Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Wizara ya Ardhi na
Maendeleo ya Makaazi (WAMM) jana imesaini Hati ya Makubaliano na Kampuni ya Kitaifa
ya Kijiografia na Misitu (IGN FI) ya Ufaransa kuhusu Mradi wa Taarifa za Usimamizi
na Usaji wa Ardhi Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya
hafla ya utiaji saini waziri dhamana wa wizara hiyo Mhe. Rahma Kassim Ali amesema kufanya kazi kwa
mfumo wa taarifa za Usimamizi na Usajili wa Ardhi utasaidia kwa kiasi kuondosha
migogoro ya ardhi iliyokuwepo Zanzibar.
Waziri Rahma aliyasema
hayo baada ya kushuhudia hafla ya utiaji saini ambapo ilifanyika Wizara Ardhi
na Maendeleo ya Makaazi, Maisara Unguja. Alisema hatua hiyo ya utiaji saini ina
manufaa makubwa hasa katika kuondoa migogoro ya ardhi ambayo inaonekana
kujitokeza kila siku.
“Tunaamini mfumo huo utasaidia sana kwani
taarifa zitakuwa kwenye mfumo na mmiliki husika hasa wa ardhi atajulikana kwani
taarifa za ardhi zipo kwenye karatasi
lakini mfumo sio rahisi kupoteza taarifa.” Alisema waziri huyo.
Waziri Rahma alisema hivi
sasa wizara yake inaendelea na zoezi la utambuzi wa ardhi ambapo pia taarifa
zake zitaingizwa katika mfumo na tayari wamefanya zoezi la utambuzi katika shehia
50 zimeshafanyiwa kazi na mategemeo ya Serikali ni kuitambua ardhi yote katika
shehia 388 za Unguja na Pemba.
“Mfumo huu tuna matumaini
makubwa kwamba migogoro ya ardhi mingi itaondoka na itakayokuwepo ni ile ya
kawaida lile tatizo kubwa ambalo linatukumba wizara litaondoka kwa asilimia 95 na
itakuwa manufaa makubwa ambayo Serikali ya awamu ya nane imepiga hatua kubwa.”
Alifafanua Waziri Rahma.
Hivyo alisema anaamini
ndani ya mwezi mmoja upembuzi yakinifu wa mfumo huo utakuwa umeshakamilika na
kwenda kwenye mfumo wenyewe hivyo ni matumaini yake ndani ya mwaka huu kabla ya
2024 mfumo huo utakamilika na kuanza kutumiwa rasmi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Dk.
Mngereza Mzee Miraji, alisema mfumo huo utakapoanza kazi utakuwa na faida kubwa
ikiwemo ya kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi kwa wawekezaji na wananchi,
kupunguza urasimu na kutoa huduma rahisi ya kuaminika na salama kwa wateja
kwani wananchi na wawekezaji wamekuwa wakitoa malalamiko katika jambo
hilo.
Alisema pia utapunguza
muda wa kukagua, kusahihisha na kubadilisha ama kuhamisha umiliki wa ardhi kwa
wananchi wawekezaji na miradi yote inayofanyika Zanzibar, kupunguza uvamizi wa
ardhi, misitu, hifadhi za barabara na sehemu za wazi, uhifadhi wa ardhi na
maliasili na kupunguza rushwa na viashiria vyote vya rushwa hasa ya ufatiliaji,
usajili na uhamisho wa hatimiliki.
Mhandisi Dkt. Mngereza
alibainisha kuwa utiaji saini huo ni mwanzo mpya ya kimapinduzi katika sekta ya
ardhi nchini ambalo ndio lengo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuondoa urasimu na kuondoa migogoro ya ardhi
hapa Zanzibar hivyo matumizi ya teknologia mpya ni njia moja ya kutatua
changamoto zilizokuwepo katika suala la ardhi Zanzibar.
Mapema Mrajis wa Ardhi Dkt.
Abdul-Nasser Hikmany alisema mfumo huo utasaidia kiutendaji pamoja na kutoa
huduma bora kwa jamii kupitia Kamisheni ya Ardhi Zanzibar ambapo taasisi hiyo
iko chini ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar.
Dkt Hikmany alisema
malengo ya taasisi hiyo kuwa taarifa
zote ambazo zitahusu ardhi zitaingizwa katika mfumo huo ikiwemo utambuzi,
mipango miji, usajili na mambo mengine ikiwemo maombi ya umiliki wa ardhi.
Alielezea kwamba mfumo
huo sio mpya duniani kwani umeshatumika
katika nchi nyengine ikiwemo Uganda, Seralione na hata Tanzania bara ambao
ufanya kazi kwa muda wa miaka mitano.
“Leo tumetia saini Hati
ya Makubaliano kwa ajili ya kutekeleza upembuzi yakinifu ambayo itatuonesha
gharama ya mfumo huu na utatengenezwa kwa jinsi ya mazingira ya Zanzibar
yalivyo.” Alisema Dkt. Hikmany.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Kitaifa ya Kijografia na Misitu (IGN FI) ya Ufaransa Christopher Dekeyne,
alipongeza Serikali kufanya kazi pamoja na Taasisi yake kwani na wana uzoefu
mkubwa katika mabara mengi hasa ya Afrika
wamefanikiwa na mradi huo na umeleta manufaa. Hivyo anaamini kwamba
mfumo huo utaleta tija Zanzibar.
Alisema kazi hiyo itaanza
kwa kufanya upembuzi yakinifu kujua mazingira ya Zanzibar na vitu
vitakavyohitajika ili kuwa na mradi utakaokidhi haja na mahitaji ya Zanzibar na
kuwezesha kutengeneza mfumo ambao utaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka huu
kwa ajili ya kuinua uchumi wa Zanzibar.
Aidha alisema ni
matumaini yake kwamba watapata ushirikiano wa kutosha ili kuweza kufanikisha
mradi huo na kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.
Mwisho.
Comments
Post a Comment