NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MRATIBU wa miradi kutoka Mwenvuli wa asasi za kiraia
Pemba ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, alisema wanatekeleza kwa vitendo, maono ya
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha elimu ya uraia na demomkrasia inawafikia
wananchi.
Mratibu huyo aliyasema hayo, wakati akizungumza na watendaji
wa serikali na wanaasasi za kiraia, katika kongamano la pamoja, la kujenga
ushirikiano, baina pande mbili hizo, kupitia mradi wa ‘uraia wetu’
lililofanyika Wawi Chake chake.
Alisema, mradi huo ni tokeo moja wapo la maono ya viongozi
hao, ambapo wameamua kuwakusanya watendaji wa serikali na wale wa asasi za
kiraia, ili kuibua changamoto zinazokwamisha ushirikiano wao.
Alieleza kuwa, washiriki wa kongamanio hilo, watapata nafasi
ya kuelezea changamoto zao kikanuni, sera na kisheria ili kuona zinatatuliwaje
kwa umoja wao.
‘’Sote ni mashahidi kuwa, wakati viongozi wetu wanaingia
madarakani, walihimiza mno suala la kuzifahamu sheria, kuona changamoto zake na
hata kuzifanyia marekebisho, ili kusiwe na mkwamo katika utekelezaji wa
shughuli husika,’’alieleza.
Aidha Mratibu huyo wa miradi kutoka ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar,
alieleza kuwa washiriki watachambua sera, kanuni na sheria ambazo wakati
wanapotekeleza majukumu yao, zinawakwaza.
Katika hatua nyingine alifafanua kuwa, PACSO imeandaa jukwaa la kuwakutanisha pamoja watendaji wa serikali na wanaasasi za kiraia, ili kujadili kwa pamoja changamoto za watu wenye ulemavu, vijana na wanawake.
Alieleza kuwa, maoni ambayo yatapatikana katika kongamano
hilo, watayaandika vyema na kuyasilisha kwa Jumuiya ya wanawake wanawake wenye
ulemavu Zanzibar, ambao nao watakeleza mradi kama huo, ngazi ya kitaifa.
‘’Kwenye mradi huu PASCO, inatekeleza ngazi ya kanda (zone), ingawa
wenzetu wa JUWAUZA wanatekeleza ngazi ya kitaifa na kisha maoni hayo, watayafikisha
kwa viongozi wa kitaifa,’’alieleza.
Akifungua kongamanio hilo, Msaidizi Naibu Mrajisi wa Asasi za
Kiraia Pemba, Saada Abubakar Khamis, alisema mradi huo, unaweza kuleta tija,
kwa vile unaangalia kwa upana wake, suala la demokrasia.
Alieleza kuwa, moja ya chanagamoto iliyopo ni kutoonekana kwa
uhusiano mzuri, baina ya asasi za kiraia na serikali kuu, jambo ambalo wakati mwengine
huchelewa kutekelezwa kwa miradi.
‘’Jambo hili lililofanywa na wenzetu ‘PACSO’ naamini
litazidisha ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali na asasi za
kiraia, hasa kwa vile pia litaangalia sheria na kanuni zinazokwamisha utendaji
wa asasi,’’alifafanua.
Alifafanua kuwa, demokrasia ni dhana pana na wakati mwengine
wapo wanaoona inahusu ngazi za juu pekee, bila ya kuona kuwa dhana hiyo, hutakiwa
kuonekana hata kwenye asasi za kiraia.
Wakichangia kwenye kongamano hilo, washiriki hao walisema ushirikishwaji
ni jambo jema, katika kufikia uamuzi wowote, katika nchi ama asasi za kiraia.
Afisa wa watu wenye ulemavu wilaya ya Chake chake Mwadini Ali
Juma, alisema bado watu wenye ulemavu, hawajatendewa haki sana katika ajira,
miundombinu na majengo ya umma.
Mwakilishi kutoka TAMWA, Asha Mussa Omar, alisema kikwazo
kilichopo ni kwa jamii, kutotaka kubadili mitazamo, juu ya dhana ya mwanamke na
uongozi.
‘’Wapo baadhi ya watu wanawavunja moyo wanawake, kwa
kuwaambia kuwa wakiwa viongozi, watakuwa wamevunja maadili, watapewa takala, dhana
hizi zinahitaji elimu kwa bidii,’’alieleza.
Akiwasilisha mada ya umuhimuwa ushirikiano baina ya asasi za
kiraia na serikali, mkufunzi Juma Bakar Alawi, alisema hakuna haja ya pande
mbili hizo, kunyimana taarifa.
Alieleza kuwa, asasia zote za kiraia Zanzibar, zinatekeleza miradi
ambayo ni maono ya serikali kuu, hivyo ni vyema pande moja wapo inapohitaji
taarifa, iwe rahisi kupeana.
Kongamano hilo la siku moja, kupitia mradi wa ‘uraia wangu’
limeandaliwa na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society kupitia Umoja wa
nchi za Ulaya.
Mwisho
Comments
Post a Comment