NA ASHA ABDALLA, PEMBA@@@@
WAALIMU na wanafunzi wa skuli ya msingi ya Wesha wilaya ya Chake chake Pemba, wamesahauriwa kuongeza juhudi
za kupambana na vitendo vya udhalilishaji, ili wanawake na watoto wabaki salama
kwa vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa na Mshauri nasaha kutoka kitengo cha mkono kwa mkono cha hospitali ya Chake
chake Asha Massoud, wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi hao, juu ya dhana ya
kupambana na udhalilishaji, mafunzo yaliyofanyika skulini hapo.
Alisema kuwa, kupitia mafunzo anaamini wanafunzi na
waalimu hao, wameshapata njia sahihi ya kuongeza juhudi za mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Alieleza kuwa, kila mmoja na kwa nafasi yake, anatakiwa kukemea na kutoa
elimu ya kujikinga na masuala la udhalilishaji, ili jamii na hasa kundi la
wanawake na Watoto libaki salama.
‘’Kwanza niwatake waalimu na wanafunzi wa skuli hii ya Msingi Wesha,
kuhakikisha wanaongeza makali ya kukemea na kutoa taarifa wanapoona viashiria
vya udhalilishaji kwa mmoja wao,’’alifafanua.
Akizungumzia mbinu zinazotumiwa na wadhalilishaji na hasa kwa waatoto Mshauri nasaha huyo, alisema moja wapo ni kupewa zawadi mfano wa pesa au pipi.
Alifahamisha kuwa, mwanafunzi yoyote asikubali kuitwa na mtu amsiyemjua na kukubali
kupokea pesa au kitu chochote, kwani
kufanya hivyo ni kuwakaribisha wahalifu hao.
"Kitendo cha udhalilishaji, kwa miaka
hii hakifanywi na mtu wa mbali, bali ni wale wazazi na walezi au wakati mwengine
hata majirani, lakini wote hawa wakianza ishara ni vyema mkatoa taarifa,"alisema.
Wakati huo huo, Mshauri huyo nasaha kutok kitengo cha Mkono kwa mkono
cha Hospitali ya Chake chake Asha Massoud, amewasisitiza wanafunzi hao, kuacha
kuitana majina mabaya
au kupigana, kwani vitendo hivyo ni sehemu ya udhalilishaji.
Nae Afisa Mshauri kutoka
kitengo cha mkono kwa
mkono cha hospitali ya Chake chake,Tatu Abass, alisema moja ya madhara makubwa kwa mtoto
aliyefanyiwa vitendo vya udhalilishaji ni kukosa elimu, kupoteza afya yake na kukosa
hamu ya kujiendeleza.
Hata hivyo, amewakumbusha Watoto wa kike, kujilinda na athari za mimba
za umri mdogo, kwani athari yake moja kubwa ni kupoteza uhai, kutoakana na
viungo vyake vya uzazi kutokuwa tayari kuhimili vishindo vya mimba.
"Mtu yeyote aliyefanyiwa udhalilishaji, anaweza kupata maradhi mbali mbali, mfano
ukimwi, kwani anayemfanyia huwa hujui afya yake,’’alifafanua.
Kwa upande Mshauri nasaha kutoka kitendo hichi hicho, Kurthumu Khamiss Msabaha, alisema kua kuna njia mbali mbali za kujikinga na udhalilishaji, ikiwemo
kutokutumia simu ukiwa bado ni mwanafunzi na kuzurura ovyo ovyo katika maeneo mbali mbali.
Nae Polisi kutoka dawati la jinsia la wanawake na watoto katika
kituo cha Polisi Chake chake Salama Omar, aliwataka wanafunzi, kuendelea kutoa taarifa wanapoona
wanataka kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
"Musimuamini mtu yoyote ambae humjui undani wake, kwani itapelekea kuja kukufanyiwa kitendo kibaya, ambacho hujakitarajia katika Maisha yako, nakukuvunjia
malengo yako,"
alieleza.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa skuli hiyo
Mafunda Sudi Sabur, alikishukuru kitengo hicho kwakuwapa mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyiakazi kwa wengine, ili elimu hiyo isambae.
Hata hivyo aliwawambia wanafunzi wake, wawe mabalozi kwa wenzao, ambao hawapo katika mafunzo hayo, ili kuona
kila mmoja amepata uwelewa.
Mwisho |
Comments
Post a Comment