia wadau katika mapamabano ya
udhalilishaji wa wanawake na watoto, kupitia skuli, madrassa, vyuo vikuu na
vikundi vya sanaa na kisha kuchukua hatua, kupitia mradi tumia jukwaa la habari
kumaliza udhalilishaji.
Mwisho
Comments
Post a Comment