PICHA NA MTANDAO SIO HALISI YA VIZIWI
NA HAJI NASSOR, PEMBA
ULEMAVU ni upungufu wa uwezo wa viungo vya mwili, akili au hisi unaomsababishia mtu, kushindwa kumudu mazingira yake au kushindwa kushiriki kikamilifu katika kazi za kijamii.
Ndivyo ilivyoa toa tafsiri ya nini maana ya ulemavu, sheria ya watu wenye ulemavu (haki na fursa ) ile namba 9 ya mwaka 2006 ya Zanzibar ielezavyo.
Sheria hii ikaenda mbali zaidi na kufafanua kuwa, ulemavu unaweza kuwa wa kudumu au wakati mwengine ni wa muda, huku baadhi ya magonjwa kama vile ya akili yanaweza kusababisha ulemavu pia.
Tendo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutunga sheria hii, ni kuona umuhimu na ulazimu ule uliomo kwenye katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwamba binadamu wote ni sawa mbele ya sheria.
Kumbe, serikali ilililia sana kundi la watu wenye ulemavu, na sasa najifunza kwamba, hata yule au mimi na wale, leo wanaviungo kamili, kesho wakipungikiwa, basi wamekuwa walemavu.
Sheria hii ya watu wenye ulemavu ya Zanzibar, ambao wenyewe walioutungiwa wakisema kwamba, inakidhi haja kwa baadhi mambo, imejumuisha vifungu 48 lakini kifungu cha 15 ni kizuri.
Chenyewe kimeelezea suala la mawasiliano kwa kundi hili, bila ya kujali aina ya ulemavu, kwamba serikali iwatekelezee, ili nao wawe sawa kwenye upatikanaji wa taarifa, kama kundi jengine.
Tena ukikichambua kifungu hichi kidogo cha (a), kimeainisha aina ya silabi ambazo zitatumika, kwamba ni maandishi ya nukta nundu, huduma za kanda zilizorikodiwa taarifa kwa maandishi makubwa.
Lakini hata wapatiwe huduma za kutafsiri, wasaidizi na waongozaji na lugha ya alama, imetajwa kwenye kifungu kidogo cha (d), naamini lengo ili nao waende sambamba katika upatikanaji wa taarifa hasa za umma.
Chakufurahisha na chakutia moyo katika kifungu cha 25 cha sheria hii, kimeeleza kwamba, lazima vituo vya kupigia kura, ikiwa ni haki ya kikatiba, vitengenezwe ili waweze kuvitumia.
CHAGUZI ZA VYAMA VINGI
Kwa mfano Tanzania na Zanzibar wameshaendesha changuzi sita za vyama vingi nchini, lakini kundi la viziwi linaendelea kukosa taarifa rasmi.
Wanasema mchakato wa uchaguzi sio siku ya kupiga kura tu pekee, bali huanzia tokea uandikishaji na kisha upachikaji majina kwenye vituo.
Tena kwenye kundi hili, mpaka wenye ulemavu wa usikivu (viziwi) walishiriki, ingawa wenyewe wanalilia kutotekelezwa ipasavyo sheria yao namba 9 ya mwaka 2006, juu ya upatikanaji wa taarifa kwa mujibu wa mazingira yao.
Kubwa wanasema, walianza kutengwa kwa kukosa taarifa tokea hatua za uandikishaji, uchaguzi wa wagombea ndani ya vyama, kampeni na kisha tukio kubwa la kupiga kura.
Wanasema kwenye vituo vya kupiga kura, Tume za uchaguzi za ZEC na NEC walishindwa kuwawekea wakalimani, ili kuwapa taarifa za kituo wanachopaswa kwenda ili kupiga kura.
Walitarajia sana, kama walinyimwa haki ya kufahamu kinachoendelea wakati wa kampeni, kwa kukosekana wakalimani, walau kwenye vituo kwa siku ya kupiga kura wengekuwepo.
Hidaya Mjaka Ali ambae anasimamia miradi ya watoto kutoka Umoja wa watu wenye Ulemavu Zanzibar ‘UWZ’ anasema alipokea malalamiko toka kwa wanachama wao, juu ya kukosa taarifa sahihi.
“Ni kweli wenzetu viziwi kwenye uchgauzi mkuu uliofanyika, waliachwa nyuma maana ile sheria yetu, kwenye kifungu cha 15 ya kupewa taarifa ikutekelezwa,’’alilalamika.
Yeye anasema, inawezekana kukosekana kwa wakalimani ni jambo lililofanywa kwa maksudi, maana hiyo haikuwa ni fursa bali ni haki kwa mujibu wa sheria, iliyopitishwa na baraza la wawakilishi mwaka 2006.
Bilali Mohamed Bilali Katibu wa Jumuiya ya wasioona wilaya ya Wete, ingawa kwa upande wao hakukuwa na mashaka makubwa, lakini kwa ndugu zao viziwi walikosa haki ya taarifa.
“Viziwi ni kweli walikosa mtu wa kuwapa taarifa sahihi kwenye vituo vya kupigia kura, ingawa sheria inasema kila mmoja apate taarifa za mawasiliano,’’alisema.
Asha Hilali Juma (kiziwi) wa Wete, akizungumza nami chini ya mkalimani wake, anaona vituo vya kupigia kura havikuwa rafiki kwao, kutokana na ulemavu wa usikivu walionao.
“Nilipofika sikukaa kwenye foleni, lakini sijui wapi jina langu lipo, na niliokuwa nikizungumza nao hawaelewi, maana mimi natumia lugha ya alama ’’,alilamika.
