JAMII Kisiwani Pemba, imetakiwa kuwa na mwamko wa kujua kuwa, jukumu la utatuzi wa migogoro kwa makosa ya madai, kwa njia ya amani ni lao wenyewe kabla ya kufika katika vyombo vya sheria.
Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa taasisi ya foundation for civil society Khamis Abass katika kikao cha kubadilishana mawazo, na kuandaa mikakati itakayosaidia kuondowa changamoto zilizojitokeza katika hatuwa za awali za utekelezaji wa mradi wa 'Dumisha amani Zanzibar' kilichofanyika shehia ya Ngwachani Wilaya ya Mkoani Pemba.
Alisema katika utekelezaji wa mradi huo kumeweza kuibuliwa migogoro mingi ikiwemo ya ardhi, ndoa, siasa, na mengine ambayo inaweza kusuluhishwa kwa kukaa pamoja wanajamii wenyewe.
Alifahamisha kuwa, ukosefu wa amani unatokea baada ya jamii kutokuwa na mazungumzo ya pamoja pale baada ya kutokezea migogoro hasa yale ya madai.
"Iwapo jamii itaipa nafasi migogoro kutawala ni wazi kuwa amani itakuwa tunu na wakati huohuo shughuli za kimaendeleo ziakosekana",alisema.
Mapema akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mradi huo Mratibu Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, alisema bado kuna changamo za ushirikishwaji mdogo kwa wanawake na watu wenye ulemavu, katika ngazi za maamuzi.
Aidha aliwaasa wanawake kushiriki katika vikao vinavifanywa kupitia shehia zao, kwani kufanya hivo kitasaidia kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi.
Akitaja mikakati ya kamisheni ya ardhi itakayopunguza migogoro ya ardhi kwa jamii, mwanasheria kutoka kamishemi hiyo Asha Suleiman Said, alisema ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii katika kujua umuhimu wa hati miliki na vipi wanaweza kuipata.
Wakati huo huo aliwataka wanajamii kurithi mali zao kupitia taasisi ya wakfu na mali ya amana na kuepusha kugaiana ardhi bila utaratibu ili kuepusha migogoro hapo baadae.
"Jamii tufahamu kuwa ardhi haigawiwi na unapompa mtu ardhi kwa muda wa miaka 12 bila usumbufu kisheria huyo ndio mmiliki husika wa ardhi hiyo"alisema.
Akichangia mada Asha Hamad kutoka shehiya ya Ngwachani alisema chanzo cha migogoro mingi ya ardhi ni usumbufu kutoka kwa watendaji, katika kupima na kutoa kibali hivyo ni vyema kwa taasisi husika kujitahidi kuifikia jamii pindi anapohitaji msaada huo.
Issa Nassor Mohamed na Said Mohamed Ali wameiomba taasisi ya foundation for civil society kuendeleza juhudi za utoaji wa elimu, kuanzia ngazi za chini katika jamii ili kuepusha migogoro na kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi.
Mradi wa Dumisha amani Zanzibar umeanza mwaka 2021 na umetekelezwa kwa muda wa miezi 18 kupitia taasisi ya Search For Common Ground na Foundation For Civil Society lengo ni kuisaidia jamii katika utatuzi wa migogoro na kudai haki kisheria.
Mwisho
Comments
Post a Comment