WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali amewashukuru
wananchi wa Kijiji cha Gando Pemba kwa uzalendo wao wa kutoa eneo la ardhi kwa
kikosi cha KMKM kwa ajili ya ujenzi wa
kituo cha Afya.
Kauli
hiyo ameitowa wakati alipoweka jiwe la msingi katika eneo hilo ikiwa ni shamra
shamra za maadhimisho ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kutimiza miaka 59 tangu
yalipotokea mwaka 1964.
Alisema
wananchi wa Kijiji cha Gando wameonesha
moyo wa uzalendo na kueka kando itikadi za kisiasa kwa kutoa eneo lao kuwapa
Kikosi cha KMKM kujenga Kituo cha Afya. hivyo ni jambo jema na la kuwashukuru.
“Hakika
nyinyi ni wana mapinduzi halisi na mmeonesha kwa vitendo jinsi mnavyoshirikiana
na Serikali kuleta maendeleo katika eneo lenu. Nasaha zangu kwa wananchi
wengine Unguja na Pemba kuiga mfano wenu
hasa ikizingatiwa kuwa maendeleo hayana chama, nakushukuruni kwa dhati kwa kutoa
eneo lenu kwajili ya kituo cha afya,”alisema.
Pia aliwashukuru
mafundi na vibarua wa KMKM, kwa hatua waliyofikia katika mradi wa ujenzi kituo hicho
kwa kwenda muda na kwa gharama ndogo kwani bila ya hivyo gharama zingelikuwa kubwa zaidi
kwa Serikali katika kutekeleza mradi huo.
Hivyo waziri
Rahma alimuagiza Komodoo wa KMKM Azana Hassan Msingiri kuwatizama kwa jicho la
huruma mafundi na vibarua waliyofanikisha ujenzi huo ili kuthamini jasho na
uzalendo wao.
Alieleza
kwamba anaamini mradi huo wa kituo cha afya utakapo kamilika huduma bora
zitapatikana kwa askari pamoja na wananchi kama vile ambavyo zinaonekana kwenye
Hospital ya KMKM Kibweni Unguja.
Aidha
alisisitiza umuhimu wa kuwepo vifaa, madaktari, manesi na maodali wa kutosha
kwa mujibu wa mwongozo wa vituo vya afya uliotayarishwa na Wizara ya Afya
Zanzibar katika kituo hicho kitakapoanza kutoa huduma.
Vile vile aliwakumbusha wafikirie umuhimu wa kutoa huduma za mama na mtoto ili
wananchi wa Gando pamoja na vitongoji
vyake wasipate tabu na usumbufu wa kwenda kujifungulia maeneo ya mbali jambo
ambalo litakuwa sio sahihi.
Aidha
alisema hatua ya wananchi kutoa eneo lao inaonesha taswira kwamba wananchi hao
wako tayari kushirikiana na KMKM kutoa taarifa za watu wanaotaka kusafirisha
magendo ya karafuu na magendo mengine ikiwemo uvuvi haramu na uchafuzi wa
bahari hali ambayo itasaidia kuimarika kwa kambi ya KMKM Gando.
“ Kuimarika
kwa kambi hiyo kusaidia Serikali na jamii juu ya uvuvi haramu na uhifadhi wa
bahari yetu. Hivyo basi, ushauri wangu kwenu wanaKMKM mzidishe mashirikiano na
wananchi wa Kijiji cha Gando na vijiji jirani kwani kufanya hivyo kutasaidia
sana ufanisi wa kazi zenu nzito ambapo huwa mnakabiliana na watu ambao
hamuwaoni lakini kwa msaada wa wananchi basi mtawaona”Alisema waziri huyo.
Sambamba
na hayo Waziri Rahama alimuagiza Katibu Mtendaji wa kamisheni ya ardhi Zanzibar
kuwapatia hatimiliki ya eneo hilo ambapo
ombi hilo liliwasilishwa kwa waziri wa
ardhi kupitia risala iliyosomwa awali.
Mwisho
Comments
Post a Comment