Lakini Ali Ali Makame wa Mkoani mweye ulemavu wa uziwi, alichokifurahia kwenye uchaguzi wa mwaka jana, ni kupewa kitambalisho maalum.
Anasema hicho kilimfanya asipange foleni, ingawa alipata tabu kujua chumba chake cha kupigia kura.
“Kila ninae muuliza kiwapi chumba changu cha kupigia kura kwa lugha ya alama, ananisemesha kama mimi sio kiziwi, kisha nikarudi nyumbani bila ya kupiga kura’’,alisema.
Baada ya kukaa zaidi ya saa moja kwenye kituo, aliamua kurudi nyumbani, bila ya kuitumia haki yake ya kupiga kura, baada ya kutokuwepo mkalimani kituoni.
Ingawa Mwanajuma Kombo Hija wa Kengeja Mkoani ambaye nae kiziwi, kwamba alifanikiwa kupiga kura, baada ya kuhangaika.
“Walikua wananifanya kama runinga, kisha wananicheka maana wao wananisemesha kama vile mimi sio kiziwi, sasa ilikuwa tabu,’’alifafanua.
Aliyekuwa Afisa wa tume ya Uchaguzi ZEC Pemba, Ali Mohamed anasema isingewezekana kwamba kila kituo kimoja awepo mkalimani, maana hilo halikupangwa.
“Sisi kama ZEC tumejitahidi walau kwepo kwa kifaa maalumu kwa wasioona, ili waweze kupiga kura kwa uhakika, jambo ambalo chaguzi zote walikuwa wakipigiwa’’,alisema.
Mkalimani wa lugha ya alama Pemba Asha Suleima, anakubali kuwa uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni Zanzibar, kundi la viziwi hawakupata taarifa sahihi za umma.
“Mimi ni mkalimani, lakini haikuwezekana kwenda kila jimbo ili kuwasaidia wenzetu hawa, sasa lazima serikali ijipange, ili kuhakikisha viziwi wanapata tarifa kwa uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025’’,alishauri.
Mratibu wa Kituo cha huduma za sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, akizungumza katika moja ya makongamano, alishauri lazima sheria zitekelezwe.
“Zanzibar tunaongoza kwa kuwa na sheria nyingi na mzuri, lakini ubaya wake unakuja kwenye utekelezaji, maana hata hii ya watu wenye ulemavu, kama ikitelezwa, basi ubora wake utaoonekana’’,alisema.
Yeye anaona ili sheria ionekane kama mzuri au inamapungufu lazima itumike “tested” na kinyume chake itakuwa kama nyumba iliojengwa pasi na kuhamiwa.
Taasisi mbali mbali za Zanzibar kama vile Chama cha waandishi wa habari Tanzania TAMWA -Zanzibar kabla ya kuingia kwenye ngwe ya kuchagua, ilitoa mafunzo kadhaa kwa kundi la watu wenye ulemavu.
Akisisitiza jambo katika moja ya mafunzo hayo Mratibu wa TAMWA Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, aliziomba tume zinazosimamia uchaguzi, kuhakikisha hakuna kundi la binadamu lenye sifa ya kuchagua au kuchaguliwa, kudhalilishwa kikatiba.
“Hata unapowakosesha wakalimani wenzetu viziwi ni aina nyengine ya udhalilishaji wa kidemokrasia, maana inawezekana wasipate haki ya kumchagua kiongozi kwa mujibu wa sera zake kwa kule kukosa taarifa sahihi’’,alisema.
Lakini hata Shirika la Internews Tanzania, ambalo liliwawezesha waandishi wa habari kimafunzo, ili kuandika habari na kutayarisha vipindi ambavyo vitawakumbusha wenye mamlaka kuwapa haki za wau wenye uziwi.
“Nyinyi waandishi wa habari lazima muziambie mamlaka husika, juu ya hawa wenzetu wenye ulemavu wa viziwi, kwamba, lazima wapatiwe haki zao hasa za kuwepo wakalimani kwenye mikutano na vituo vya kupigia kura’’,alisema mkuu wa Program wa Internews Shaaban Maganga.
Lakini hata aliyewahi kuwa mkufunzi kutoka shirika hilo Ofisi ya Zanzibar Ali Haji Mwadini, alisisitiza haja kwa waandishi wa habari kuandika habari za juu ya haki za kundi la watu wenye ulemavu.’
Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ Mwandawa Khamis Mohamed, amesema moja ya changamoto kubwa ni kundi la viziwi kukosa taarifa za umma.
Mjumbe wa baraza kuu la viziwi Zanzibar Mohamed Khamis, alisema bado wamekuwa wakifuata mkubo katika kila chaguzi kwa kukosekana mkalimani.
Aidha Said Khatibu kiziwi wa Mtemani Wete, anasema zisipotekelezwa sheria zao ipasavyo, ni kuongezewa unyonge katika taifa.
Mkurugenzi wa baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar mwalimu Ussi Khamis, alisema jamii inapaswa kusimamia haki za watu wenye ulemavu kikamilifu.
Mtendaji mkuu wa Shirikisho la Jumuiya za watu wenye ulemavu taifa Tanzania, Ernest Kimaya, anasema lazima tume za uchaguzi ziwajali viziwi.
“Viziwi ni jamii ya watu kama walivyo wengine, hivyo lazima uimarishaji kwa chaguzi zijazo ufanyike ili wapate taarifa zaote za mwenendo wa uchaguzi mkuu,’’anasema.
Mwisho
Comments
Post a Comment