HABIBA
ZARALI, PEMBA@@@@
“HATUWEZI
kwenda na kasi ya maendeleo, kwetu kutokana na uchakabu wa barabara,’’wanasema
wananchi na watumiaji wa barabara ya Konde- Msuka.
Wakaongeza kuwa, hata gari ya abiria hawana, shida kubwa
hasa wanapotaka kwenda mjini kwa ajili ya kufuata matibabu.
Wakizungumza na mwandishi wa makala haya, wananchi wa kijiji
cha Msuka wilaya ya Micheweni mkoa wa kaskazini Pemba, wanasema hawajui ni lini
watajengewa barabara hiyo.
Kwa kuwa barabara huchangia pato kubwa katika maendeleo
ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, ndio maana wananchi hawa sasa wanataka
kujengwa barabara ya kudumu.
Kuna shughuli nyingi ambazo bila ya kuwepo miundombinu ya
barabara haziwezi kufanyika ama kufanyika kwa wakati wake.
Ingawa umuhimu wa barabara hauonekani kwa ghafla mpaka
pale panapotokezea tatizo, ikiwemo wafanyabiashara, wanapotaka kuingiza ama
kutoa bidhaa zao mbalimbali.
Akina mama wanapotaka kufuatia huduma za afya katika
hospitali kubwa ama za rufaa hakuna mafanikio bila ya kuwepo kwa barabara.
WANANCHI
WANASEMAJE
Halima Khamis Abdalla (50) anasema tokea azaliwe,
barabara yao hiyo imekuwa ikipokea ahadi, na hadi sasa haijajengwa na
wanaendelea kupata usumbufu.
‘’Kwa ahadi za kujengwa kwa barabara yetu hii,
zimeshatolewa zaidi ya 20, lakini mimi sasa natimizi miaka 50, bado huna
utekelezaji,’’anasema.
Anasema barabara hiyo yenye mashimo makubwa na mchanga
mwingi kwa baadhi ya maeneo hata wakiwaita wenye gari wanapofikwa na tatizo
kama la kuhitaji kufika hospitali au safari ya haraka hawataki.
Wengi wa wenye agari huhofia kupata hasara badala ya
faida, kutokana na uchakavu wa miundombini ya bara bara hiyo, kw amuda mrefu
sasa.
“kila siku tunaambiwa barabara iko kwenye bajeti, lakini
hatuoni maendeleo yoyote nasi tunatamani kuwa nayo kama wenzetu wa maeneo
mengine”, anasema.
Rufea Mohamed Seif anasema wenye kupata tabu zaidi ni
wanawake hasa pale wanapofuatia huduma mbalimbali za kijamii huko mtaa wa Konde
na Micheweni.
Anaona sio ajabu kwa akinamama wa Msuka kujifungulia
njiani wakiwa ndani ya magari ya Ng’ombe, kwani hawana gari kutokana na uchakavu
wa barabara yao.
Akitowa ushuhuda wa mtoto wake baada ya kujifunguwa
njiani Maryam Adam Juma, anasema baada ya kukosa usafiri wa gari ilibidi mwanawe
aingizwe kwenye gari ya Ng’ombe na hatimae kujifungua kabla ya kufika hospitali.
Kwake hali hiyo hujitokeza pale wenye gari zao kukataa kuwapeleka
huku wakidai kuwa, mara wanaporudi hulazimika kwenda kwa mafundi kutengeneza.
"Kwa kusema kweli ni mateso makubwa, maana sisi huku
ni watu tunaishi tu ila kwa upande wa barabara, hatujanufaika nayo", anaeleza.
Hapa akasema, lazima mamleka zijue kuwa, inapokosekana
barabara ya kisasa katika kijiji, waathirika wakubwa ni wanawake na watoto na
sio wengine woowte.
‘’Mwanamke ndio mzazi, ndio mlezi, ndio anayefuatilia
huduma za kijamii kutoka kijijini hadi mjini, sasa barabara ikiwa chakavu
waathirika ni sisi,’’anasema.
Ali Juma Mohamed
anasema wamechoka kupigwa dana dana kila siku huambiwa barabara hiyo iko katika
mpango wa kutatengenezewa, lakini
hawauoni.
Anasema huwa na woga sana wake zao wanapotaka kujifunguwa,
kwani hulazimika kuwaingiza kwenye gari za Ng’ombe kuburuzana na wakati
mwengine huzaa njiani.
“Tunaiomba serikali nasi ituone, kwa uhakika tunateseka
wananchi wa Msuka hasa ukizingatia barabara, ndio kila kitu katika kujiendeleza
kiuchumi”, anasema.
Akasema huduma za kijamii, haziwezi kutimia vyema kama miundombinu
ya barabara iko chakavu, kwani ndio kichecheo kikubwa cha kusukuma mbele
maisha.
Bimkubwa Salim Fadhil anasema roho ina choyo na wao hadi
sasa wanapoona maeneo ya wenzao wamefikiwa na huduma ya barabara hutamani nao
siku na moja waweze kupata huduma hiyo.
“Yote hayo nasi kama wananchi tunaopata shida hiyo ya
barabara lazima tuone wivu na tutamani siku moja tuone tunapita katika barabara
safi kabisa.
