NA ZUHURA JUMA, PEMBA:::
MAPINDUZI
ya 1964 chini ya jemedari wake marehemu Abeid Amani Karume, yamekuja kutatua
changamoto za wananchi pamoja na kuimarisha sekta mbali mbali ya kimaendeleo, hapa
nchini.
Miongoni mwa hayo ni kuimarisha huduma za mawasiliano ya
kimtandao, kila kona ya Zanzibar, ili kuhakikisha kwamba wananchi wanafanya
kazi zao vizuri kupitia mawasiliano.
Mawasiliano ya kimtandao ni muhimu, katika maisha ya kila siku
ya mwanadamu, kutokana na kurahisisha kila kitu katika ulimwengu huu wa sasa
kidijitali.
Wanajamii wana msemo wao usemao… ‘dunia kiganjani’ hii
inaonesha dhahiri kwamba mawasiliano ya kimtandao, yamerahisisha kila kitu katika
ulimwengu huu na sasa kuwa kiganja.
Njia mbali mbali zinatumika kuwasiliana kwa sasa,
ukilinganisha na zamani kabla ya Mapinduzi yam waka 1964 ambayo sasa
tunasherehekea miaka 59, ambapo watu walilazimika, kupeleka barua kufikisha
ujumbe ambapo ulikuwa ukichukua muda mrefu.
Lakini kwa miaka hii 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar,
unaweza kufikisha taarifa nchi yeyote kwa sekunde tu na kupata mrejesho papo
hapo (feedback).
Hiyo ni faraja kubwa kwa wananchi wa Zanzibar, wanaotembea
kifua mbele sasa ndani ya miaka hii 59 ya mapinduzi Zanzibar, kwani mawasiliano
ya kimtandao yamekuja kuwarahisishia maisha yao.
Ibrahim Saleh Juma ambae ni Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi Pemba anasema, kutokana na uharaka wa mawasiliano ya
kimtandao, wananchi wanapata kufanya biashara zao mtandaoni, pamoja na
mawasiliano ya moja kwa moja.
Kuna mitandao mbali mbali ambayo hutumiwa kwa mawasliano,
ikiwemo kupiga simu, ambazo kampuni zake zimeekeza kisiwani hapa, kwa lengo la
kuwafanya wananchi kupata mawasiliano popote walipo.
Kuna kampuni kama vile Zantel, Tigo, TTCL, Vodacom, Halotel na
Airtel ambazo mitandao yake ipo vizuri kisiwani hapa na wananchi wanaedelea kuitumia
kila siku.
Kwake anaona miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefanikiwa
kuimarisha huduma ya kiinteneti maeneo yote ya mjini na vijijini, kutokana na kampuni
hizo, kujenga minara ambayo inawezesha huduma hiyo kuingia kila pembe ya kisiwa
hiki.
‘’Kabla ya mapinduzi haya, wazanzibari wenye taifa lao hili
hawakuwa na uhuru wa kuwasiliana, kupata habari, kufikishiana taarifa kwa
wakati kama ilivyo sasa, maana hayo yalikuwa kwa wale watawala,’’anasema.
Mdhamini huyo anaeleza kuwa, mitandao kama kijamii ya whatsApp,
Twitter, facebook na Instagram imekuwa ikiwarahisishia wananchi kutumiana ujumbe
na kufika kwa muda mfupi, jambo ambalo kabla ya Mpinduzi ya Zanzibar halikuwepo.
“Tuna kila sababu ya kujivunia matunda ya Mapinduzi yetu ya
miaka 59, kwa sababu zamani watu walikuwa wanafikisha taarifa kwa kutumia barua
na walikuwa wakisukuma baiskeli kutwa nzima, lakini kwa sasa tuna simu, za
haraka za kufikisha ujumbe”, anasema.
Wakati huo hata gari hazikuwepo nyingi, hivyo inapotokea
dharura kama vile kifo, basi jamaa wa mbali, wanaweza kupata taarifa kuanzia
siku ya tatu na kuendelea.
“Kwa kweli kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964, hali ilikuwa ni
tete ya kimawasiliano, wananchi walikuwa wakihangaika kwa kila jambo, kwa
sababu huduma nyingi, zilikosekana wakati huo”, anafahamisha.
