NA HAJI NASSOR, PEMBA
WAZAZI na walezi visiwani Zanzibar, wametakiwa kutoingilia kimabavu,
faragha za watoto wao, kwani kufanya hivyo, kunaweza kuwa chanzo cha ukosefu wa
nidhamu kwao, katika maisha yao ya baadae.
Ushauri huo umetolewa na wataalamu wa malezi na
makuzi ya kisayansi ya awali ya watoto ‘SECD’ kisiwani Pemba, wakati
wakizungumza na mwandishi wa habari, juu ya dhana ya faragha kwa watoto wadogo.
Walisema, suala la faragha na umri wa mwanadamu
halina uhusiano wowote, hivyo watoto kama walivyo watu wazima, hawatakiwi
kubugudhiwa na kuingiliwa kimabavu faragha zao.
Mmoja kati ya wataalamu hao, Rashid Said Nassor,
alisema faragha hata ya mtoto mdogo, mzazi, mlezi au mtu mwengine, hatakiwi
kuiingilia, kwani kufanya hivyo ni kumvunjia haki zake.
Alieleza kuwa, mtoto ni mwanadamu kama walivyo
wengine, hivyo anaowakati hujiweka kwenye faragha yake, na kufanya mambo yake
binafsi, na mzazi au malezi hatakiwa kumyima uhuru huo.
‘’Mtumzima gani ambae anafurahia anaponyimwa haki
yake ya faragha, bila shaka hakuna, basi na hata kwa mtoto, nae anayohaki ya
faragha na haitakiwi kuingiliwa kiholela na mtu yeyote,’’alieleza.
Nae mtaalamu wa malezi hayo ya kisayansi na
makuzi ya awali ya mtoto ‘SECD’ Omar Mohamed Ali, alieleza kuwa suala la kila
mmoja kuwa na faragha yake iliyohalali, halitakiwi kuingiliwa wala kutikishwa
na mtu mwengine.
‘’Ndio maana, hata vipo vyombo vya habari
vimeshashtakiwa kwa kuingilia faragha za watu, vivyo hivyo kwa wazazi na walezi
wasiangalie umri wa watoto wao na kuingilia faragha zao,’’alishauri.
Hata hivyo, alisema katazo hilo halimzuii mzazi
kumfundisha malezi na makuzi yenye maadili mtoto wake, au kumzuia kushiriki
kwenye vikundi viovu, bali kinachokatazwa, ni kuingia faragha yake halali pasi
na sababu ya msingi,’’alieleza.
Nae Khadija Omar Haji, anasema kitaalamu watoto
huwa na muda wa kujiweka pahala peke yao, na kufanya shughuli zao binafsi za
halali, mfano kulala, kufikiria jambo au kuangalia burudani isiyoharibu maisha
yake.
‘’Wazazi na walezi hawana haki ya kuvuruga wala
kuingilia uhuru wa faragha wa watoto wao, maana ukuaji wa ubongo unahitaji
mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na heshima ya awali,’’alieleza.
Nae muuguzi wa mama na mtoto wa Hospitali ya
Abdalla Mzee Mkoani, dok. Rabia Mohamed, alisema faragha ya watoto ni sehemu ya
kibailojia inayompa nafasi, kukuza ubongo wake.
Msimamizi wa kitengo cha lishe Wilaya ya Chake
Chake, Harusi Masoud Ali, alieleza kuwa, mtoto baada ya kushiba huhitaji kupata
faragha ya kujipumzisha, ili kukipa nafasi chakula kusagika kwa urahisi.
‘’Kama alivyomtu mzima anahitaji kuthaminiwa na
kuenziwa kwa uhuru wake wa faragha, na vivyo hivyo watoto wetu wanahitaji uhuru
huo kwa upana zaidi,’’alifafanua.
Meneja
‘ECD’ tasisi ya Maendeleo ya binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mombasa
Joyce Marangu, alisema huduma za wazazi kwa mtoto wao, ni pamoja na kutii uhuru
wa watoto wao.
Mkuu wa
wilaya ya Mkoa Khatib Juma Mjaja, alisema endapo wazazi na walezi watathamini
uhuru wa faragha kwa watoto wao, watakua katika malezi na makuzi hayo, nao
kufikia kuwaheshimu wengine.
Wazazi
Khadija Haji Khamis, Wahidi Omar Kassim na Maua Othman Ziadi wa mji wa Chake
chake, walisema wamekuwa hawatambui hilo, na kuona mtoto hana haki hiyo.
Mwanasheria
dhama wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kisiwani Pemba Ali Haidar, alisema
sheria ya mtoto ya Zanzibar nambari 6 ya mwaka 2011, imetambua uhuru wa faragha
kwa watoto.
‘’Ukiangalia
katika sheria hiyo moja ya haki za mtoto ni pamoja na wazazi au walezi,
wanawajibu wa kuheshimu faragha ya watoto na kutambua utu wao na ulinzi
kamili,’’alieleza.
Wataalamu wa malezi ya kisayansi, makuzi na uchangamshi wa mtoto kwa hatua za awali ‘SECD’ wametaja njia tano ambazo familia ikizifuata, itakuwa ni chac hu ya ukuaji wa ubongo wa matoto, ikiwa ni pamoja na kumpa uhuru wa kuchangamana na wenzake.
Nae sheikh Ramadhan Mohamed wa Chake chake, alisema dini inatambua hilo, na ndio maana imewaelekeza waumini kutaja jina la muumba mara mtoto anapozaliwa.
Mchungaji wa kanisa la KKKT Chake chake Benjamen Kissanga, alisema maandiko yako wazi na kuwa yataka kila mtu kwa utu wake aheshimiwe pasi na kuangali umri.
Comments
Post a Comment