WANANCHI wa mkoa wa kusini Pemba,
wameipongeza hutuba ya uzinduzi wa mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka 2026,
iliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein
Ali Mwinyi.
Walisema, hutuba
hiyo ilitoa mwelekeo wa umoja, mshikamano, upendo miongoni mwa wananchi wa
Tanzania, jambo linalofaa kuungwa mkono.
Wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa hafla ya
uzinduzi wa mwenge huo, jana uwanja wa michezo Gombani, walisema hutuba
imewakumbusha watanzania wajibu wao, kwa maslahi mapana ya taifa.
Mmoja kati ya wananchi hao Ali Ameir Haji wa
Mchangamdogo, alisema hutuba hiyo kama wananchi waliifuatilia kwa makini, basi ni
darasa tosha wa ujenzi wa amani.
Alieleza kuwa, hutuba nyingi anazozitoa Dk. Mwinyi
kwenye hafla kadhaa za kitaifa, huwa na mwelekeo mpana, ingawa hiyo ya kwenye
uzinduzi wa mwenge wa uhuru, imeongezeka mara dufu.
‘’Kwa hakika hutuba hiyo, ilijaa kila kitu mfano,
imehamasisha upendo, nidhamu, umoja na mshikamano wa dhati miongoni mwa wananchi
wa makundi mbalimbali,’’alifafanua.
Nae Ibrahim Haji Machano wa Mkoani, alisema yeye
hutuba hiyo ilimnasa, hasa alipozungumzia suala la kuulinda na kuuendeleza
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alifahamisha kuwa, mara nyingi Dk. Hussein Ali
Mwinyi, huwa haachi kuugusa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ingawa kwenye
hutuba yake ya jana, alionesha vitu tofauti vya kuulinda.
‘’Kwanza alisema kila mmoja anaowajibu wa
kuhakikisha, Muungano huo anauenzi, na alionesha faida kadhaa ikiwemo ulinzi,
usalama, upendo na kuwaunganisha wananchi wote,’’alifafanua.
Kwa upande wake Mwanaisha Haji Makame wa Mtambile,
alisema hutuba hiyo inafaa kutengenezewa kitabu maalum, na kusambaazwa kwa wanafunzi
na makundi ya kijamii.
Alishauri kuwa, kwa vile imejaa nasaha, rai,
ushauri na mwelekeo wa taifa kwa ujumla, ni vyema wananfunzi hasa wa skuli za
msingi na makundi mingine, kuwafikia.
‘’Ushauri wangu hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alioitoa wakati wa uzinduzi wa
mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, ichapishwe na iwekwe pamoja na kusambaazwa,’’alishauri.
Mwajuma Haji Kombo wa Ole, alisema mwananchi
alikuwa kwenye usikivu mzuri, wakati Dk. Mwinyi anatoa hutuba hiyo, iliyogusia
pia njia za kupamba na dawa za kulevya.
‘’Kwanza alisema, kila mmoja anawajibu wa
kushirikiana na Mamlaka husika, katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, maana
kwa serikali pekee vita itakuwa ngumu,’’alisema.
Mapema Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Rashid Hadid
Rashid, akitoa salama za mkoa huo, alizipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na ile ya Zanzibar, kwa kuwaamini na uzinduzi, kufayika mkoani
humo.
Alisema, naamini utulivu, upendo, usikivu na
mazingira bora yaliomo ndani ya mkoa huo, yamechangia kwa mkoa wa kusini Pemba,
kuingia katika historia kwa mara ya pili.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Chake chake Rashid Abdalla,
alisema uzinduzi wa mwenge huo mkoa wa kusini Pemba, ni ishara ya umoja, upendo
na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi,
aliwakumbusha wananchi wajibu wao katika vita dhidi ya udhalilishaji.
Alisema, kila mmoja anaowajibu kushirikiana na mamlaka
nyingine, katika kuhakikisha Tanzania, inaendelea kubaki salama.
Kabla ya uzinduzi wa mwenge huo wa uhuru, wananchi na
viongozi mbalimbali waliohudhuria, walikonga nyoyo zao kwa ngoma asili, utenzi,
halaiki na mchezo wa sarakasi.
Mwisho
Comments
Post a Comment