NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
……..MWENGE wa uhuru ni chombo cha kitaifa.
Baada ya taifa la Tanzania kupata huru, kilianzisha
chombo hicho, kikiwa na malengo kadhaa ndani yake.
Kwa wakati huo, taarifa zinaeleza ni
hayati Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndie
aliyeuasisi.
Kumbe unaweza kuthibitisha kuwa, chimbo
la mwenge huo wa uhuru, ni maono ya Baba wa taifa, hasa pale alipousimamisha
juu ya mlima Kilimanjaro.
Akatamka kuwa, ‘lengo ni kuleta
matumaini pale pasipo na matumaini, upendo pale penye chuki na heshima pale
palipojaa dharau’.
Mwenge huo, kwa mara ya kwanza, uliwashwa
mwaka 1961, baada ya Mwalimu Nyerere kumteua Luteni Alexander Gwebe Nyirenda
kutekeleza azma hiyo iliyoitwa “Operesheni Mwangaza”.
Kwa mwaka jana, aliyekua Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philipi Isdori Mpango, wakati akiwahutubia wananchi
wa Mkoa wa Pwani, kwenye uzinduzi, alisema mwenge ni kielelezo cha umoja na
mshikamano.
Akafafanua kuwa, tangu wakati huo, mwenge
huo umekuwa ukikimbizwa katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, bara na visiwani, na kupitia mbio hizo hamasa kubwa huonekana.
Ingawa kwa mwaka huu, heshima ya uzinduzi wa mwenge huo wa
uhuru, umepewa Mkoa wa kusini Pemba, tena ndani ya wilaya ya Chake chake.
Pamoja na mambo mingine, tayari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, imeshaandaa
zaidi ya kamati saba kwa lengo la kufanikisha maandalizi.
Maana, Mkuu wa huo Rashid Hadid Rashid, anasema zipo kamati
kadhaa, ikiwemo ya hamasa, usafiri, afya na zote zinafanyakazi kwa
kushirikiana.
Kwenye uzinduzi wa mbio hizo za uhuru kwa mwaka huu, ipo kaulimbiu,
ambayo inamaana pana na halisi kwa watanzania.
‘’TANZANIA NI YETU SOTE, TUSHIKAMANE KWA PAMOJA, KULETA MAENDELEO’
Hii ndio kauli mbiu ya ujumbe wa mwenge wa uhuru wa mwaka 2026,
ambapo ndani yake imebeba vijumbe vidogo vidogo kadhaa.
Kauli mbiu hii, ilichambuliwa vyema na Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba,
Rashid Hadid Rashid, akisema Tanzania ni ya watu wote.
Akafafanua kuwa, hakuna haja ya kujitokeza kwa wachache,
kuichafua Tanzania, kwa maslahi ya mtu mmoja.
‘’Kwa mfano, ukichambua neno Tanzania ni yetu sote, hapa
inakukataza wizi, uchafuzi wa amani, rushwa na hata matuzi ya dawa za kulevya,’’anasema.
Akaeleza kuwa, neno ‘tushikamane’ inamaana pana zaidi,
ikiwemo kila mmoja anawajibu wa kuliletea maendeleo taifa hili.
Akiwa na maana, kuwa suala la kuwa na maadili ya kazi, kwenye ofisi
za umma na binafsi, linasaidia mno, kwa watanzania kuheshimiana.
‘’Tunapogusia maana halisi ya mshikamano, sio kwa
watendaji wakuu wa serikali pekee, bali hata mwananchi wa kawaida, mtumishi wa
chini na wale wa waliojiajiri,’’anaeleza.
Mratibu wa mwenge mkoa wa kaskazini Pemba Zadida Abdalla,
anasema ‘kushikamana na kuleta maendeleo’ ni wajibu wa mwanachi
kuungana na viongozi, pale wanapoleta miradi.
Anaona kuwa, maagizo na miradi ya serikali haiwezi kufanikiwa
vyema, ikiwa kila mmoja hatoitilia maanani kaulimbiu ya mwenge ya mwaka 2026.
Mratibu huyo anasisitiza kuwa, isiwe kuwa mwenge umekuja na kufurahia
pekee, bali maneno yaliotengeneza kauli mbiu, ni muhimu kuyachambua.
‘’Ndani ya maneno ya kaulimbiu ya mwenge wa uhuru kwa mwaka
2026, ukiamua kuyachambua ni darasa tosha la kila mmoja, kutekeleza wajibu wake
tena pasi na kusimamiwa,’’anaeleza.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, akizungumza na
masheha, aliwataka kuwaelezea wananchi, maanali halisi ya kualimbiu ya mwenge ya
mwaka huu.
Akaeleza kuwa, imekuja kuharakisha umoja, mshikamano na ulinzi
wa taifa, bila ya kujali mtu dini yake, rangi wala wapi anatokea.
