NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKUU wa wilaya ya Wete Rashid Abdalla
Rashid, amesema jambo la kugawa chakula kwa mayatima, lililofanywa na Shirika
la Bima Zanzibar ‘ZIC’ ni la kiutu na linafaa kuigwa na mashirika mingine.
Mkuu huyo wa wilaya, aliyasema hayo jana, kwenye
kijiji cha kulelea mayatima, Bwagayamoyo Mtambwe Wete, mara baada ya kumaliza
hafla ya ugawaji wa chakula kwa ajili ya sikukuu, iliyoandaliwa na ‘ZIC’.
Alisema, ‘ZIC’ imefikiria jambo jema kwa watoto hao,
kwani wameondokewa na baba zao, hivyo wanapopata mashirika kama hayo, hurejesha
matumaini na furaha.
Alieleza kuwa, ijapokuwa kuondokewa na jambo kubwa
na linalochelewa kusahaualika, lakini ugawaji huo wa chakula hicho, na kwa
uhakika, inawapunguzia machungu watoto hao.
‘’Kwanza niwapongeza sana wenzetu wa ‘ZIC’ kwa uamuzi
wao, kwanza kuwagawiya futari mayatima tena hawa, waliopo hapa Mtambwe,’’alisema.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya ya Wete,
aliwataka wazazi na walezi wanaowalea watoto hao mayatima, kuendelea kuvumilia,
kwani ulezi wa mzazi mmoja, huwa na changamoto zaidi.
‘’Hata ulezi wa watoto ambao wazazi wao wote wawili
bado wapo hai, huwa ni mgumu, hivyo na nyinyi endeleeni kuvumilia, katika hili,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, amelitaka shirika la Bima
Zanzibar ‘ZIC’ kuendelea kuwa karibu na makundi mbali mbali, ili matunda yake yarudi
kwa jamii.
Mapema Mkurugenzi Utawala ‘ZIC’ Juma Khamis Hija alisema, wamekuwa na utamaduni wa kushirikiana na jamii, katika nyanja mbali mbali, ikiwemo elimu.
Alieleza kuwa, hata msaada huo wa chakula kwa ajili
ya mayatima, ni eneo moja wapo la kushirikiana jamii.
‘ZIC ni shirika la wananchi wenyewe, hivyo kila muda
tumekuwa tukikutana nao, iwe ni kwenye huduma za kibinaadamu, elimu au afya kwa
ajili yao,’’alifafanua.
Hata hivyo, amewakumbusha wananchi kundelea kukata
bima mbali mbali, ikiwemo ya vyombo vya maoto, nyumba, bima za maisha na mali
nyingine.
Mapema Kaimu Meneja wa ‘ZIC’ Pemba Saida Baraka Saleh
alisema, wamekuwa wakiwajali mno wananchi wote, na hasa wale waliokatika
mazingira magumu, wakiwemo mayatima.
Alieleza kuwa ‘ZIC’ itaendelea kushirikiana na kuwa karibu
na jamii, kwani ni shirika lao, kama yalivyo mingine kutoka serikalini.
Hata hivyo, alisema jambo la kuwapa chakula mayatima
ni jema, na ndio maana uongozi wa ZIC, umeamua kukutana nao na kuwapa chakua
hicho.
‘’Sisi ZIC tunawajali wananchi wote, na ndio maana
leo tumeshagawa vyakula kwa mayatima na familia zao,’’alifafanua.
Akisoma risala ya kijiji hicho, mwakilishi wa wazazi
hao Mohamed Sharif Mohamed, alisema wamekuwa wakikabiliwa na chagamoto ya ukosefu
wa umeme kijijini hapo.
Alisema jingine, ni umbali wa kituo cha elimu ya
maandalizi kwa watoto, ukosefu wa usafiri hasa nyakati ya usiku, inapotokezea
dharura, jambo linalowapa ukakasi wa maisha.
Wakati huo huo, ungozi wa ZIC uliungana na watoto hao mayatima na familia zao, katika futari ya pamoja, iliyofanyika kijijini hapo.
Kijiji cha kulelea watoto mayatima kilichopo Bwagamoyo
Mtambwe, ambacho kina nyumba 14, kinajumuisha watoto 52, wakiwemo wakike 32 na
wanaume 20.
Mwisho
Comments
Post a Comment