NA MARYAM SALUM, PEMBA
MWENYEKITI wa UWT Taifa Mary Pius Chatanda amewataka
wanawake wenzake kuacha tabia ya kuwanyanyasa
na kuwatelekeza watoto kwani hilo sio jambo la busara kwa jamii na hata
mbele ya Mungu.
Wito huo ulitolewa Machi 8, 2023 na Mwenyekiti huyo katika Kiwanja
chakufurahishia watoto kilichopo Tibirinzi Chake Chake kwenye wiki ya siku ya
mwanamke Duniani ambapo huadhimishwa kila ifikapo machi 8 ya mwaka.
Alisema kuwa suala la malezi kwa watoto sio la mzazi mmoja ni jukumu la kila
mmoja ndani ya jamii ili kuondosha changamoto mbali mbali zinazoweza
kujitokeza.
Alieleza kuwa sio jambo la busara kwa mzazi kutupa mtoto
ama kutelekeza mtoto kwa sababu tu yakukosa huduma ama mahitaji kutoka kwa
mwenza wake.
“Tusitupe watoto kwani hatujui hapo mbeleni mtoto huyo
unaemtupa atakuja kuwa nani katika jamii, hivyo tulee watoto wetu kwa kila hali
ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili wa Kijinsia ambao umeshamiri ndani ya
jamii zetu,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alifahamisha kuwa siku ya wanawake Duniani yalianza
kutimiza miaka 112 tangu kuasisiwa
kwake, ambapo kwa Tanzania ilianza mwaka 1911, kufuatia maandamano ya wanawake
wafanyakazi wa sekta viwandani nchini Marekani ambapo waliandamana na kupinga
mazingira duni ya kazi kama vile ukosefu wa huduma za kijamiina vitendo vya
unyanyasaji.
Alisema kuwa suala la Ukatili wa Kijinsia ni suala la
kupambana nalo kwa kushirikiana pamoja ili kuhakikisha halipati nafasi.
“Wapo akinamama wengi hupigwa na waume zao, na pia wapo
watoto wadogo hutelekezwa na wazazi wao ama familia zao kutokana na sababu
mbali mbali ambazo hazina msingi,” alieleza mwenyekiti huyo
Alifahamisha kuwa kufuatia hali hiyo mnamo mwaka 1977
Umoja wa mataifa ulithibitisha azimio lililozitaka nchi wanachama kuadhimisha
siku ya wanawake ifikapo machi 8 ya kila mwaka nakuenzi mchango wa wa wanawake
katika ujenzi wa Taifa husika.
“Hapa Tanzania siku ya mwanamke Duniani ilianza
kudhimishwa mwaka 1997, hivyo tunaendelea kudhimisha kila mwaka katika Mikoa na
kitaifa ambapo sherehe hizi huadhimishwa kila baada ya miaka mitano,
alifahamisha.
Alisema kuwa
sherehe hizi ni tathmini niutekelezaji
wa sera mpango wa mikakati na miongozo mbali mbali itakayo faa iliyoandaliwa na kwa ajili
yakuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, mfano ilani ya CCM ya
mwaka 2020 – 2025 sura ya 9 imeeleza bayana kwamba kuanzishwa kwa madawati ya
jinsia na watoto katika vituo vya kulelea watoto.
“Hivyo kila mmoja wetu anaona wazi jinsi wanavyofanya kazi
katika madawati hayo, hivyo niwaombe wananchi kutoa mashirikiano katika kupiga
vita ukatili wa Kijinsia”, alieleza.
Alifahamisha kuwa kumekuwa na shida katika suala zima la
ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni jambo ambalo lipo miongoni mwa familia, wanawake
wapo wengine wanapigwa mpaka unashangaa kutokana na kipigo kama vile anapigwa
nguruwe.
“Lakini wapo wengine pia wanawanyanyasa watoto wao,
kwakuwaacha watoto na kujilea mwenyewe jambo ambalo linapelekea mtoto huyo
kushinda mitaani, barabarani, kitu kinachopelekea sura mbaya nchini,” alifahamisha Mwenyekiti Mery.
Aidha aliwataka wanawake na walezi kwa ujumla kurudi kwa Mungu
wao kwa kuswali na kuomba dua, ili kuweza kulea watoto wao kwa misingi mizuri
na yenye maadili kwa maendeleo.
“Tanzaznia tumeingiliwa na matatizo makubwa ya ubakaji, ya
ulawiti, tumeingiliwa na mataifa kutoka nje hadi wengine wameanzisha skuli kwa
masuala hayo hata Wizara ya Elimu imegundua hilo, hivyo tuswali ili tuondokane
na mambo maovu,” alisema.
Wakati akimkaribisha Mwenyekiti wa UWT Taifa katika hafla
hiyo Makamu Mwenyekiti wa UWT Zainab
Khamis Shomari(MNEC), alisema kuwa lengo la kuchaguliwa kuwa viongozi kwenye
Jumuia ni kuimarisha Jumuia, Kiuchumi Kisiasa na Kimaendeleo.
“Hivyo nafasi mliotupatia tutaiheshimu tutailinda kwa
kadri ya uwezo wetu hivyo tunaomba mashirikiano yenu ili tuweze kufikia
malengo, na kutekeleza majuku yale ambayo katiba ama kanuni ya UWT
inavyowaongoza,” alisema.
Alieleza kuwa kutokana na dhamana walizopatiwa ndani ya
Jumuia watafanya kazi bega kwa bega na viongozi wenzao pamoja na wananchama katika
kuhakikisha wanaiweka ccm madarakani pale ifikapo 2025.
“Sisi akinamama tupo wengi kwa mujibu idadi ya Sensa ya
mwaka huu na ndio wapiga kura wakubwa na wengi, hivyo ifikapo 2025 tuone kwamba
asilimia hiyo imekwenda kwa mwanamke mwenzetu katika kumchagua kuwa Rais,”
alieleza.
Hivyo aliwataka akinamama wa Jimbo la Chake Chake
kuhakikisha wanachangamkia fursa mbali mbali zinazotolewa na Serikali katika
kujikita zaidi kwenye masuala mbali mbali ya kimaendeleo kwa maslahi ya taifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii Jinsia
Wazee na Watoto Anna Athanas Paul alieleza mwaka huu wameweza kupokea jumla ya
kesi 1360 za ukatili wa Kijinsia.
“Hivyo kutokana na
idadi hii kwa mwaka huu tunahitaji mashirikiano kutoka kwa jamii ili kupinga
vitendo hivyo,” alifahamisha Naibu Waziri huyo.
Nae Katibu Mkuu wa UWT Philis M.Nyimbi(MNEC), alifahamisha
kuwa mkusanyiko wa wanawake katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ni
kuthamini mchango uliotolewa na wanawake wenzao katika kupinga ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia duniani.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Tunu Juma Kombo alisema kuwa lengo la siku ya
wanawake duniani ni kufikia kwenye malengo yakimaendeleo.
Hata hivyo aliwataka wanawake wenzake siku hiyo sikusherehekea tu
pekee, pia ipo haja kutoa mashirikiano yakuhakikisha wanapambana kupiga vita
vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, ili kufikia
malengo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment