NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
WANANCHI
6,680 wa shehia ya Shumba mjini wilaya ya Micheweni Pemba, waliokuwa wakikabiliwa
na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa muda wa mwezi mmoja, sasa
huduma hiyo, imerejea kama kawaida.
Itakumbukwa kuwa, Novemba
20, mwaka 2022, blog hii https://pembatoday.blogspot.com/2022/11/shumba-pemba-watumia-maji-ya-bahari-kwa.html
ilichapisha habari ikielezea tatizo la ukosefu wa huduma hiyo kwa wananchi hao.
Walisema, huduma hiyo kwa
sasa imerudi kama asili yake, baada ya huduma ya nishati ya umeme, nayo kurudi
kama kawaida hasa kwenye kisima chao cha maji safi na salama kilichopo Shumba
wilayani humo.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi kupitia blog hii, walisema huduma hiyo imerejea vyema, baada ya blog
ya pemba today kuripoti ukosefu huo mwezi mmoja uliopita.
Walisema kabla ya kurejea
kwa huduma hiyo, awali walilazimika kununua kwa dumu moja lenye ujazo la lita
20, kati ya shilingi ya 500 hadi shilingi 1,000, kutoka shehia za Micheweni.
Wananchi hao wa vijiji vya Chamboni,
Vumbini, Nduaga, Momogu, Mkunguni, Kichekwani, Tundumwe na Msasani kwa wale
wasio na uwezo walilazimika kutumia maji ya bahari, kwa shughuli nyingine.
Mmoja kati ya wananchi hao
Hamad Ali Hamad, alisema kwa sasa wanaishi kwenye furaha na kujipangilia vyema
kazi zao, baada ya huduma hiyo kurejea.
‘’Ni kweli, kwa sasa huduma ya
maji safi na salama imeanza kurejea na hili tulipofuatilia tuliambiwa ni baada
ya huduma ya nishati ya umeme kurejea kama kawaida,’’alisema.
Nae Kurata Bakar Said,
alisema huduma hiyo ya maji safi na salama, imekuwa nzuri sasa, na imewarahisishia
kupanga na kuendesha shughuli zao mbali mbali.
Kwa upande wake Fatma
Mohamed Awadhi, alisema maji ya ‘ZAWA’ sasa yamerudi na wanalishukuru shirika
la Umeme la Zanzibar ZECO kwa kuituliza huduma ya umeme.
‘’Mwezi mmoja nyuma ilikuwa
unaweza kukaa wiki ukasikia maji eneo fulani yanatoka, lakini ukifika unaweza
kubahatika ndoo moja au mbili, na kisha yanafungwa, lakini sasa twashukuru,’’alifafanua.
Nao wananchi Omar Khamis
Kombo na Biache Mohamed Hamad walisema, sasa kama imerejea ni vyema wenzao
wakaitumia kwa uangtalifu sambamba na kuyalinda miundombinu husika.
Sheha wa shehia ya Shumba Mjini mjini Rahila
Ramadhan Juma, alikiri kuwa sasa malalamiko ya wananchi wake, juu ya ukosefu wa
huduma hiyo, hayapo tena.
Alisema anaelewa kuwa, kwa
zaidi ya siku 30, baadhi ya wanachi hawakuwa wakiipatia kabisa huduma hiyo, na
baadhi ya maeneo yakitoka huwa ni kwa kusua sua.
‘’Kwa hakika, huduma ya maji
safi na salama ndani ya shehia yangu, ilikuwa tatizo, lakini sasa imerejea kama
zamani, twaamini kilio chetu kimesikika,’’alieleza.
Afisa wa Mamlaka ya Maji ‘ZAWA’
wilaya ya Micheweni Ali Rajab, awali alikiri kupokea malalamiko ya sheha huyo,
juu ya huduma hiyo kuwa ndogo, ingawa kwa sasa imekaa pahala pake.
Alieleza kuwa, tatizo hilo
halitokani na uhaba wa huduma ya maji kwenye kisima wanachokokitegemea cha
Kijichame, bali ilikuwa ni kupanda na kushuka kwa nishati ya umeme.
Hata hivyo afisa huyo,
alisema kuwa kisima hicho ambacho kinauwezo wa kuzalisha lita 17,000 kwa saa
moja, na kuwekwa bomba lenye ujazo wa nchi tatu.
Afisa Uhusiano wa ‘ZAWA’
Pemba Suleiman Anasi Massoud, alisema mashine iliyopo kwenye kisima
wananchokitegemea wananchi hao wa Shumba, kilipata hitilafu ya umeme kwa kule
kupanda na kushuka.
‘’Mshine iliyopo kwenye
kisima hicho ni ya kisasa, hivyo kama umeme ukiwa mkubwa au mdogo kama ilivyokuwa,
hujizima wenyewe na kukosa nguvu ya kusukuma maji,’’alieleza.
Hata hivyo, alisema
changamoto kubwa ambayo ipo kwa wananchi hao, ni ukosefu wa tenki la kuhifadhia
maji, ambapo hilo huisababishia mashine iliyopo, kufanyakazi kwa saa 24 bila ya
mapumziko.
Afisa Mawasiliano na Huduma kwa wateja wa Shirika
la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ Pemba Haji Khatib Haji, hivi karibuni alinukuliwa na
vyombo vya habari, akisema tatizo la kupungua kwa umeme ovyo ovyo, kutokana na
eneo la Tanga kupata hitilafu.
Hivi karibuni, kwenye
kongamano la kutimiza miaka miwili ya rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi,
ilifahamika kuwa, kwa Pemba kuna vituo 27 vya huduma ya maji safi na salama na
ujenzi wa matenki matano (5), yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 1,
kila moja.
Mwisho.
Comments
Post a Comment