NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, utakaofanyika Aprili 2 mwka huu katika Uwanja wa michezo Gombani Chake Chake Pemba.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2026 ofisini kwake Chake Chake Pemba.
Alisema kuwa, katika uzinduzi huo Dk. Mwinyi atahutubia wananchi pamoja na kuzindua rasmi mbio za mwenge wa uhuru na kuendelezwa kwa ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo katika wilaya nne kisiwani Pemba.
Alisema, mwenge wa uhuru hukimbizwa nchi nzima ikiwa ni sehemu ya kuenzi uhuru wa taifa, kuenzi maendeleo ya nchi sambamba na kudumisha Amani, mshikamano na maelewano ya wananchi katika shughuli mbali mbali za maendeleo ya taifa.
"Mwenge wa uhuru mwaka huu 2026 unatarajiwa kuzinduliwa Pemba kitaifa mnamo tarehe 2 Aprili, 2026 katika uwanja wa Michezo Gombani wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba, hivyo tunawaomba muzifikishe taarifa hizi kwa wananchi ili wahudhurie kwa wingi,’’
Alieleza kuwa, matayarisho ya uzinduzi wa mbio za mwenge huo yamekamilika na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kikamilifu kuhakikisha tukio hilo la kihistoria linakamilika kwa mafanikio makubwa.
Mkuu wa mkoa huyo alieleza kuwa, vikundi vya usalama, vikundi vya hamasa na halaiki vimejipanga ipasavyo na kuhakikisha viongozi na wananchi kwa ujumla wanakua salama.
Alieleza, tukio la uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru linatarajiwa kudhuriwa na viongozi mbali mbali pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Tanzania, hivyo aliwaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika tukio hilo la kihistoria.
Mkuu huyo aliwataka wananchi kuendeleza umoja na mshikamano ulipo Zanzibar, ili kudumisha taswira nzuri iliopo katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Aliwahakikishia wananchi usalama wa kutosha katika uzinduzi huo, huku akieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga katika kuhakikisha hali hiyo inadumu katika mkoa huo.
"Niwahakikishie wananchi usalama upo katika Mkoa wa Kusini Pemba na vikosi vya ulinzi na usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha hali hiyo inadumu muda wote", alisisitiza.
Aidha, aliwataka wananchi kutoka maeneo yote ya Tanzania kufika katika Mkoa wa Kusini Pemba kujumuika kwa pamoja ili kufanikisha kwa kiasi kikubwa uzinduzi huo.
Alifahamisha kuwa, baada ya kukamilika uzinduzi huo, mwenge wa uhuru utaanza mbio zake katika wilaya ya Chake chake na Mkoani, pamoja na kuendelea kukimbizwa katika wilaya nyengine na mikoa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.
Hivyo aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano uliopo nchini hususan katika kipindi hichO cha uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru, ili kuhakikisha tukio hilo linamalizika kwa salama na amani.
Hata hivyo aliwasihi wafanyabiashara na wajasiriamali wa bidhaa mbali kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa zao, pamoja na kudumisha usafi katika maeneo yao ili kudumisha haiba ya maeneo yao.
Alisema, iwapo wafanyabiashara watatumia vizuri fursa hiyo watawawezesha wageni kuona bidhaa mbali mbali sambamba na kujionea fursa za kiutamaduni na utalii zilizopo kisiwani Pemba.
‘’Tuna vivutio vingi vya utalii kwenye Mkoa wetu na Pemba yote kwa ujumla, hivyo tunawaomba wageni watakaofika kisiwani hapa pia wakajionee historia zetu ambazo ni za kusisimua, kufurahisha na kujifunza,’’ alifafanua Mkuu huyo.
Mwenge wa uhuru kitaifa mwaka huu utazinduliwa Aprili 2 katika uwanja wa Michezo Gombani Chake Chake Pemba, ambapo hilo ni tukio la pili kufanyika kisiwani Pemba, kwani miaka kumi iliyopita mwenge wa uhuru kitaifa ulizinduliwa Chokocho wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Comments
Post a Comment