WAFANYABIASHARA
WANASEMAJE
Salim Makame mfanyabiashara ya samaki kutoka Chake chake
anasema tatizo kubwa linalowarejesha nyuma, ni uchakavu wa miundombinu ya barabara,
kwani huwawia vigumu kutoka Konde hadi bandari ya Msuka na kurudi.
Kwa sababu ya
ubovu wa barabara hiyo yenye mashimo na mchanga mwingi, kwa muda mwingi
hughairi kwenda kununuwa samaki, katika badari hiyo kwani vyombo vyao vya
usafiri wanaporudi huharibika.
“Mimi naamini wafanyabiashara tunapokuja kwa wingi katika
badari ya Msuka na tukanunuwa bidhaa maendeleo zaidi wanayapata wananchi
wenyewe,’’anafafanua.
Juma Ali Kombo mfanyabiashara wa vyakula, anasema
itakapotengenezwa barabara ya Konde -Msuka wataweza kufanya biashara zao bila
ya shida.
Kwa sasa wanalazimika kupata hasara, kwani hiyo gari
inayowapelekea bidhaa zao, lazima wapandishe bei kutokana na uchakavu wa
barabara.
VIONGOZI
WA SERIKALI
Sheha wa shehia ya Msuka Magharibi Amina Khatib Ali, anasema
miongoni mwa hatuwa, waliyoichukuwa ni kupeleka taarifa hizo katika Ofisini ya mkuu
wa wilaya kwa hatuwa za mbele.
"Kwa kweli barabara yetu ya Konde- Msuka ni mbovu na
hakuna linaloendelea la kimaendeleo bila ya barabara,’’ alisema.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, anasema barabara
hiyo imo kwenye mpango wa barabara za wilaya zitakazojengwa.
Anasema anafahamu kuwa wananchi wa Msuka, wana kiu ya
maendeleo lakini wavute subra, hadi pale muda utakapofika wa utengenezaji wa
barabara katika wilaya yao.
“Naelewa wananchi wanakiu ya maendeleo, lakini nawaomba
muwe wastahamilivu bara bara yenu, imo katika mpango wa kutengenezwa, ili na
nyinyi muweze kufaidika “, alisema.
Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Pemba Ibrahim Saleh Juma anasema kwa upande wa Pemba barabara za ndani ambazo
ziko katika mpango wa ujenzi ni kilomita 134.95 ikiwemo ya Msuka yenye kilomita
4.1.
Ambapo kwa ujumla katika wilaya ya Micheweni zipo jumla ya barabara sita
zinazojumuisha kilomita 47.4 na zimo katika mpango wa ujenzi kwa kiwango cha
lami kwa mwaka huu.
Kwa upande wa wilaya ya Mkoani zipo barabara sita zinazojumuisha
kilomita 24.1 ikiwemo ya Mbuguwani tironi yenye kilomita 3, Kengeja- Shamiani–
Kiimbini yenye kilomita 4.4.
Mdhamini anabainisha kuwa hata wilaya ya Chake chake kuna
jumla ya kilomita saba za barabara za ndani ikiwemo ya Wesha Mkumbuu yenye
urefu wa kilomita 10 pamoja na Chanjamjawiri –Pujini yenye urefu wa kilomita 4.3.
zinazojumuisha kilomita 29.5.
“Wizara pia ina dhamiria ya kuzijenga barabara 11 zenye
urefu wa kilomita 33.95 kwa wilaya ya Wete ikiwemo ya Kiungoni – Tovuni yenye
urefu wa kilomita 1.5, Mkarafuu mmoja –jumapili kilomita 5.15, Bagamoyo –Kele
kilomita 6.5.
Akisoma
bajeti kuu ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2022/2023 waziri wa wizara hiyo Dk.
Khalid Salum Mohamed amesema wizara imepanga kujenga barabara za ndani zenye
urefu wa kilomita 275.9 Unguja na Pemba, ili kuwaondoshea wananchi changamoto
ya usafiri iliyopo hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini.
Mradi
huo unatekelezwa na Kampuni ya ASER na IRIS kutoka nchini Uturuki na tayari
wizara imekamilisha maandalizi ya ujenzi wa barabara hizo na kazi inayoendelea
ni kuzifanyia usanifu wa michoro barabara zilizopendekezwa katika mradi huo.
Kwa
mujibu wa waziri huyo kazi ya usanifu wa michoro imekamilika kwa barabara ya
Kibonde Mzungu– 18 Mwera kilomita 6.1, Dimani Sokoni – Dimani Beach kilomita
1.5, Kombeni – Nyamanzi kilomita 1, Jumbi – Chuo cha Utumishi (IPA) – Tunguu
(Ringroad) kilomita 5, Kidimni – Ubago kilomita 4.3, Jumbi Sokoni – Kibondeni
Skuli - Hospitali kilomita 4.4, Mgeni Haji – Kwambani kilomita 2.4 pamoja na
barabara ya Cheju – Kibele kilomita 4.1.
Aidha, Barabara ya majaribio kutoka Kibonde
Mzungu hadi Mwera yenye urefu wa kilomita 6.1 tayari ujenzi wake umeanza, hadi
kufikia Machi, 2022 jumla ya shilingi 18,536,160,000 zimepatikana ikiwa ni
malipo ya awali Advance payment ya Mkandarasi kwa mujibu wa mkataba.
Mwisho.
Comments
Post a Comment