Na Salma Lusangi
NAIBU waziri Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shabaan Ali Othman amesema uongozi wa wizara yake uko tayari kukosolewa pamoja na kupokea maelekezo yaliyotolewa na kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ili kuleta ufanisi katika majukumu ya wizara hiyo.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho kilichofanyika jana katika ukumbi wa ZURA Maisara Zanzibar, baada ya kamati hiyo kumaliza ziara ya kutembelea miradi ya umeme na maji kwa Unguja na Pemba ambayo inatekelezwa na WMNM, alisema wapo tayari kukosolewa kiutendaji pamoja na kupokea ushauri ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
“Kwanza nawapongeza watendaji wote hasa nampongeza Katibu Mkuu Kilangi, kama wizara tumepokea maelekezo ya kamati,tutayatekeleza kama tulivyotumwa naomba kamati isisite kutukosoa zaidi naona kamati imetoa ushauri mzuri utatusaidia sana katika kutekeleza majuku yetu, tumeyapokea maelekezo yote” alisema Othman.
Alisema wizara yake itaongeza kasi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Maji na Nishati pamoja na kuangalia upya mikataba ya wakandarasi kwa lengo la kumaliza miradi yote kwa wakati ili kuwaondolea shida wananchi.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo Abdallah Rashid Aballah ameitaka WMNM kukamilisha miradi ya maji na umeme kwa wakati ili kutimiza ahadi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi aliyowaahidi wananchi kuwafikishia huduma ya maji na umeme mjini na vijijini.
Alisema miaka mitano sio mengi, lazima ahadi za Mhe. Rais zikamilike kabla ya kufikia muda huo kwani wananchi bado wanalalamikia ukosefu wa kupata huduma ya maji.
Alieleza kwamba kamati yake imeshatoa maelekezo kwa changamoto walizoziona katika Miradi ya Maji na umeme ikiwemo kuwashirikisha waakaazi wa eneo husika wakati wa kufanya utafiti kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi/ miradi ili kuepusha migogoro isiyonaulazima.
Aidha amepongeza ripoti na utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na WMNM kwani kamati imeona vifaa vya miradi ya umeme ambavyo vimenunuliwa na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) pamoja kuona maendeleo ya miradi ya Maji ikiwemo uchimbaji wa visima, ujenzi wa matangi na utandazaji wa mabomba ya maji kwa unguja na Pemba.
Mapema katibu Mkuu WMNM Joseph Kilangi aliwasilisha ripoti ya utekezaji wa wizara hiyo kwa kipindi cha Febuari hadi June ,2022 ikiwemo mafanikio na changamoto zilizowakabili katika utekelezaji wa miradi ikiwemo idadi ya visima vilivyofanikiwa kuchimbwa, pamoja changamoto za kiutalamu, vifaa vya miradi kuchelewa kufika kwa wakati hali ambayo ilisababisha baadhi ya miradi kusita kidogo kiutendaji.
Alisema hivi sasa vifaa vingi vya miradi vimeshawasili nchini ikiwemo mita za umeme, mabomba ya maji , kokoto , saruji nk hivyo kazi itaendelea kwa kasi zaidi kwasababu watendaji wa wizara yake wanafanya kazi kwa mashirikiano ya karibu ili kuleta ufanisi zaidi.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Maji ( ZAWA) Mhandisi Dkt Salha Mohammed Kassim alisema wanafanya kazi kwa usimamizi mkubwa bali amekabiliwa na changamoto ya ukosefu wa watalaam hivyo wakati mwengine anahitaji kuazima wahandisi na mafundi kutoka Tanzania Bara ili kuongeza kasi ya utendaji.
“Naomba Serikali kuekeza nguvu ya elimu kwa vijina katika fani ya Mechanical engineer, Civil engineer na Electrical engineer kwani wakati mwengine huwa na lazimika kuomba wataalamu kutoka Tanzania bara kwasababu nimetafuta hapa Zanzibar nimekosa” alisema Mhandisi Dkt Salha.
Mwisho
ReplyReply allForward |
Comments
Post a Comment