Katika ziara iliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliibua changamoto za mawasiliano
na baada ya hapo, ilipata kujengwa minara 13 mipya.
“Kipindi cha katikati kuna watu kwenyebaadhi ya vijiji,
walikuwa wanapanda hata kwenye miti kutafuta mawasiliano na wengine walikuwa
hata hawajui mawasiliano ni kitu gani”, anahadithia.
Lakini kwa sasa kufikia miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali
imeimarisha eneo hilo la mawasiliano ya kimtandao, hasa kupitia simu za mkononi
na internet.
Anafafanua kuwa, kila kwenye mnara mawasiliano, yanavuta
kutoka kilomita moja hadi kilomita nne masafa yake yanavyokamata, hivyo inawezekana
mtu yupo karibu sana ya mnara na mawasiliano, yakawa ya shida kidogo.
Kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba wapo
masafa ya karibu lakini hawapati mawasiliano vizuri, anasema Mdhamini huyo kuwa,
ni kweli kwa sababu minara hiyo kuanza kukamata zaidi masafa ya mbali kuliko karibu
kwani inavuta juu.
Hivyo, inawezekana wapo watu wachache wanaoweza kupata shida
ya mawasiliano, lakini hayo yanaendelea kerekebishwa na mnara katika eneo
jengine ambao utawanufaisha wao.
“Pia kuna mawasiliano ambayo tunayatumia ya ujazo wa 2G, 3G na
4G lakini kwa sasa tunakwenda kuimarisha kwenye eneo la ujazo wa 5G, hii ni
kuhakikisha kwamba Serikali, ipo mstari wa mbele kuwaimarishia wananchi wake
miundombinu ya mawasiliano”, anaeleza.
Taarifa za kitaalamu zinaonesha kwamba ujazo wa 2G inakamata
watu 200 hadi 300 kwa sekunde, 3G inaunganisha watu kati ya 300 hadi 350 kwa
sekunde na 4G inaunganisha watu kati ya 400 hadi 500 kwa sekunde.
Anasema, katika kisiwa cha Pemba maeneo mengi tayari yana
mawasiliano kwa kiwango kikubwa, ambacho sasa hakimuachi mtu nyuma.
‘’Kama ukitaja matunda ya mapinduzi ya Zanzibar ndani ya miaka 59, basi kwenye mawasiliano sasa jamii iko vizuri, maana mawasiliano ndio kila kitu na sekunde moja ikiwa ikikosekana, kuna hasara,’’anasema.
Anaeleza kuwa, Dk. Mwinyi mara baada ya kuingia madarakani
alifanya ziara maalumu ya kupita maeneo mbali mbali kwenye kisiwa hiki na
kusikiliza wananchi.
Aliibua changamoto mbali mbali ikiwemo ya mawasiliano na
kuwaahidi wananchi kwamba atalifanyia kazi na ndio maana kisiwa hiki kikapata
minara hiyo 13 mipya iliyojengwa na kampuni ya HTC wakishirikiana na kampuni ya
Zantel.
“Minara hiyo tayari imeshakamilika na inaendelea kutoa huduma
za mawasiliano katika yale maeneo ambayo yalikuwa na changamoto kubwa ya
mtandao”, anasema.
Kati ya minara hiyo 13, Wilaya ya Chake Chake ilipata minara
mitano katika maeneo ya Wesha, Vikunguni, Mfikiwa, Shungi na Ngomeni hizo zote
ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wananchi wake
waishi maisha bora.
Kwa Wilaya ya Wete minara hiyo ilijengwa katika maeneo ya
Kangagani, Mchangamdogo, Finya pamoja na Ukunjwi.
Kwa upande wa visiwa tayari wamejenga mnara katika kisiwa cha
Fundo ambao unashika pia katika maeneo ya kisiwa cha Kokota, Funzi na Ukunjwi.
Serikali haijasimama hapo tu, bali itaendelea kuvifikishia
visiwa vyengine huduma hiyo, ili mawasiliano yapatikane bila ya usumbufu.
