ZOEZI la uchukuaji wa fomu
za kuomba ya kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na viti maalum
kupitia chama cha Mapinduzi ‘CCM ‘wilaya ya Chake chake, linaendelea vyema.
Zanzibar leo ambalo lilifika
ofisi ya CCM wilayani humo majira ya saa 2:00 asubuhi, liliwashuhudia wanaccm
wakijitokeza mfululizo kuchukua fomu hizo, kwa nafasi kadhaa zilizotangaazwa.
Mtinia wa kwanza kwa nafasi
ya uwakilishi kutoka Jimbo la Chonga Ahmed Abubakar Mohamed, alifika ofisini
hapo majira ya saa 2:40, na kufika chumba cha kwanza, kwa ajili ya usaili, kabla
ya kukutana na Katibu wa CCM na kukabidhiwa fomu.
Akizungumza na waandishi wa
habari nje ya ofisi ya CCM mjini Chake chake, mtia nia huyo alisema, ameamua
kuchukua fomu hiyo, ili kuunga nguvu za Rais wa sasa wa Zanzibar, ya kuwaletea
maendeleo wananchi.
Alisema, amekuwa akivutiwa
mno na kasi ya Dk. Mwinyi jinsi anavyowafanyia wananchi wake maendeleo, na ndio
maana miongoni mwa sababu zake za kuchukua fomu hiyo, ni hilo.
‘’Fomu hii nimekuja kuichukua
ili kumsaidia kazi Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kuwaletea maendeleo wananchi
wa Jimbo la Chonga, pindi chama kikinipendekeza na kushinda,’’alisema.
Aliitaja sababu nyingine ya
kutia nia hiyo, ni kutumia demokrasia komavu iliyomo ndani ya CCM ya kuwaruhusu
wanachama wake kugombea, nafasi waipendayo.
‘’Unajua CCM ni ndio mwalimu
wa vyama vingine kidemokrasia, na hili ndilo lililonivutia, kuona nimtumie haki
yangu ya kuomba kuchaguliwa hapo baadae,’’alifafanua.
Akizungumzia vipaumbele vyake,
pindi vikao vya chama vikirejesha jina lake na kugombea nafasi hiyo ya
uwakilishi wa Jimbo la Chonga na kushinda kwenye uchaguzi mkuu, ni pamoja na
elimu, afya na huduma za kijamii.
Kuhusu ikiwa anauzoefu kwenye
uongozi, mtia nia huyo kwa nafasi ya uwakilishi, Ahmed Abubakar Mohamed,
alisema alianzia akiwa skuli ya sekondari na kisha kua rais ngazi vya vyuo
vikuu Tanzania.
Alisema, eneo jingine ni kushika
nafasi ya utumishi wa umma kama vile PBZ na kuwa Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais kwa miaka mitano sasa.
‘’Mimi kwenye uzoefu wa
kuongoza sina shaka, nimeshakuwa mzoefu na ndio maana, kama vikao vya chama
vitarejesha jina langu na kisha kushinda, sina hofu kuongoza jimbo,’’alisema.
Hata hivyo, alisema pamoja na
kwamba hii ni mara yake ya tatu kugombea nafasi hiyo, lakini ataheshimu na
kuthamini mno uamuzi wowote wa chama juu yake, kwani kipaumbele chake ni chama,
kisha uongozi.
Nae mtia nafasi kwa nafasi ya
ubunge jimbo la Chake chake Ashura Abdalla Simai, alisema ana nia hiyo, ili kuona
anataka kwenda bungeni kuwatetea wanawake.
‘’Wanawake wamekuwa wakikosa
mtetezi kwa kina, kwa mambo yanayotuhusu, hivyo nimechukua fomu, kujaribu
bahati yangu kwa mara nyingine,’’alisema.
Kwa upande wake mtia nia
nafasi ya ubunge jimbo la Ziwani Othman Kassim Juma, alisema sababu za kuchukua
fomu hiyo, ni kutaka kulikomboa jimbo hilo.
Hata hivyo mtia nia kwa
nafasi ya ubunge jimbo la Chake chake Issa Mohamed Kassim ‘mzee wa nyungu’
alisema kwa sasa, hana cha kuwaambia wananchi, kama uamuzi wa chama haujafanyika.
‘’Mimi ni mwanaccm damu, sihofii
kutorejeshwa kwa jina langu, maana maamuzi ya chama iwe ni ya halmashauri kuu
au kamati kuu, naayamini na nayaheshimu, kwa dhati ya moyo wangu,’’alisema.
Mapema mtia nafasi kwa nafasi
ya viti maalum kwa watu wenye ulemavu, Awena Khamis Rashid, alisema kundi hilo
linamuhitaji yeye kwa ajili ya kulikomboa.
‘’Nimeona watu wenye ulemavu
hawajapata mtetezi, na ndio maana nimetumia haki yangu ya kikatiba kupitia chama
changu cha CCM, ili kuomba kuteuliwa,’’alifafanua.’
Aidha mtia nia kwa nafasi ya
ubunge jimbo la Ole Burhan Khamis Juma, alisema kilichomvuta kuchukua nafasi
hiyo, ni kutaka kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi.
Awali Katibu wa CCM wilaya ya
Chake chake, Nicholaus Samson Chibwana, alisema kwa jana waliwapokea na kuwapa
fomu watia nia 12 kwa nafasi ya ubunge 12 na wanne kwa nafasi ya uwakilishi.
Alisema, hio ni kuonesha kuwa,
CCM imepevuka kidemokrasia, kwa wanachama wake kuitumia haki yao nyingine, na
sio ile walioizea ya kuchagua pekee.
Zoezi la uchukuaji fomu kwa
nafasi za unbunge, uwakilishi na viti maalum, lilianza juzi Juni 28,
likitarajiwa kumalizika Julai 2 mwaka huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment