NA HAJI NASDSOR, PEMBA@@@@
KESI ya kupatikana dawa, zinazoaminika kuwa ni za kulevya, iliyopo Mahakama kuu Zanzibar kisiwani Pemba, imeshindwa kuendelea, baada ya shahidi na wakili wa utetezi, kutochomza mahakamani hapo, kwa udhuru wa kuumwa.
Awali mtuhumiwa katika shauri hilo Ame Kheir Ali, aliwasili mahakamani hapo, akimsburi wakili wake Zahran Mohamed Yussuf, ili aendelee na hatua ya kumskiliza shahidi wa upande wa mashtaka, ingawa alielezwa na Jaji wa mahakama kuu kuwa, wakili wake anaumwa.
Jaji Ibrahim, alimueleza mtuhumiwa huyo kuwa, kwa mujibu barua iliyopokelewa mahakamani hapo ni kuwa, wakili wake huyo hayupo kisiwani Pemba kwa sasa.
‘’Mtuhumiwa leo (jana) tunakuomba radhi, maana wakili wako Zaharan Mohamed Yussuf, hayupo hapa mahakamani na kisiwani Pemba, yuko Tanzania bara kimatibabu,’’alisema Jaji.
Kisha, Jaji huyo aliupa nafasi upande wa mashtaka kusema, jambo juu ya hilo na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Seif Mohamed Khamis, alikubaliana na taarifa hiyo.
Mapema wakili huyo, aliimbia mahakama hiyo kuwa, hata kwa upande wao, wanae shahidi mmoja juu ya shauri hilo, ingawa nae hakuweza kuhudhuria mahakamani, kutokana na shida ya kiafya.
Wakili huyo alidai kuwa, kesi hiyo imefikia hatua ya kusikilizwa, na tayari kwa mujibu wa kumbu kumbu zao, wameshampokea shahidi mmoja, ingawa naye, hatoweza kusikilizwa kutokana na kuumwa,’’alidai.
Hivyo wakili huyo wa serikali, aliiomba mahakama hiyo kuu, kulighairisha shauri hilo, na kulipangia siku nyingine, kwa ajili ya kuendelea na hatua iliyofikiwa.
Jaji Ibrahim alikubaliana na ombi hilo, na kumtaka Mwendesha mashtaka kuhakikisha siku hiyo, wanamuarifu shahidi wao, ili afike mahakamani hapo.
Alipomuuliza mtuhumiwa Ame Kheir Ali, Jaji wa mahakama kuu Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim, juu ya kulighairisha shauri hilo, alidai hana pingamizi na uamuzi huo.
‘’Unasemaje mtuhumiwa Ame, maana wakili wako anaumwa na yuko Tanzania bara na shahidi mmoja wa upande wa mashtaka, nae hakuweza kufika mahkamani kwa sababu kama hiyo, je unasemaje,’’aliulizwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo Ame Kheir Ali miaka 35 wa Jiondeni Mkoani Pemba, alipatikana na dawa zinazosadikiwa kuwa ni za kulevya.
Ilidaiwa kuwa, alipatikana na kete 70, aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 1.57, Septemba 18, mwaka 2022, majira ya saa 2:00 asubuhi eneo la Makombeni wilaya ya Mkoani Pemba.
Kufanya hivyo ni kosa, kinyume na kifungu 21(1) (d) cha sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti, na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, sheria nambari 8, ya mwaka 2021.
Kesi hiyo imeghairishwa mahkamani hapo, hadi Machi 4 na 5, mwaka 2024 ambapo itasikilizwa siku mbili mfululizo, na Jaji Ibrahim, kutaka mashahid siku hiyo wafike.
Mwisho
Comments
Post a Comment