Anasema, kwa wakati huu wanaendelea kufanya utafiti wa maeneo
ambayo bado kuna shida sana ya mawasiliano ingawa asilimia 90 ya wananchi
wanapata mawasliano bila ya usumbufu.
Aliwaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuiamini
Serikali yao na kushirikiana pamoja, kwani ina malengo makubwa ya kuhakikisha
kila mwananchi pale alipo anapata mawasiliano ya uhakika ambayo hayatakuwa na
shida ya aina yeyote.
Mdhamini anaeleza pia wana mkonga wa taifa ambao unarahisisha
kutoa huduma za mawasiliano za internet katika taasisi za Serikali na jamii kwa
ujumla.
“Kwa Pemba tunavyo vituo vinne vya Tehama, vituo hivi
vinawarahisishia sana wananchi kuweza kurahisisha mambo yao, mfano maombi ya
kazi, kujifunza kuingia kwenye internet na pia tunawapatia mafunzo mbali
mbali”, anafafanua.
Vituo hivyo vya Tehama vimejengwa Machomane Wilaya ya Chake
Chake, Mtambile kwa Wilaya ya Mkoani, Utaani kwa Wilaya ya Wete na Micheweni,
ambapo vinaendelea kutoa huduma ya kupatiwa mafunzo kwa wananfunzi na wananchi
wa kawaida.
Mwanafunzi wa skuli ya Sheikh Idrisa Abdulwakil iliyopo
Kizimbani Wete Raya Suleiman anasema, akimaliza kidato cha nne tu ataenda kituo
cha Tehama Utaani kujifunza vitu mbali mbali, ili atakapoingia chuo asipate
shida.
“Serikali yetu inatupenda sana kwa sababu kama haikuweka vituo
hivi vya Tehama ingebidi tukalipie pesa ya kusomea na wazazi wengine hawana
uwezo kifedha, hivyo inatusaidia sana”, anaeleza.
Mama mmoja mkaazi wa Chasasa Wete, Asha Juma Ali mwenye miaka 66
anasema kuwa, Mapinduzi ya mwaka 1964 yamekuja kuimarisha kila kitu, ikiwemo
hiyo mtandao.
“Zamani ilikuwa hakuna simu wala hayo mambo yenu munayotumia
siku hizi ‘internet’, ilikuwa pakitokea msiba watu wanakwenda kupeleka taarifa
kwa miguu au baskeli, ata watu wakifika maiti ishazikwa”, anasema.
Anaeleza kuwa, yeye binafsi alishawahi kupeleka barua kwenda
mpaka Dar-Es-Salaam, jambo ambalo lilikuwa likiwasumbua sana kwani walikuwa
wanapotezea muda.
Ali Khamis Ali mkaazi wa Kichungwani Chake Chake anasema,
mawasiliano ndio yaliyorahisisha kila kitu, kwa sababu watu mpaka biashara zao kwa
sasa wanafanya kwenye mitandao.
“Mitandao ni kitu muhimu sana, kwa sababu dakika tu
ikikosekana kwa dharura kama ikiwa kwenye matengenezo, basi tunalalamika, kwa
kweli inatusaidia sana”, anaeleza.
Mkaazi wa Micheweni Suleiman Faki Hamad anasema kuwa, bila ya
kuwepo kwa mtandao kwa maisha ya sasa hayawezi kwenda, kwa sababu hata
unapokwenda sehemu kama huijua, ukiwa na simu tu basi hupotei.
Mfanyabiashara anaetumia mitandao kuuza bidhaa zake ambae
hakutaka jina lake litajwe mkaazi wa Chake Chake anasema, amekuwa akiingiza
mapato kupitia mitandao, kwani biashara inafanyika vizuri.
“Unapoweka bidhaa zako mtandaoni watungi wanaona, hivyo ni
rahisi kuuza mara moja na kuingiza mzingo mwengine, mawasiliano
yameturahisishia kila kitu kwa kweli”, anaseama.
Januari 12 mwaka 2023 wananchi wa Zanzibar wanaadhimisha miaka
59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar yakiongozwa na Rais wa awamu ya nane Dk.
Hussein Ali Mwinyi ambae anaendeleza kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo
katika sekta zote.
MWISHO.
Comments
Post a Comment