Hata Katibu Tawala mkoa wa Kusini Pemba, Mwalimu Amour, wakati
akizungumza na kamati za matayarisho ya uzinduzi wa mwenge huo, alisisitiza kuizingatia
kauli mbiu.
‘’Kauli mbiu huwepo nyingi kila mwaka na kila kwenye uzinduzi wa
mwenge, lakini hii ya mwaka huu, imekusanya kila kitu,’’anasema.
WANANCHI NA KAULIMBIU YA MWENGE 2026
Issa Haji Machano wa Mkoroshoni Chake chake, anasema kaulimbiu ya
mwaka huu, inafahamika kwa haraka, maana halisi iliyokusudiwa.
‘’Ukiisoma kama inakutaza kula rushwa, kuacha wizi, viya dhidi
ya dawa za kulevya, maana ndani yake mna neno ‘Tanzania ni yetu sote’,’’anaeleza.
Ilyassa Hassan Omar wa Kichungwani anasema, ndani ya sentesi ya
kaulimbiu ya mwaka huu, inatoa taaluma, kwa kila mtanzania.
Habiba Kombo Othman, anasema kama kila mmoja kuanzia viongizi
hadi wananchi wa kawaida, wataifanyia kazi kaulimbiu ya mwenge ya mwaka huu, hakurajii
mabaya.
‘’Maana kama vile inakataza udhalilishaji, matumizi mabaya ya
ofisi, rushwa, lishe bora, maana sentensi zake zimepangika,’’anasema.
Mwanahija Hassan Kassim wa Pondeani Chake chake, anasema kama
sio Tanzania kuzidiwa na wanasiasa wapotoshwaji, basi ujumbe huo ni darasa tosha,
kwa wananchi.
‘’Wapo wingine wanaweza kuubeza, lakini kama utatulia na kuusoma
kwa umakini, na kisha kuanza kuuchambua, utagundua umebeba kitabu kizima,’’anaeleza.
VIJUMBE VYA KUDUMU VYA MWENGE
Kwa kawaida, kila mwaka kaulimbiu ya mwenge, hubadilika kwa aina
ya mazingira, ingawa vipo vijumbe vyingine kadhaa, ambavyo ni vya kudumu.
Mfano, suala la lishe bora, ni ujumbe ambao upo kwa muda mrefu,
ambapo wakimbizwa mwenge hutakiwa kuwachambulia wananchi.
Eneo jingine ni vita dhidi ya dawa za kulevya, malaria, ukimwi
na janga jingine la kupinga suala la rushwa Tanzania.
MGENI RASMI KWA MWAKA 2026
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa mwenyeji wa uzinduzi wa mwenge huo wa
uhuru kitaifa, anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi ni, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Juzi akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, alisema Dk. Mwinyi
atawasili ndani ya uwanja wa Gombani Chake chake, kwa ajili ya kazi hiyo na kisha
kuwahutubia wananchi.
Akaeleza kuwa, baada ya zoezi hilo, mwenge huo utakabidhiwa kwa uongozi
wa wilaya ya Chake chake, kwa ajili ya kukimbizwa na ufunguzi wa miradi na
uwekaji wa mawe ya msingi utafuta.
Kumbe kabla ya April 4, kwenye mkoa wa kaskazini Pemba, siku
inayofuata itakuwa ni zamu ya wilaya ya Mkoani, ambapo mwenge huo utaifungua na
kuitembelea miradi iliyopangwa.
BURUDANI
Mkuu huyo wa Mkoa, aliwaalika wananchi wake na wale wa kaskazini
Pemba, ambapo pamoja na mambo mingine, ni kuburudishwa na wasanii.
Akasema, wameshamualika msanii Mau Mpemba, Maswga classic, K-Official,
msewe wa vijana Mchangamdogo, Kirobo na Dula Makabila kutoka Tanzania bara.
Eneo jingine, alisema watakaohudhuria watawaona mubashara,
watoto wa halaiki, waliofunzwa na kufunzika, wakiandika maumbo kadhaa.
Utenzi na kwaya zenye nyimbo za ufafanuzi wa kaulimbiu ya mwenge
na vijumbe vyake vya kudumu, zitatikisa ndani ya uwanja wa Gombani.
Akaongeza kuwa, mwenge wa
uhuru hukimbizwa nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya kuenzi uhuru wa taifa.
Pia ni kuenzi maendeleo ya nchi, sambamba na kudumisha amani,
mshikamano na maelewano, miongoni mwa wananchi.
Anaeleza kuwa, matayarisho ya uzinduzi wa mbio za mwenge huo,
yamekamilika na serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imejipanga kikamilifu
kuhakikisha tukio hilo la kihistoria, linakamilika kwa mafanikio.
Akwasihi wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia fursa hiyo,
kutangaza bidhaa zao, pamoja na kudumisha usafi, katika maeneo yao ili kulinda
haiba ya maeneo yao.
MWISHO
.jpg)


Comments
Post a Comment