NA KHAULAT SULEIMAN, PEMBA
WANANCHI wa shehia ya Pandani wilaya
ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi,
ili kudumisha amani na utulivu kwa kupambana na matendo maovu katika shehia
yao.
Walieleza hayo katika kikao cha
pamoja na mkaguzi wa shehia hiyo cha kujadili na kupanga mikakati ya kuzuiya
uhalifu katika shehia hiyo, kilichofanyika shehiani.
Saada Hamid Ali mkazi wa shehia hiyo
na Said Juma walieleza kwa niaba ya wanakijiji wenzake walipongeza jitihada za
Mkaguzi huyo kwa kuona wanafikia lengo la kuondosha uhalifu.
Walieleza kuwa, kijiji kinapokuwa salama,
huwapa nafasi vijana na wananchi wingine, kufanya shughuli zao mbali mbali za
maendeleo kwa ufanisi
Akifafanua kikao hicho, Mkaguzi
wa shehia hiyo kutoka Jeshi la Polisi mkoa wa kaskani Pemba Khalfan Ali Ussi,
alieleza kuwa wanazo mbinu kadhaa za kukabiliana na uhalifu.
Hata hivyo, aliwasisitiza wananchi hao,
kutoa taarifa kwa uongozi wa shehia yao, juu uingijia wa wageni wa aina yoyote,
ili kuhakikisha amani inatawala.
‘’Moja ya jukumu la wananchi, ni
kuhakikisha wanailinda mipaka yao, lakini eneo jingine ni kutoa taarifa kwa
mamlaka, kila mnapopata ujio wa wageni kijijini kwetu,’’alifafanua.
Hata hivyo aliwasisitiza wazazi na
walezi, kuendelea kufuata nyendo ya watoto wao, kwani wahanga wakubwa na
matukio ya ukatili na udhalilishaji ni wao, licha ya jitihada zinazochukuliwa.
Nae sheha wa shehia hiyo Khamis
Rashid Ali aliwasisitiza wananchi hao, kuacha muhali kwani kufanya hivyo, itasasabisha
kutofikia malengo husika katika jamii na nchi kiujumla.
"Kila mwananchi ana wajibu wa
kutumia jitihada za kutosha, ili kuondokana na kadhia ambayo ni kilio kikubwa
katika jamii na taifa kwa ujumla,"alieleza.
Mwisho
Comments
Post a Comment