NA MWANDISHI MAALUM, ZANZIBAR@@@@
AFISA Uchunguzi kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Ofisi ya Zanzibar, Abdul-latif Ali Sheha amewasihi wazazi na walezi wa Shehiya ya Kinuni, kujenga utamaduni wa kuzilinda na kuziishi haki za watoto kwa vitendo.
Abdullatif alitoa nasaha hizo kwa wazazi na walezi 637 katika Madrasatul
Thamaraatul Jannah iliyopo Shehia ya Kinuni, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akiwapa
hao elimu ya haki za watoto na wajibu wa jamii katika kuzuia vitendo vya
ukatili wa watoto na uvunjwaji wa haki za binadamu ikiwa ni mwendelezo wa kutoa
elimu na msaada wa sheria wakati wa mwendelezo wa zoezi la Kampeni ya Msaada wa
Kisheria wa Mama Samia Awamu ya Pili (MSLAC
II)
unaoendelea katika Wilaya tatu za Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Mtoto
ana haki ya kuishi katika mazingira salama, kupatiwa elimu na kulindwa dhidi ya
aina zote za unyanyasaji" Alisisitiza bw. Abdullatif.
Pia
aliwaeleza wazazi hao kuwa jamii inapaswa kuachana na tabia ya kuoneana muhali
katika kushughulikia matukio ya udhalilishaji. Sambamba na kuwahimiza wazazi
hao kujenga utamaduni wa kuripoti mara moja matukio ya udhalilishaji kwa
mamlaka za kisheria badala ya kuyamaliza kwa maelewano yasiyo rasmi au
kuwalazimisha watoto wa kike kuolewa na watu wanaodaiwa kuwafanyia
udhalilishaji.
Aliongeza
kuwa hatua hizo humwongezea mtoto madhara ya kisaikolojia, humkatiza haki yake
ya elimu na huathiri maendeleo yake ya baadaye.
Wakati
huo huo kwa maeneo mengine tofauti ya Mkoa wa Mjini Magharibi Ofisa huyo wa
THBUB Bw. Abdullatif, akishirikiana na maafisa wengine wa Sheria na Mawakili
kutoka Wizara za Katiba na Sheria za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa ushirikiano na Maofisa kutoka
Jeshi la Polisi kanda ya Zanzibar waliwafikia wanafunzi wengine 465 na walimu wa
Madrasa tatu zilizomo ndani ya Mkoa huo zikiwemo "Madrasatul
Answaar", "Madrasatul Fatma Islamia" na "Madrastul Nurrul
Islamiyya" katika kutoa msaada wa kisheria na elimu ya haki za binadamu wakti
wa mwendelezo wa Kampeni ya Msaada wa
Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili (MSLAC
II)
inayoendelea visiwani Zanzibar.
Halikadhalika
maofisa hao waliwaelekeza wanafunzi hao, kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria,
pamoja na kujiepusha na vikundi viovu vinavyojihusisha na dawa za kulevya,
vibanda vya gemu chafu, tamaa, pamoja na kuwaelimisha juu ya kujiepusha na
michezo ya kubeti.
Kwa
upande wa Jesho la polisi liliwafunza wanafunzi wa Madrasa hizo kujenga
utamaduni wa kutoa taarifa kwa mamlaka za kisheria hasa wanapokumbana na
matukio yanayohatarisha usalama wao na uvunjifu wa amani.
Mafunzo ya haki za binadamu na msaada wa kisheria yaliyotolewa kwa wanafunzi wa Madrasa hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili (MSLAC II), yenye kaulimbiu isemayo "Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo" ambayo ilizinduliwa rasmi visiwani Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi Juni 20, 2026 ambapo maonesho ya Kampeni hizo yaliendelea katika viwanja vya Nanenane vilivopo Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi A na maonesho hayo yanaendelea kwa wilaya tatu za mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yanatarajiwa kutamatika, Julai 05, 2026.
Aidha, THBUB imeendelea kutoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda haki za watoto kwa kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kila mtoto anapata ulinzi, haki na fursa ya kukua katika mazingira yenye usalama, utu na heshima.
MWISHO
Comments
Post a Comment