HABIBA ZARALI, PEMBA
WANANCHI
wa shehia ya Mfikiwa Wilaya ya Chake chake kisiwani Pemba, wameupongeza mradi
wa 'dumisha amani Zanzibar’ kwa kuwapa elimu ya utatuzi wa migogoro, uliowawezesha
kupunguza mivutano na sasa kuishi kwa amani.
Walisema kabla ya kuwafikiwa na mradi
huo, katika shehia yao kulikithiri migogoro hasa ya ardhi, kati yao na serikali
ingawa kwa sasa hali inaendelea vizuri.
Wakizungumza kwenye mkutano wa
ufupisho wa mradi huo na kuangalia changamoto za migogoro, waliyoibuwa
ulioandaliwa na tasisi ya Search for Common Ground na Foundation for civil
society shehiani humo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo walisema
chanzo cha uvunjifu wa amani ni kutotendeka kwa haki.
Mmoja kati ya wananchi hao Khamis
Ali Khamis, alisema migogoro ya ardhi, waliyokuwa nayo nyuma ilisababishwa na
kutotendewa haki na baadhi ya taasisi za serikai, baada ya kuchukuwa ardhi bila
ya kuwashirikisha wananchi.
Alisema kama haki itatendeka vyema
katika kila sekta, na idara zote suala la uvunjifu wa amani, wala kuibuka kwa migogoro
halitokuwepo.
"Migogoro itaweza kupunguwa
iwapo Serikali itawashirikisha wananchi ipasavyo na kuwatendea haki, wakati
wanapowahudumia wananchi ",alisema.
Nae Mwaache Juma Abdalla alieleza kuwa, pamoja na kupata elimu hiyo ya utatuzi wa migogoro na kuweza kuifanya kazi, katika shehia yao bado watendaji wa serikali wana jukumu la kutekeleza haki.
Alifahamisha kuwa, ili juhudi hizo
ziweze kifanikiwa ni jukumu la Serikali kupunguza tozo kwenye sekta ya ardhi,
ili kuwafanya wanyonge waweze kumiliki hati za ardhi bila ya vikwazo.
"Kila mmoja anahitaji kupata
hati ya kumiliki ardhi, lakini mizunguko na gharama wengi wetu tunashindwa
kuihimili kutokana na hali zetu za umaskini,’’alisema.
Habib Haji Saleh alieleza kuwa,
uvunjifu wa amani hujitokeza baada ya mwenye haki kukoseshwa na kupewa mtu
mwengine, bila hata ya kupewa elimu stahiki.
Alifahamisha kuwa, uvunjifu wa amani
Zanzibar, husababishwa na kuwepo kwa migogoro mengi ikiwemo ya uchaguzi, ardhi,
ndoa na udhalilishaji, hivyo ni jukumu la jamii, kutilia maanani maeelekezo
yaliyotolewa na mradi na kuweza kuishi kwa amani.
Mapema mpatanishi wa migogoro kutoka
taasisi ya foundation for civil society Maalim Mohamed Said, alisema lengo la
taasisi hiyo, ni kuifanya Zanzibar kuwa na amani endelevu.
Alisema, tayari ipo migogoro kadhaa
kiwemo ya ardhi, ndoa, mirathi na kusisitiza kuendelea kutimiza njia ya utatuzi
wa migogoro kwa amani.
‘Zanzibar kwa sasa inaendeshwa kwa
mfumo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambapo suala la amani ni jambo la
mwanzo, na huku tasisi hizi za Fcs na Search kuja na mradi huu, ni jambo la
faraja,’’alieleza.
Akiwasilisha baadhi ya changamoto
zilizoibuliwa katika mradi huo, Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar
ZLSCA TAWI LA Pemba, Safia Saleh Sultan alisema ni matarajio ya mradi huo
utakapomalizika kuona wananchi wanaendeleza, wajibu wao wa kudumisha amani,
katika maeneo yao.
Nae Mwanasheria kutoka kamisheni ya Ardhi
Pemba Asha Suleiman Said, alisema jambo linaloweza kuondosha migogoro ya ardhi
kwa jamii, ni kufuata sheria zikiwemo za ununuzi na uuzaji, kutafuta hati
miliki na kupeana elimu ili kila mmoja aweze kuwa na uwelewa.
Mradi wa dumisha amani Zanzibar
ambao ulizinduliwa mwaka 2021 unatekelezwa
kwa pamoja kati ya search for Common Ground, the foundation for Civil Society,
kwa ufadhili wa Jumuiya ya nchi za Ulaya ‘EU’ na ukitarajiwa kumalizika mwaka
huu.
Mwisho
|
Comments
Post a Comment