NA TATU MAKAME, ZANZIBAR@@@@ SERIKALI imesema bandari ya Fumba itakuwa na uwezo wa kushusha na kupakia kontena 40 kwa wakati mmoja ifikapo Januari mwakani hali itakayorahisisha ushushaji wa mizigo katika bandari hiyo na kuondosha usumbufu kwa wafanyabiashara. Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar Akif Ali Khamis alisema hayo Fumba wakati akitoa maelezo ya ujenzi wa gati ya bandari hiyo kufuatia ziara iliyofanywa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yussuph Juma Mwenda aliyefika bandarini kukagua ujenzi wa bandari hiyo. Alisema ujenzi wa bandari utakapokamilika utarahisisha usafirishaji wa mizigo kwa wafanyabiashara na kuongeza mapato kupitia mamlaka ya mapato TRA hasa usafirishaji wa mizigo. Alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kushusha vyombo 750 kwa wakati mmoja kutokana na ukubwa wa bandari na kueleza kuwa bandari itarahisisha ushushaji wa mizigo kutofautisha na bandari ya Malindi ambayo inashusha kontena 10 hadi 12 kwa w...