NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
ABIRIA wanawake kisiwani Pemba,
wamelalamikia tabia ya baadhi ya madereva wa pikipiki ‘boda boda’ kuwaingia
mwilini wakati wanapokuwepo kwenye vituo vyao, kutaka usafiri wa aina hiyo.
Walisema
mara unapofika kwenye eneo lao la vituo na kutaka usafiri, huvamiwa na kuanza
kukukopea mizigo na wengine kuwashika mikono, wakivutiana kwenye chombo chake.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwenye eneo la Mtuhaliwa wilaya ya Mkoani Pemba,
walisema wamekuwa wakisikitishwa na tabia hiyo.
Mmoja kati
ya wanawake hao aliyekataa jina lake lichapishwe alisema, baadhi ya waendesha
boda boda hao, wamekua wakiwaingia mwilikini, kwa lengo la kufanya ushawishi.
Alieleza
kuwa, kinachowaudhi ni kule kuanza kupokea kuanzia mizigo mikubwa hadi vipochi
vya mkononi, na wengine kukumata mikono.
‘’Ukiteremka
gari tu, wanaaza kukuzonga, wengine wanakupokea hata vipochi vyenye simu, na
wengine wanaanza kukushika shika mikono, wakitaka upande boda bado
yake,’’alisema.
Kazija Issa
Mohamed wa Mwambe alisema, juzi kwenye kituo cha boda boda cha Mtambile-Kengeja
aliangushwa chini, baada ya waendesha boda boda, kuvutia mkoba wake.
Alieleza
kuwa, mara alipoteremka gari akitokea Chake chake, alishuhudia ameshadakwa na
wendesha boda boda, na kuvutwa kwa ghafla mkoba wake na kuanguka chini.
‘’Hawa
waendesha boda boda baadhi yao sio wastaarabu, maana wamekuwa wakituingia
maungoni kutaka abiria, jambo ambalo sio zuri,’’alieleza.
Kwa upande
wake Mmanga Haji Kassim, alisema juzi mume wake aligombana na mwendesha boda
boda eneo la Kenya-Chambani, baada ya kumvamia mke wake.
‘’Ni kweli
waendesha boda boda wengi wao hawana nidhamu, maana mimi juzi kushuka gari
wakati mume wangu yupo na usafiri ananisubiri, yeye ameshanikamata
mkono,’’alilalamika.
Mwendesha
boda boda wa njia ya Mtambile-Kengeja Mohamed Haji, alisema wamekuwa
wakikatazana jambo hilo, ingawa badhi yao wapo watukutu.
‘’Ndio maana
tulitaka tuweka zamu, ili kuepusha hilo, lakini bado hatujakubaliana na ndio
maana, tumekuwa tukishtumiwa kuwafanyia vurugu abiria hasa wa kike,’’alieleza.
Mwendesha
boda boda wa Machomane Chake chake Issa Kassim Issa, alisema nidhamu na
ustaarabu ndio jambo ambalo wamekuwa wakisisitiza kila siku na viongozi.
Mwenyekiti
wa waendesha boda boda mkoa wa kusini Pemba Kassim Juma, aliwataka abiria wanawake
kuripoti katika vyombo vya sheria, wanapogundua kuvunjiwa haki zao.
‘’Hakuna
hata boda boda mmoja, aliyeruhusiwa kumvamia abiria, bali kama kuna zamu ndio
jambo jema kama hakuna, aulizwe kistaarabu,’’alisisitiza.
Hivi
karibuni mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, aliwataka waendesha
boda boda hao, kutojihusisha na kitendo cha aina yoyote, kinachoashiria
uvunjifu wa haki za binadamu.
Kwa sasa
kisiwa cha Pemba kina wastani wa boda boda 300, zikiwemo zile zilizotolewa kwa
njia ya mkopo kutoka kwa Rais wa Zanzibar chini ya benki ya CRDB na wafadhali
wengine.
Mwisho
Comments
Post a Comment